The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Solomoni akasema,
“Mwenyezi-Mungu alisema ya kwamba
atakaa katika giza nene.
2Hakika nimekujengea nyumba tukufu,
mahali pa makao yako ya milele.”
3Kisha Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wamesimama, akawabariki.
4Akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ameitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa baba yangu Daudi akisema,
5‘Tangu niwaondoe watu wangu kutoka nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; na sikumchagua mtu yeyote awe mkuu wa watu wangu Israeli.
6Nimeuchagua mji wa Yerusalemu uwe mji ambamo nitaabudiwa, na nimemchagua Daudi awatawale watu wangu Israeli.’
7“Kwa hiyo, baba yangu Daudi alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
8Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba.
9Hata hivyo, si wewe utakayejenga hiyo nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’”
10“Na sasa Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
11Katika nyumba hiyo nimeliweka sanduku la agano, ambalo ndani yake mna agano la Mwenyezi-Mungu alilofanya na watu wa Israeli.”
12Kisha, Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu halafu mbele ya jumuiya yote ya watu wa Israeli, aliinua mikono yake juu.[#6:12-28 Sehemu hii karibu ni sambamba na 1Fal 8:22-53.]
13Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba ambalo aliliweka katikati ya ua. Urefu na upana wake ulikuwa mita mbili na robo, na kimo chake mita moja na robo. Alipanda jukwaani na kupiga magoti mbele ya jumuiya yote ya Israeli, akainua mikono yake kuelekea mbinguni.[#6:12-14 Lilikuwa jambo la kawaida kwa wafalme na makuhani au makasisi kumwomba Mungu kutoka majukwaa yaliyoinukia (taz pia 34:31). Hapa, jukwaa hilo lilikuwa karibu na mahali pa kutambikia (au, madhabahu ya kutolea sadaka) na sio ndani ya hekalu lenyewe.]
14Aliomba akisema, “Ee, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, mbinguni ama duniani. Wewe ni mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote.
15Umetimiza ahadi uliyotoa kwa mtumishi wako baba yangu Daudi; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe.
16“Kwa hiyo sasa, Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu, ukisema, ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watafuata kwa uangalifu sheria yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’[#6:16-17 Solomoni anagusia hapa ile ahadi iliyotolewa na Mungu kwa njia ya nabii Nathani kwamba daima kutakuwa na mtawala atakayetoka katika nasaba ya Daudi kuwatawala Waisraeli (1Nya 17:14 maelezo).]
17Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakusihi utimize yote uliyomwahidi mtumishi wako Daudi.
18“Lakini, ee Mungu kweli utakaa humu duniani na binadamu? Hata mbingu zenyewe, wala mbingu za mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga?[#6:18-39 Hapa Solomoni anashughulikia jambo ambalo lilimtia wasiwasi. Anamwomba Mungu hekalu hilo liwe mahali kitovu cha taifa kwa ajili ya sala na maombi ambayo yatapokelewa na kusikilizwa na Mungu. Anaanza na ombi la kiujumla — Mungu asikilize sala za watu (aya 18-21), akitaja mazingira saba mwafaka ambayo yanaweza kuhitaji sala au maombi hekaluni au kwa kuelekea huko (aya 22-29). Hali hii ya maombi ya Solomoni, inawatia moyo aghalabu wasomaji wake wakati wa marekebisho yaliyofuata kurudi kwa Waisraeli kutoka uhamishoni Babuloni, walilifanya lile hekalu kuwa kitovu cha sala wakati ule.]
19Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako, nakuomba unisikilize na kunitimizia ombi langu ninalokuomba leo.
20Ichunge nyumba hii mchana na usiku, mahali ambapo umechagua watu wako waliabudu jina lako. Unisikie mimi mtumishi wako ninapokuja mahali hapa kuomba.
21Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni na ukisha sikia, utusamehe.[#6:21 Solomoni anatumia maneno hayo mara nne katika sala yake (aya 21,30,33,39), jambo ambalo linaliweka hekalu mahali pake panapostahili kidini, hekalu lenyewe likichukukuliwa kuwa ni mahali mwafaka duniani pa kukaribia mahali pa Mungu mbinguni kwa njia ya matambiko yaliyofanywa hapo na ahadi Mungu alizotoa kwa kuweko kwake huko (1Nya 13:6 maelezo).]
22“Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, na akiapa tafadhali
23wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake; asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake.
24“Wakati watu wako Israeli watakaposhindwa na maadui zao, kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kukiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii,
25basi, usikie kutoka huko mbinguni. Usamehe dhambi zao na uwarudishe katika nchi uliyowapa wao na babu zao.
26“Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao, tafadhali
27uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi zao watumishi wako watu wako Waisraeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu, ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yao.[#6:27 Dhambi husababisha maafa mbalimbali kwa mtu au taifa ambalo halitaki kumtii Mungu. Baadhi ya maafa hayo yanatajwa: njaa, ukame, maradhi ya mimea, uvamizi wa wadudu waharibifu, tishio la vita. Ili kuepa hayo, mtu au taifa sharti limrudie Mungu na kutii (aya 31); rejea pia aya 32.]
28“Iwapo kuna njaa nchini au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi, au ikiwa watu wako wamezingirwa na maadui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote,
29tafadhali usikie maombi yoyote yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli, kila mtu akijua taabu yake na huzuni yake akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea nyumba hii.
30Basi usikie kutoka kwako mbinguni, utoe msamaha, pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili, kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote.
31Hivyo watakutii na kuenenda katika njia zako wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu.
32“Vivyo hivyo wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli atakuja kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako kuu, na kwa sababu ya nguvu na ulinzi wako, kuomba katika nyumba hii,
33nakusihi umsikie toka huko kwako mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako Israeli na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga inajulikana kwa jina lako.[#6:32-33 Solomoni anaomba kwamba hata wageni, yaani watu wasio Waisraeli, wasikilizwe na Mungu wanaposali au kuomba humo hekaluni. Manabii nao walitumaini kwamba wakati ungefika ambapo watu wasio Waisraeli wangejumuishwa katika kundi la watu wa Mungu (Isa 56:6-8; Zek 8:20-23; 14:16-21). Kujumuishwa kwa watu wengi wasio Waisraeli katika kundi la watu wa Mungu kulikuwa jambo lililokamilishwa kwa tukio lake Kristo Yesu (Rom 3:29; Gal 3:14; Efe 2:14-22).]
34“Watu wako wakienda vitani kupigana na maadui zao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji huu uliouchagua na nyumba ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako,
35nakusihi usikie sala yao na maombi yao ukiwa huko mbinguni na uwapatie ushindi vitani.
36“Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako, maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, na ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya mbali au ya karibu;
37kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi kwa roho yao yote na kwa moyo wao wote na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu’;
38pia kama watatubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote wakati watakapokuwa katika nchi ya uhamisho, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako;
39basi, nakusihi usikie huko mbinguni uliko sala yao na maombi yao na uwapatie haki zao, uwasamehe watu wako ambao wametenda dhambi dhidi yako.
40“Sasa ee Mungu wangu, tuangalie na upokee maombi tutakayoomba mahali hapa.
41Sasa inuka ee Bwana Mungu,
uingie mahali pako pa kupumzika
wewe pamoja na sanduku la agano la nguvu zako.
Makuhani wako ee Bwana Mungu, wapate wokovu,
na watakatifu wako wafurahie wema wako.
42Ee Bwana Mungu, usimpige kisogo masiha wako.[#6:42 Katika Kiebrania maana yake ni: “mpakwa mafuta au aliyetawazwa rasmi na Mungu”.]
Kumbuka fadhili zako kwa mtumishi wako Daudi.”