The chat will start when you send the first message.
1Solomoni, mwanawe mfalme Daudi, alijiimarisha katika utawala wake, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wake alikuwa pamoja naye, akambariki na kumfanya awe mkuu sana.[#1:1 Mwandishi wa simulizi hili mara nyingi hutumia maneno kama haya kuonesha ushindi wa mfalme baada ya shida au magumu fulani (12:13; 13:21; 17:1; 25:11; 27:6). Bila kukubali moja kwa moja, mwandishi anatambua kwamba utawala wa Solomoni ulikuwa wa mapambano ingawa hataji kinaganaga yale yanayotajwa katika 1Fal 2.; #1:1 Taz 15:9 maelezo.; #1:1-17 Kisehemu hiki kinaendana na sehemu moja sambamba ambayo inasema juu ya utajiri wake Solomoni (9:13-28).]
2Mfalme Solomoni aliwaita makamanda wote wa vikosi vya maelfu na vya mamia, waamuzi, na viongozi wote wa koo za Israeli.
3Kisha akaandamana nao hadi mahali pa ibada huko Gibeoni. Walikwenda huko kwa sababu hapo ndipo mahali lilipokuwa hema la mkutano la Mungu alilolitengeneza Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, nyikani.
4(Lakini, sanduku la Mungu lilikuwa Yerusalemu katika hema ambalo mfalme Daudi alilipigilia alipolileta kutoka Kiriath-yearimu).
5Tena, madhabahu ya shaba iliyotengenezwa na Bezaleli, mwana wa Uri na mjukuu wa Huri, pia ilikuwa huko Gibeoni mbele ya hema takatifu la Mwenyezi-Mungu. Hapo mfalme Solomoni na watu wote wakamwomba Mwenyezi-Mungu.[#1:2-5 “Gibeoni” ulikuwa katika eneo la kabila la Benyamini, yapata kilomita kumi kaskazini-magharibi ya Yerusalemu. Mji huo ulijulikana pia kama “Gibea”. “Hema la Mkutano” ambalo ndani yake kulikuwa na sanduku la agano ambalo lilichukuliwa kama kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu Mwenye Nguvu lilikuwa huko kabla ya mfalme Daudi kulileta Yerusalemu. Tunaambiwa katika aya ya 5 kwamba huko pia kulikuwa na mahali pa kutambikia au madhabahu ambayo ilitengenezwa na Bezaleli ambaye alikuwa fundi stadi (Kut 31:1-11).]
6Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo.
7Usiku huo, Mungu alimtokea Solomoni, akamwambia, “Omba chochote, nami nitakupa.”[#1:7 Kama vile katika 1 Wafalme, mwandishi wa 2Nya kati anasema kwamba Mungu aliongea na Solomoni kwa njia ya ndoto (taz pia 7:12 na 1Fal 3:5).]
8Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake.[#1:8 Kwa kusema hivyo Solomoni anaonesha dhahiri mtazamo wa wadhifa wa mfalme kwamba amechaguliwa na Mungu kutekeleza matakwa yake.]
9Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi.[#1:9 Mungu aliahidi kwamba kutakuwa daima na mzawa wa Daudi ambaye angewatawala watu wake. Rejea 2Sam 7:10-16; 1Nya 17:7-14.; #1:9 Mwa 13:16; 28:14.]
10Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?”[#1:10 Fahari ya utawala wa Solomoni ni matokeo ya hekima aliyopewa na Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya kuwaongoza watu wake (rejea pia 1Fal 3:9; ling Hes 27:17; Kumb 31:2; Zab 119:34,73; Meth 3:13; Yak 1:5). Hekima ya Solomoni ilikuwa kama mfano uliotangulia wa hekima ya Yesu Kristo ambaye kwa ukamilifu kamili alikuwa hekima ya Mungu (Isa 11:1-2; Kol 2:3).]
11Mungu akamjibu Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili uliloomba limo moyoni mwako, na wala hukuomba mali, wala utajiri, wala heshima wala hukuomba wanaokuchukia waangamizwe, wala maisha marefu, lakini umeomba hekima na maarifa ili uwatawale vizuri watu wangu ambao nimekupa uwe mfalme wao,
12ninakupa hekima na maarifa. Pia, nitakupa utajiri, mali na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote aliyekuwako kabla yako na mfalme mwingine yeyote atakayetawala baada yako.”
13Basi, Solomoni aliondoka mahali hapo pa kuabudia, huko Gibeoni, lilipokuwa hema la mkutano, akarudi Yerusalemu. Akaitawala Israeli.
14Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi; alikuwa na magari ya farasi 1,400, na wapandafarasi 12,000, ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi na kwake katika Yerusalemu.[#1:14 Haya yalikuwa magari ambayo yalikuwa wazi upande wa nyuma na yalikokotwa na farasi. Kwa kawaida wakati huo yalitumiwa vitani. Kuwa na farasi wengi ilikuwa ni ishara ya utajiri. Taz 1Sam 8:11-12; 1Fal 4:26; Yobu 39:21-25.]
15Mfalme Solomoni aliongeza fedha na dhahabu zikawa nyingi kama mawe katika Yerusalemu, na mbao za mierezi zikapatikana kwa wingi kama mikuyu ya Shefela.[#1:15 Jina “mwerezi” hapa linatafsiri mti ambao uliota kwa wingi kaskazini ya Palestina kwenye eneo ambalo sasa ni nchi ya Lebanoni. Miti ya namna hiyo kwa karibu sana ni kama miti ya mikangazi ambayo ni miti migumu na yenye kufaa sana kwa kujengea na ambayo, tofauti sana na miti ya mierezi kama tuijuavyo, iliweza kustahimili uharibifu wa wadudu. Miti hiyo ilikuwa na rangi ya kupendeza na harufu nzuri.]
16Farasi wa Solomoni walitoka Misri na Kilikia; wafanyabiashara wake waliwanunua huko.
17Walinunua gari moja la farasi kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha, na farasi mmoja kwa shekeli 150 za fedha. Kisha waliwauzia wafalme wa Wahiti na Shamu farasi hao na magari.