2 Wafalme 2

2 Wafalme 2

Elia anachukuliwa mbinguni

1Ikawa wakati ulipofika ambapo Mwenyezi-Mungu alitaka kumchukua Elia mbinguni katika upepo wa kisulisuli, Elia na Elisha walikuwa njiani, wakitoka Gilgali.[#2:1-25 Kwa simulizi la kifo cha Elia, kipindi cha huyu nabii mashuhuri kinamalizika na kuanza kipindi cha mfuasi wake, nabii Elisha. Licha ya miujiza mingi inayohusika na huyu nabii, kipindi hiki kinasimulia visa vya vita (2Fal 3:1-27; 6:24—7:20) na matendo ya nabii nje ya nchi yake (8:7-15; 13:14-21; rejea 5:1-23).; #2:1 Jina hili kwa kawaida lahusu mahali pa ibada kati ya Yeriko na Mto Yordani (taz Yos 4:19). Lakini mazingira yenyewe hapa yanaelekea kwamba yahusu mahali pengine panapoitwa kwa jina hilo hilo, karibu na Betheli.]

2Baadaye walipokuwa njiani, Elia alimwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Betheli.”[#2:2 Mji huu ambao ulikuwa maarufu sana tangu wakati wa mababu wa Waisraeli (taz Mwa 12:8; 28:10-22; 35:1-15) ulikuwa karibu kilomita ishirini Kaskazini ya Yerusalemu. Yeroboamu aliufanya kuwa mahali pa ibada pa utawala wa Kaskazini wa Israeli badala ya Yerusalemu (1Fal 12:28-33; Amo 7:13).]

Lakini Elisha akamwambia, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo, sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja hadi Betheli.

3Wanafunzi wa manabii waliokuwa huko wakamwendea Elisha, wakamwuliza, “Je, unajua kwamba leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.”[#2:3 Taz 1Fal 20:35.]

4Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Yeriko.” Lakini Elisha akakataa akisema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja mpaka Yeriko.

5Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.”

6Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja.

7Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo.

8Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ng'ambo ya pili, wakapitia mahali pakavu.[#2:8 Kitendo hiki cha kuyapiga maji nayo yakagawanyika sehemu mbili kinakumbusha tukio la Musa wakati Waisraeli walipovuka Bahari ya Shamu (Kut 14:16,21-22), na pia Mto Yordani (Yos 3:13-17).]

9Walipofika ng'ambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.”[#2:9 Tuko katika mazingira ya kama mtoto na baba yake, wakati baba karibu aondoke duniani. Elisha anaomba arithi nguvu ya Elia, tena maradufu kama ilivyokuwa kwa mtoto mzaliwa wa kwanza. Taz pia Kumb 21:15-17.]

10Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.”

11Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli.[#2:11 Hapa, wazo muhimu linaloafikiana na tukio hili ni lile la nguvu kuu ya Mwenyezi-Mungu isiyoshindwa na chochote (rejea 2Fal 6:17; Zab 18:17).]

12Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia.[#2:12 Yamkini kilio hiki ni kilio cha uchungu kwa upande wa Elisha ambaye sasa anamwona bwana na mkufunzi wake anaondoka kabisa. Maneno: “gari la Israeli na wapandafarasi wake” labda yana shabaha ya kuonesha kwamba Elia alikuwa kama nguvu kubwa ya jeshi kwa Waisraeli wote. Maneno hayo hayo yanatamkwa na Yehoashi, mfalme wa Israeli, alipokwenda kushuhudia kwamba Elisha alikuwa amekufa (taz 2Fal 13:14).]

Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili.

13Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani.[#2:13 Vazi hili lilimthibitisha Elisha kuwa ndiye sasa aliyekuwa na roho ya Elia, yaani nguvu yake (2:14-15).]

14Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ng'ambo.

15Wale wanafunzi wa manabii kutoka Yeriko walipomwona, walisema, “Roho ya Elia iko kwa Elisha.” Basi, wakaenda kumlaki, wakasujudu mbele yake.

16Wakamwambia, “Sisi watumishi wako tunao mashujaa hamsini; tafadhali waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Ikiwa roho ya Mwenyezi-Mungu imembeba na kumtupa juu ya mlima fulani au bondeni.” Elisha akajibu, “La, msiwatume.”[#2:16 Mara kwa mara Elia alitoweka na kutokea tena kwa namna isiyoelezeka (taz k.m. 1Fal 18:9-16).]

17Lakini wao waliposisitiza mpaka akaona haya, aliwaambia “Watumeni.” Hivyo wakawatuma watu hamsini, wakaenda wakamtafuta kila mahali kwa muda wa siku tatu wasimwone.

18Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?”

Miujiza ya Elisha

19Baadaye watu wa Yeriko walimwendea Elisha, wakamwambia, “Bwana, kama uonavyo mji huu ni mzuri, lakini maji tuliyo nayo ni mabaya na yanasababisha mimba kuharibika.”[#2:19-25 Kipindi cha Elisha, tofauti na kile cha Elia, kina miujiza mingi zaidi: kuyafanya maji mabaya kuwa mazuri (2Fal 2:19-22); dubu wawili dhidi ya vijana wazomeaji (2:23-24); kuongeza mafuta (4:1-7); muujiza wa chakula (4:38-41); kuongeza mikate (4:42-44); kupatikana kwa shoka (6:1-7); kufufuliwa kwa mtu aliyekufa (13:20-21). Lakini miujiza miwili inaelezwa kwa kirefu na kwa mapana zaidi: kuzaliwa na kufuliwa kwa mtoto wa mama mmoja Mshunami (4:8-37) na kuponywa kwa Naamani (5:1-27).]

20Elisha akawaambia, “Tieni chumvi ndani ya bakuli jipya, kisha mniletee.” Nao wakamletea.[#2:20 Ingawa chumvi tangu awali iliweza kusafisha maji, hapa uwezo wake unatoka kwa Mungu mwenyewe na ni kitendo cha vitendo vingi vinavyoonesha uwezo wa Mungu wa miujiza.]

21Elisha akaenda kwenye chemchemi ya maji, akatupa chumvi hiyo ndani na kusema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeyafanya maji haya kuwa yenye kufaa; tangu sasa hayatasababisha vifo au kutoa mimba.”

22Na maji hayo yamekuwa ya kufaa mpaka leo, kama alivyosema Elisha.

23Elisha aliondoka Yeriko, akaenda Betheli. Alipokuwa njiani, vijana fulani walitoka mjini wakaanza kumzomea wakisema, “Nenda zako, nenda zako mzee kipara!”[#2:23-24 Nyakati hizo za kale kuwa na kipara kulikuwa ni jambo la balaa. Huenda Elisha alikuwa kipara kimaumbile au labda alikuwa amenyoa kipara kujitenga kama nabii. Hatujui, lakini hao watoto walimdhihaki nabii na kwa kufanya hivyo ni kama walimtukana Mungu. Idadi ya watoto “arubaini na mbili” huenda inaashiria picha au mfano wa uharibifu (rejea k.m. 2Fal 10:14; Ufu 11:2; 13:5).]

24Elisha aligeuka akawatazama na kuwalaani kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Dubu wawili majike wakatoka mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao.

25Elisha akaendelea na safari yake mpaka mlima Karmeli na kutoka huko akarudi Samaria.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania