2 Mambo ya Nyakati 16

2 Mambo ya Nyakati 16

Yuda na Israeli zafarakana

(1 Fal 15:17-22)

1Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa mfalme Asa, Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga mji wa Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.[#16:1 Alitawala yapata mwaka 909-886 K.K. Kuhusu mfalme huyu Baasha, rejea pia 1Fal 15:33—16:7.; #16:1 Mji katika eneo la Benyamini, yapata kilomita nane kaskazini ya Yerusalemu.]

2Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, akazituma Damasko kwa Ben-hadadi, mfalme wa Aramu na ujumbe akasema,[#16:2 Anayetajwa hapa ni Ben-hadadi I. Kulikuweko Ben-hadadi II (rejea 1Fal 20:1-34; 2Fal 6:24; 8:7-15) na Ben-hadadi III (rejea 2Fal 13:3; Yer 49:27). Kitendo cha Asa cha kuchukua hazina ya hekalu na kumpelekea Ben-hadadi kilikuwa makosa kwa namna mbili: kwanza ni kuonesha dharau kwa nyumba ya Mungu (rejea 28:21); pili, kufanya mkataba na wenye nguvu wa kigeni na kutumia hazina hiyo kwa ajili hiyo kulionesha kwamba yeye anategemea zaidi nguvu za binadamu kuliko kumtegemea Mungu.]

3“Na tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama nakupa zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli ili aache mashambulizi dhidi yangu.”

4Hapo mfalme Ben-hadadi alikubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao waliiteka miji ya Iyoni, Dani, Abel-maimu, na miji yote ya Naftali iliyokuwa na ghala za vyakula.

5Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo, aliacha kuujenga mji wa Rama, akasimamisha kazi yake.

6Ndipo mfalme Asa alipowapeleka watu wote wa Yuda, wakahamisha mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha Asa alitumia vifaa hivyo kujengea miji ya Geba na Mizpa.

Mwonaji Hanani

7Wakati huo, Hanani mwonaji alimwendea mfalme Asa wa Yuda, akamwambia, “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Shamu badala ya kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Shamu limekuponyoka.[#16:7 Hapa Hanani anaitwa “mwonaji” kama wengine walivyoitwa: Samueli (1Sam 9:9, 11,18-19), Gadi (2Sam 24:11; 1Nya 21:9; 2Nya 29:25), Hemani (1Nya 25:5), Ido (2Nya 9:29), Asafu (2Nya 29:30), Yeduthuni (2Nya 35:15).]

8Je, wale Waethiopia na Walibia hawakuwa jeshi kubwa na magari na wapandafarasi wengi? Lakini kwa vile ulimtegemea Mwenyezi-Mungu, yeye aliwatia mikononi mwako.[#16:8 Au, “Wakushi”. Rejea 2Nya 14:9-15.; #16:8 Hawa hawatajwi katika 2Nya 14:9-15. Walikuwa watu walioishi eneo la kaskazini la Afrika.]

9Mwenyezi-Mungu huuchunga kwa makini ulimwengu wote, ili kuwapa nguvu wale walio waaminifu kwake. Umetenda jambo la kipumbavu, kwa hiyo tangu sasa, utakuwa na vita kila mara.”

10Maneno haya yalimfanya Asa amkasirikie sana Hanani mwonaji, hata akamfunga gerezani. Wakati huohuo, Asa alianza kuwatesa vikali baadhi ya watu.

Mwisho wa utawala wa Asa

(1 Fal 15:23-24)

11Matendo ya Asa, toka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha “Wafalme wa Yuda na Israeli.”

12Katika mwaka wa thelathini na tisa wa ufalme wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu, akaugua sana. Lakini hata wakati huo, Asa hakumgeukia Mwenyezi-Mungu amsaidie, bali alijitafutia msaada kutoka kwa waganga.[#16:12 Rejea pia 1Fal 15:23. Mwanahistoria ya Mambo ya Wakati hapa anaonesha kwa namna ya pekee ujasiri wake juu ya hali ya watu wasiotaka kumtegemea Mungu. Kosa lake sio kuwaendea waganga, bali ni kule kuacha kumtegemea Mungu.]

13Hatimaye Asa alifariki mnamo mwaka wa arubaini na moja wa utawala wake.

14Alizikwa katika kaburi alilokuwa amejichimbia mwenyewe mwambani, katika mji wa Daudi. Walimlaza ndani ya jeneza lililokuwa limejazwa manukato ya kila aina yaliyotayarishwa na mafundi wa kutengeneza marashi, wakawasha moto mkubwa sana kwa heshima yake.[#16:14 Linganisha heshima alizopewa Asa katika kifo chake na jinsi watu walivyochukua kifo cha Yehoramu katika 21:19.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania