The chat will start when you send the first message.
1Watu wa Yuda walimtwaa Yehoahazi, mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme mahali pa baba yake.[#36:1 Huyu alikuwa mfalme wa kumi na sita wa Yuda na alitawala kwa miezi mitatu katika mwaka 609 K.K., ingawa hakuwa mtoto wa kwanza wa kiume wa mfalme Yosia.]
2Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala kwa muda wa miezi mitatu huko Yerusalemu.[#36:2-14 Mwandishi wa Mambo ya Nyakati anapitia harakaharaka tawala za watoto watatu wa Yosia yaani Yehoahazi, Yoakimu na Sedekia, na simulizi ni fupi kuliko lile la 2Fal 23:31—24:20.]
3Baadaye mfalme wa Misri alimwondoa huko Yerusalemu na akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za fedha na kilo 34 za dhahabu.[#36:3 Baada ya kuangamia kwa mfalme Yosia (609 K.K.) Misri ilitawala Yuda.]
4Kisha mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu; lakini Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye mpaka Misri.[#36:4 Huyo Yehoyakimu alikuwa mfalme wa kumi na saba wa Yuda. Jambo la mfalme mmoja kuweza kubadili jina la mfalme mwingine linaashiria kwamba mfalme huyo ana mamlaka juu ya huyo mfalme mwingine. Maana ya jina la mtu, wakati huo lilikuwa muhimu sana, na kwa kubadili “Eliakimu” (maana yake “Mungu amesimika”) na kuwa “Yehoyakimu” (maana yake “Mwenyezi-Mungu amesimika”), Nebukadneza ndiye aliyekuwa mtawala. Nebukadneza alitawala Babuloni mwaka 605-562 K.K.]
5Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
6Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alimshambulia, akamfunga kwa pingu ili kumpeleka mateka Babuloni.
7Nebukadneza pia alitwaa baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu akavipeleka Babuloni na kuviweka katika ikulu yake huko Babuloni.
8Basi, matendo mengine ya Yehoyakimu, pamoja na machukizo aliyotenda na mengine yaliyoonekana dhidi yake tazama yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda. Yehoyakini mwanawe alitawala badala yake.
9Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu na siku kumi. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.[#36:9 Yehoyakini alikuwa mfalme wa kumi na nane wa Yuda na alitawala kwa miezi mitatu katika mwaka 598 K.K.]
10Mwaka ulipokwisha, mfalme Nebukadneza alituma wajumbe, wakamchukua Yehoyakini mateka hadi Babuloni, pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akamtawaza Sedekia, nduguye, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.[#36:10 Mambo hayo yalitukia mwaka 597 K.K. Taz pia Yer 22:24-30: 24:1-10; 29:1-2; 37:1; Eze 17:12-13.]
11Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja.[#36:11 Huyu alikuwa mfalme wa kumi na tisa wa Yuda na alitawala mwaka 598-587 K.K. Nebukadneza alibadili jina lake la Matania (maana yake “Zawadi ya Mwenyezi-Mungu”) kuwa Sedekia (maana yake “Uadilifu wa Mwenyezi-Mungu”). Taz 36:4 maelezo juu ya mtindo huo wa kubadili jina la mtawala.]
12Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, wala hakunyenyekea mbele ya nabii Yeremia ambaye alisema maneno yaliyotoka kwa Mwenyezi-Mungu.
13Sedekia alimwasi pia mfalme Nebukadneza aliyekuwa amemfanya aape kwa jina la Mungu kwamba hatamwasi. Alikuwa mkaidi sana na mwenye kiburi akakataa kumgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
14Hata makuhani, viongozi wa Yuda pamoja na watu walikosa uaminifu kabisa wakiiga matendo yote ya kuchukiza ya watu wa mataifa mengine; waliichafua nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambayo yeye mwenyewe alikuwa ameitakasa huko Yerusalemu.
15Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, mara kwa mara alituma kwao wajumbe wake maana alikuwa na huruma kwa watu wake na makao yake.[#36:15 Maonyo ya manabii yanatokea mara kwa mara katika Mambo ya Nyakati (taz 20:20). Nabii Yeremia alihudumu wakati wa Sedekia (Yer 1:3; 34:1—38:28). Manabii Ezekieli na Habakuki walihudumu wakati huo pia.]
16Lakini wao waliendelea kuwadhihaki wajumbe wa Mungu, wakayapuuza maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka hatimaye ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya watu wake hata kusiwe na namna yoyote ya kutoroka.
17Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu alimleta mfalme wa Wakaldayo ambaye aliwaangamiza vijana wao kwa upanga hata ndani ya mahali patakatifu; wala hakumhurumia mtu yeyote awe mvulana au msichana, mzee au mnyonge. Wote Mwenyezi-Mungu aliwatia mikononi mwake.
18Alitwaa vyombo vyote vya nyumba ya Mungu vikubwa na vidogo na hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya mfalme na maofisa wake. Alivipeleka vyote mpaka Babuloni.
19Aliichoma moto nyumba ya Mungu, akaubomoa ukuta wa Yerusalemu, akayachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu vyombo vyake vyote vya thamani.
20Watu walionusurika vitani aliwachukua uhamishoni Babuloni. Huko wakawa watumwa wake na wa wazawa wake mpaka mwanzo wa ufalme wa Persia.
21Hivyo likatimia neno la Mwenyezi-Mungu alilosema nabii Yeremia: “Nchi itabaki tupu bila kulimwa miaka sabini kulingana na muda wa pumziko ambao haukuadhimishwa.”
22Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili litimie neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake wote na kuiweka katika maandishi:[#36:22 Mambo yaliyo katika aya 22-23 ni sawa na yale ya Ezra 1:1-4. Inahisiwa kwamba hapo awali vitabu vya Ezra na Nehemia vilikuwa sehemu ya mwisho ya kazi yote ya maandishi ya Mambo ya Nyakati. Lakini ilipofikiriwa kwamba masimulizi ya Ezra na Nehemia ni maendelezo ya vitabu vya Samueli na Wafalme vilitenganishwa na vitabu vya Mambo ya Nyakati na kuwekwa kabla yake katika Biblia ya Kiebrania. Tena, 1 na 2 Mambo ya Nyakati katika Biblia ya Kiebrania vilipata nafasi ya mwisho kabisa katika orodha ya vitabu vya Biblia ya Kiebrania.; #36:22 Huyo alikuwa Koreshi wa pili ambaye alianza nasaba ya Akemenidi na dola la Persia; alitawala mwaka 549-530 K.K. Moja ya ushindi wake mkubwa ulikuwa kuiteka Babuloni mnamo mwaka 539. Nabii Isaya anamsifu Koreshi kuwa “mteule wa Mungu” kwani ndiye aliyetumiwa na Mungu kuwawezesha Waisraeli kurudi makwao na kumwabudu Mungu huko (Isa 45:1-4). Koreshi alikuwa na mtazamo usiojifunga kuhusu uhuru wa watu wa mataifa mengi waliokuwa wahamishiwa kule Babuloni.]
23“Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni, na ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, nchini Yuda. Basi, sasa kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake na awe pamoja naye, na aende.”[#36:23 Mungu alimfanya Koreshi awaamuru Waisraeli warejee makwao kwa lengo maalumu la kujenga upya hekalu. Katika simulizi la kazi yake, mwandishi wa Mambo ya Nyakati anatilia mkazo unaostahili hekalu na ibada zake, akionesha jinsi urekebishaji wake ungeweza kufanyika ili kumrudia Mungu.]