2 Wakorintho 2

2 Wakorintho 2

1Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.[#2:1 Ionekanavyo mahala pengine, hasa katika 2Kor 12:14, Paulo aliwatembelea Wakristo wa Korintho mara mbili. Yamkini ni wakati wa ziara hiyo ya pili Paulo alipohuzunishwa na mtu fulani naye Paulo akaitaka hiyo jumuiya kumchukulia hatua kali mtu huyo.]

2Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha!

3Ndiyo maana niliwaandikia: sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi.[#2:3-4 Ling na 2Kor 7:8-12. Yahusu barua nyingine ambayo Paulo aliandika baada ya ile ya kwanza na kabla ya hii Barua ya pili kwa Wakorintho.]

4Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno.

Msamaha

5Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi, ila amewahuzunisha nyinyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.

6Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.[#2:6 Paulo anasema juu ya adhabu ambayo yeye na Wakorintho waliijua; labda ilikuwa adhabu ya kutengwa na jumuiya ya waumini. Lakini Paulo anawataka Wakorintho wamsamehe mtu huyo na kumpa moyo (aya 7).]

7Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.

8Kwa hiyo nawasihi: mwonesheni kwamba mnampenda.

9Madhumuni yangu ya kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.

10Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe, kama kweli ninacho cha kusamehe, nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

11ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.

Wasiwasi wa Paulo mjini Troa

12Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana.

13Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.[#2:13 Paulo alikuwa amemtuma Tito Korintho (labda pamoja na ile barua anayotaja katika 2:3-4) na yamkini alikuwa anatazamia kupata habari za Wakorintho na alikuwa na wasiwasi sana juu ya kukawia kwake Tito.; #2:13 Kama kawaida ni namna au neno la kumtaja Mkristo kwa vile Wakristo wote ni kama wa jamaa moja ya Mungu au ya Kristo.; #2:13 Alikuwa mwenzi wake Paulo katika kuhubiri Habari Njema. Huyu ndiye yule yule aliyeandikiwa barua ijulikanayo sasa kama “Barua kwa Tito”. Kama jina lake linavyoashiria, yeye hakuwa Myahudi.]

Ushindi kwa msaada wa Kristo

14Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.[#2:14 Tafsiri nyingine yamkini: “Shukrani kwa Mungu ambaye hutuwezesha kushinda kwa kuungana na Kristo”.]

15Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea.

16Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?

17Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania