The chat will start when you send the first message.
1Solomoni alifanya ushirikiano na Farao mfalme wa Misri, kwa kumwoa binti yake. Akamleta binti Farao na kumweka katika mji wa Daudi, mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake mwenyewe, nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ukuta wa kuuzunguka mji wa Yerusalemu.[#3:1 Ndoa ya mfalme na binti mfalme wa kigeni, jambo ambalo lilifanyika mara kwa mara, ilisimika uhusiano wa kisiasa na wa urafiki kati ya tawala hizo. Rejea 1Fal 11:1; 16:31; 2Fal 8:18.]
2Kabla yake, watu walikuwa wakitoa tambiko vilimani, kwa kuwa nyumba ya Mungu ilikuwa bado haijajengwa.[#3:2 Mahali pengi pa kutambikia pa Waisraeli kulikuwa kwenye vilima mahali ambapo miungu ya mataifa mengine ilikuwa inaabudiwa. Kutokana na jambo hilo desturi ambazo hazikupatana na ibada ya Mungu wa kweli ziliingia kwa Waisraeli, desturi hizo zilipigwa vita sana na kulaumiwa na manabii (rejea Eze 20:28-29; Hos 10:8; Amo 7:9). Wengine waliopinga desturi hizo ni mfalme Hezekia (2Fal 18:4) na hasa mfalme Yosia (2Fal 23:4-15). Katika Hes 33:52; Kumb 7:5 na 12:3 mahali hapo pote pa kutambikia ilibidi paharibiwe na kwamba mahali pa kumwabudu Mungu pawe pale tu ambapo Mungu angepachagua (Kumb 12:5-19).]
3Solomoni alimpenda Mwenyezi-Mungu, akazingatia maongozi ya Daudi, baba yake; ila tu, naye ilimbidi kutoa tambiko na kufukiza ubani vilimani.
4Wakati mmoja, Solomoni alikwenda kutoa tambiko huko Gibeoni, maana palikuwa ndipo mahali maarufu pa ibada. Ilikuwa ni kawaida ya Solomoni kutoa maelfu ya sadaka za kuteketezwa katika madhabahu hiyo.[#3:4 Mahali katika eneo la kabila la Benyamini, yapata kilomita tisa Kaskazini mwa Yerusalemu.]
5Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.”[#3:5 Ndoto katika A.K. zilikuwa njia kawaida za kupata ufunuo wa ki-Mungu (rejea Mwa 26:24; 28:11-15; 31:11,24; Amu 7:13; 1Sam 3; 28:6).; #3:5-9 Kwa kuomba hivyo, mfalme Solomoni anadhihirisha kwamba ukuu wa mfalme si kuhusu mamlaka yake ila ni kule kuwa tayari kuhudumu kwa faida ya watu wake. Taz Zab 72:1-2.]
6Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi.
7Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu.
8Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao.
9Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi?”
10Ombi hili la Solomoni lilimfurahisha Mwenyezi-Mungu,
11naye akamwambia, “Kwa kuwa umetoa ombi hili, na hukujiombea maisha marefu au mali, na wala hukuomba adui zako waangamizwe, bali umejiombea utambuzi wa kutoa hukumu au kutenda haki
12basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako.[#3:12 Watu wa Agano la Kale kama vile mataifa mengine mengi jambo la kuwa na hekima ni jambo muhimu sana hasa kwa viongozi ambao wanaihitaji sana kuwaongoza watu wao na kuweka mpango mzuri katika jumuiya.]
13Pia, nitakupa yale ambayo hukuomba: nitakupa utajiri na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote wa nyakati zako.
14Tena kama ukifuata njia na maagizo yangu na kushika amri zangu kama alivyofanya baba yako Daudi, basi, nitakupa maisha marefu.”
15Solomoni alipoamka, alitambua kwamba ilikuwa ndoto. Ndipo akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, akamtolea tambiko za kuteketezwa na za amani. Halafu akawafanyia karamu watumishi wake wote.
16Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni.
17Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani.
18Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu.
19Halafu, usiku mmoja, mtoto wake alifariki kwa sababu alimlalia.
20Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu.
21Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.”
22Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme.
23Ndipo mfalme Solomoni akasema, “Kila mmoja wenu anadai kwamba, mtoto wake ndiye aliye hai na kwamba aliyekufa si wake.”
24Basi, mfalme akaagiza: “Nileteeni upanga!” Wakamletea mfalme upanga.
25Mfalme akasema: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, umpe mmoja nusu na mwingine nusu.”
26Yule mwanamke aliyekuwa mama yake huyo mtoto aliye hai alishikwa na huruma juu ya mwanawe, akamwambia mfalme, “Tafadhali mfalme, msimuue mtoto. Mpe mwenzangu huyo mtoto aliye hai, amchukue yeye.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “La! Mtoto asiwe wangu wala wake. Mkate vipande viwili.”
27Mfalme Solomoni akasema, “Usimuue mtoto! Mpe mwanamke wa kwanza amchukue, kwani yeye ndiye mama yake.”
28Watu wote wa Israeli waliposikia juu ya hukumu ya mfalme, walimwogopa, wakatambua kwamba alikuwa na hekima ya Mungu iliyomwezesha kutoa hukumu.[#3:28 Hadithi hii ya 3:16-28 inadhihirisha jinsi watu wa Biblia walivyoielewa hekima. Hekima ni kipaji cha kuweza kujua mambo ya ndani ya mtu, mambo ambayo ni Mungu tu peke yake anayeyajua, ili kuweza kutenda yaliyo sawa hasa katika kuwaongoza watu na kuwaamulia mambo yao.]