The chat will start when you send the first message.
1Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu, ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme.[#10:1 Mji katika nchi ya Efraimu karibu na mpaka wa nchi ya Manase. Huko kulikuwa mahali pa kuabudia Mwenyezi-Mungu na mahali wafalme kadhaa walipotawazwa (rejea Mwa 12:6; 33:18-20; Yos 17:7; 1Fal 12:1,25). Yusufu alizikwa huko (rejea Yos 24:32). Kuhusu mji huu, rejea pia Amu 8:31; 9:6,45; 21:19; 1Fal 12:25; 1Nya 7:28; Yer 41:5; Zab 60:6.]
2Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (wakati huo alikuwa bado anaishi Misri alikokwenda alipomkimbia Solomoni) alitoka Misri.
3Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na Waisraeli wote walimwendea Rehoboamu na kumwambia,
4“Baba yako alitutwika mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.”
5Rehoboamu akawajibu, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” Basi wakaondoka.
6Baadaye, Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa Solomoni, baba yake, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?”
7Wazee hao wakamjibu, “Ukiwahurumia watu hawa, ukiwafurahisha na kusema nao maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako daima.”
8Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee na badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake.
9Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia, ‘Punguza mzigo ambao baba yako alitutwika?’”
10Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia ‘Baba yako alitutwika mzigo mzito, lakini wewe utupunguzie,’ wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo cha mwisho ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu.[#10:10 Huu ni msemo mithili ya methali. Tafsiri nyingine yamkini: “Kama baba yangu alikuwa mkali kwenu mimi nitakuwa mkali zaidi” Au, “ukilinganisha, baba yangu alikuwa dhaifu kuliko mimi”.]
11Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”[#10:11 Makala ya Kiebrania hapa ina: “nitawapiga kwa nge”.]
12Basi katika siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza.
13Naye mfalme Rehoboamu akawajibu kwa ukali, akapuuza shauri la wazee,
14na kufuata shauri la vijana wenzake. Basi akasema, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba”
15Hivyo mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mungu ili Mwenyezi-Mungu atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati kwa njia ya Ahiya wa Shilo.
16Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali walimwambia,[#10:12-19 Hapa mwandishi anamaanisha makabila kumi ambayo yalijumuika kufanya utawala wa Kaskazini na tangu wakati huu maneno “watu wa Israeli” yatakuwa yanatumiwa kumaanisha utawala huo wa Kaskazini, hali maneno, “watu wa Yuda” yatakuwa yanatumiwa kumaanisha utawala wa kusini.]
“Tuna sehemu gani kwa Daudi?
Hatuna urithi katika mwana wa Yese.
Kila mmoja na arudi nyumbani kwake, enyi watu wa Israeli.
Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.”
Hivyo watu wote wa Israeli wakarudi makwao.
17Lakini Rehoboamu alitawala watu wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda.
18Kisha mfalme Rehoboamu alipomtuma Hadoramu aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Ndipo Rehoboamu alipopanda gari lake haraka akakimbilia Yerusalemu.
19Hivyo, watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya maasi dhidi ya utawala wa ukoo wa Daudi mpaka leo.