The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo.[#1:1 Paulo anawataja hawa wawili: Silwano ambaye anaitwa pia Sila, (taz Mate 15:22 maelezo), na Timotheo (taz Mate 16:1 maelezo) ambao waliandamana naye wakati alipokuwa anaunda jamii ya Kikristo kule Thesalonike na pia kwa sababu hawa wawili walikuwa wanajulikana sana huko Thesalonike. Walikuwa na Paulo katika mji huo wa Makedonia (taz 1Thes 1:7 maelezo). Kuhusu kuanzishwa kwa Kanisa la Thesalonike, taz Mate 17:1-9.]
Tunawatakieni neema na amani.
2Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu.[#1:2-10 Kama kawaida ya barua zake, Paulo hapa ana maneno ya salamu pamoja na shukrani kwa Mungu, na kwa kiasi fulani wazo hilo linarudiwa pia mwishoni mwa sura ya 3.]
3Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti.[#1:3 Aya hii ina makala ya kale kupita zote katika barua za Paulo ambamo anaeleza hali tatu muhimu na za msingi katika maisha ya Kikristo. Hali hizo tatu zinatajwa hapa pamoja na sifa za kila moja: imani inayodhidhirika kwa matendo; upendo katika kufanya kazi au kuhudumia wengine; na matumaini ambayo yanasababisha uthabiti au uvumilivu.]
4Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake,
5maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.[#1:5 1Kor 2:4-5.]
6Nyinyi mlifuata mfano wetu, mkamwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.[#1:6 1Kor 4:16; 11:1; Fil 3:17.; #1:6 Mate 17:5-9. Taz pia 1Thes 2:14; 3:3; 2Thes 1:4.; #1:6 Neno “furaha” ni neno muhimu sana katika barua za Paulo na pia katika sehemu nyingine za A.J. (taz k.m. Rom 12:12; 15:13,32; 2Kor 7:4; 8:2; Gal 4:27; Fil 1:4,25; 2:17-18,29; 3:1; 4:4,10; Luka 10:21; Mate 8:8; Ebr 12:2; 1Pet 1:8). Aidha “furaha” ni jambo linaloandamana na Habari Njema. Wote wanaoiamini hiyo Habari Njema juu ya Yesu Kristo ni watu wenye furaha na heri. Hali hiyo ya furaha si matokeo ya bidii ya mtu ila ni zawadi ya Roho Mtakatifu (Rom 14:17; Gal 5:22).]
7Kwa hiyo nyinyi mmekuwa mfano mzuri kwa waamini wote wa Makedonia na Akaya.[#1:7 Hii ilikuwa mikoa miwili ya Kiroma ambayo ilikuwa Kaskazini na Kusini mwa nchi ya Ugiriki. Mji mkuu wa Akaya ulikuwa Korintho; Paulo aliandika Barua hii akiwa huko.]
8Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si huko Makedonia na Akaya tu, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.
9Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu, mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli,[#1:9 Wengi wa watu walioupokea Ukristo huko Thesalonike hawakuwa Wayahudi na kwa jumla walisifika kwa kuwa na miungu yao na sanamu zao (taz Mate 17:4).]
10na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, yaani Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.[#1:10 Mat 10:23; 13:41; 24:27,30; Luka 17:24. Wakristo wa kwanza waliamini kuwa Yesu Kristo alikuwa amekaa upande wa kulia wa Mungu mbinguni (Mate 2:34; Rom 8:34; Ebr 8:1; 10:12) na kwamba angekuja tena duniani punde si punde (taz 2:19; 5:23; 1Kor 1:7; 7:31; Fil 4:5; Tito 2:13; 1Pet 4:7).; #1:10 Kifo na ufufuo wake Yesu Kristo ni kitovu cha mahubiri ya Paulo na ya Kanisa la mwanzo (taz Mate 3:16; 1Kor 2:2; 15:1-58; 1Pet 3:18).; #1:10 Au, “adhabu kali … inayokuja”.]