The chat will start when you send the first message.
1Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, nyinyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana?[#9:1 Paulo ndiye aliyelianzisha kanisa la Korintho. Rejea 1Kor 3:6.]
2Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu nyinyi mimi ni mtume. Nyinyi ni uthibitisho wa utume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana.
3Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii:
4Je, hatuna haki ya kula na kunywa?[#9:4 Rejea Luka 10:7. Katika sura hii kwa jumla Paulo anatamka kwamba anayo haki ya kupata faida fulanifulani zinazoandamana na kazi ya kuwa mtume; hata hivyo aliachilia haki hizo kwa faida ya Habari Njema (aya 12,15,18; 2Kor 11:9; 1Thes 2:7).]
5Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa?[#9:5 Taz Mat 12:46 maelezo. Yakobo ni mmoja wa hao ndugu zake Bwana (Mat 13:55; Marko 6:3; Gal 1:19).; #9:5 1Kor 1:12 maelezo.]
6Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi?[#9:6 Rejea Mate 4:36-37; 13—15.]
7Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake?
8Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo?
9Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe?[#9:9 Kumb 25:4. Inanukuliwa pia katika 1Tim 5:18.]
10Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno.
11Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia?
12Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao?
Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo.
13Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka?
14Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo.
15Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure.
16Ikiwa ninaihubiri injili, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri injili!
17Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze.
18Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.
19Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo.
20Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya sheria, nimejiweka chini ya sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya sheria.
21Na kwa wale walio nje ya sheria, naishi kama wao, nje ya sheria, ili niwapate hao walio nje ya sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo.
22Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia.
23Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, nipate kushiriki baraka zake.
24Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi?[#9:24-27 Hapa Paulo anachukua fursa ya matukio ya michezo ya wanariadha; Wagiriki na Waroma walithamini sana michezo ya riadha. Kila miaka mitatu walifanya michezo ya Olimpiki na kila miaka mitatu ilifanyika huko Korintho. Rejea Fil 3:14; 2Tim 4:7. Kutokana na hayo Paulo anachukua picha ya maisha ya waumini ambao daima lazima wawe mbioni kushinda maisha ya kiroho.]
25Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji isiyoharibika.[#9:25 Taji waliopata washindi ilikuwa ya dhahabu; na Paulo anatamka kwamba taji ya waumini ni ya namna isiyoharibika.]
26Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani.
27Naupa mwili wangu mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili, nisije mimi mwenyewe nikakataliwa baada ya kuwahubiria wengine.