The chat will start when you send the first message.
1Usimkemee mwanamume mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana wa kiume kama ndugu zako,[#5:1 Hapa neno “mzee”, tofauti na mazingira kama yale ya Tito 1:5 ambapo neno hilo latumika kuhusu baadhi ya watu ambao walikuwa na madaraka katika kanisa, linatumika kuhusu mtu wa umri mkubwa. Katika aya ya pili wanatajwa pia “wanawake wazee”. Rejea pia Tito 2:2-3.]
2wanawake wazee kama mama zako, na vijana wa kike kama dada zako, kwa usafi wote.
3Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli.[#5:3 Yaani, wasio na wa kuwasaidia; rejea Mate 6:1.]
4Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu.
5Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana.
6Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai.
7Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama.
8Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini.
9Usimtie katika orodha ya wajane mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu,[#5:9 Ionekanavyo katika maelezo ya aya 9-10 si orodha ya kawaida hii kama wajane waliotajwa katika aya ya 3-5. Inaonekana kwamba yahusu kikundi cha pekee cha wajane kilichokuwa na majukumu fulani katika kanisa na ambacho wanachama wake walikuwa wametoa ahadi (aya 12) pamoja na ahadi ya kutoolewa mara ya pili (1Tim 3:2 maelezo).]
10na awe mwenye sifa nzuri: aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema.[#5:10 Huduma inayotajwa kama ishara ya unyenyekevu na ukarimu; taz Yoh 13:2-11 maelezo, na 13:14 maelezo.]
11Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena,[#5:11-12 Taz 5:9 maelezo.]
12na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali.
13Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema.
14Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu.
15Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani.
16Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.[#5:16 Hati nyingine zina: “Kama mwanamume”, na nyingine chache zina: “Kama mwanamume au mwanamke”.]
17Viongozi wa kanisa wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha.[#5:17 Hawa yamkini ni wale wale wanaotajwa katika 1Tim 3:1-7 (na katika Tito 1:5).]
18Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka,” na tena “Mfanyakazi astahili malipo yake.”[#5:18 Kumb 25:4; rejea 1Kor 9:9.; #5:18 Maneno sawa na yale aliyosema Yesu katika Luka 10:7 (rejea Mat 10:9-10). Paulo anagusia maneno hayo hayo katika 1Kor 9:14.]
19Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu.
20Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa.
21Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu na mbele ya malaika watakatifu, uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda.
22Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi.[#5:22 Tafsiri hii imesema wazi maana ya kitendo hicho hapa, yaani: “kwa ajili ya kumtumikia Bwana” (taz 1Tim 4:14 maelezo, na rejea 2Tim 1:6). Baadhi wanafikiri maana ya kitendo hicho hapa ni kumpatanisha mtu na jumuiya ya kanisa baada ya huyo mtu ambaye alikuwa ametengwa kubadili mwenendo wake.]
23Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.[#5:23 Divai katika sehemu hizo zilizopakana na Bahari ya Mediteranea ilikuwa kinywaji cha kawaida katika chakula na karamu (rejea Yoh 2:1-10) na ilifikiriwa pia kuwa ni kitu kilichosaidia kuyeyusha chakula tumboni na kuleta nafuu katika baadhi ya magonjwa. Hata hivyo, utumiaji wake usio na kipimo ulilaaniwa vikali (rejea Meth 20:1; 23:29-35; 1Kor 11:21-22).]
24Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi, nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye.
25Vivyo hivyo, matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika.