The chat will start when you send the first message.
1Kisha mfalme Nahashi, wa Waamoni. alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.”[#10:27—11:1 Tafsiri ya aya hizi mbili ni kulingana na makala ya Kiebrania. Lakini hati za Kumrani zilizogunduliwa karibu na Bahari ya Chumvi zina: “Mfalme Nahashi wa Amoni aliwadhoofisha watu wa Gadi na Reubeni. Alimng'oa kila mwanamume jicho lake la kulia na hakuna mtu ye yote katika Israeli aliyemzuia. Alimng'oa jicho lake la kulia kila mwanamume Mwisraeli aliyeishi magharibi ya mto Yordani. Ni wanaume elfu saba tu walitoroka kwa Waamoni wakaenda katika mji wa Yabeshi katika Gileadi. Yapata mwezi mmoja baadaye …”.; #11:1 Waamoni walikuwa wazawa wa Loti (taz Mwa 19:38; Kumb 2:19) na waliishi mashariki ya eneo la kabila la Gadi katika sehemu za miinuko ya mto Yaboki (taz Kumb 2:37; Yos 12:2).; #11:1 Mji uliokuwa Mashariki ya Yordani katika eneo la kabila la Manase, yapata kilomita 72 kaskazini ya Bahari ya Chumvi au kilomita 36 kusini ya Ziwa Galilaya.]
2Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamng'oa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.”[#11:2 Licha ya kwamba kitendo hicho kikatili kilikuwa cha kuaibisha, kwa upande mwingine pia kiliwadhoofisha maadui kwani waliohusika hawakuweza kupigana vita kwa kutumia ngao na upanga. Taz pia Amu 1:6.]
3Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.”
4Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti.
5Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi.
6Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali.
7Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja.[#11:7 Au: “Mwenyezi-Mungu” aliwatia hofu Waisraeli.]
8Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda.[#11:8 Kule kutaja “Israeli” na “Yuda” hapa wakati huu, inaonesha kwamba maandishi haya yalikamilika kuandikwa baada ya kugawanyika utawala wa kifalme wa Waisraeli katika utawala wa kaskazini (wa Israeli) na wa kusini (wa Yuda). Rejea 1Fal 12:1-25.]
9Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana.
10Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.”
11Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja.
12Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.”
13Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.”
14Samueli akawaambia, “Twendeni wote Gilgali na kwa mara nyingine tutamtangaza Shauli kuwa mfalme.”
15Watu wote wakaenda Gilgali, na walipofika huko, wakamtawaza Shauli kuwa mfalme mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani hapo. Na Shauli pamoja na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.[#11:15 Rejea Lawi 3.]