2 Wafalme 22

2 Wafalme 22

Mfalme Yosia wa Yuda

(2 Nya 34:1-2)

1Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala huko Yerusalemu, akatawala kwa miaka thelathini na mmoja. Mama yake alikuwa Yedida, binti Adaya, mkazi wa mji wa Boskathi.[#22:1 Ingawa watu hawawezi kuelewa mtoto wa umri huo kuwa mfalme, nchi nyingi zenye utawala wa kifalme wa jadi mtindo huo unaeleweka. Hapa lakini yamkini yaweza kufikiriwa kwamba utawala wa Yuda ulikuwa na uhakika wa ahadi ya Mwenyezi-Mungu kwa Daudi kuhusu kudumu kwa nasaba ya ufalme (2Sam 7:16). Kutokana na hilo hakuna aliyetilia mashaka mtindo wa kutawala kulingana na nasaba ya kifalme, hata kama aliyehusika alikuwa mtoto (rejea 2Fal 11:1-3,12).; #22:1-23 Yosia alikuwa mfalme wa kumi na tano wa Yuda. Alianza marekebisho ya kidini katika Yuda baada ya kuhani mkuu Hilkia kugundua Kitabu cha Sheria ya Mungu kule hekaluni Yerusalemu (rejea 2Nya 34:1-2).]

2Yosia alitenda mema na alimpendeza Mwenyezi-Mungu. Alifuata mfano wa mfalme Daudi aliyemtangulia, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa makini.

Kitabu cha Sheria chagunduliwa

(2 Nya 34:8-28)

3Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, mfalme alimtuma katibu Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akisema,

4“Nenda kwa kuhani mkuu Hilkia umwambie ahesabu zile fedha zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambazo mabawabu walizikusanya kutoka kwa watu.

5Kiasi cha fedha hizo zipewe wasimamizi wa marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kulipa mishahara ya mafundi wanaofanya marekebisho,

6yaani maseremala, wajenzi na waashi. Kiasi kingine kitumike kununua mbao na mawe yaliyochongwa kwa ajili ya kurekebisha nyumba.

7Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.”[#22:4-7 Yapata miaka mia mbili kabla, mfalme Yoashi alikusanya fedha pia kwa ajili ya kufanya marekebisho ya hekalu.]

8Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma.[#22:8 Wafafanuzi wengi wa Biblia wanafikiri hicho kitabu huenda kikawa sehemu ya Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria ambayo inajumuisha sheria Mungu aliyompa Mose. Baadhi wanadhani yahusu Kumb 5 ambapo kuna pia zile Amri Kumi; wengine wanafikiri yahusu Kumb 28-30 sehemu ambayo inasema juu ya baraka na laana zitakazowapata watu kama wakishika au wakivunja agano lake. Wengine wanafikiri yahusu vitabu vyote vitano vya kwanza vya Biblia.]

9Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”

10Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.

11Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake.[#22:11 Taz 5:7 maelezo. Hapa pia ni kama ishara ya masikitiko na huzuni kwa vile sheria ya Mungu haikushikwa na kuzingatiwa kama ilivyotakiwa.]

12Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema,

13“Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.”

14Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye.[#22:14 Kwamba hapa ushauri unatakiwa sio kutoka kwa nabii yeyote yule, ila kutoka kwa nabii mwanamke, labda ni kwa sababu huyo aliishi karibu na hekalu. Wanawake wengine wanaotajwa katika Biblia kama manabii ni Miriamu (Kut 15:20), Debora (Amu 4:4), Hana (Luka 2:36). Rejea pia Neh 6:14 na Mate 21:9.]

15Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu,

16Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Nitaleta uovu juu ya mahali hapa na juu ya wakazi wake kama ilivyo katika kitabu kilichosomwa na mfalme wa Yuda.

17Kwa sababu wameniacha na kufukizia ubani miungu mingine na hivyo kunikasirisha kwa kazi zote za mikono yao, ghadhabu yangu dhidi ya Yerusalemu itawaka na haitaweza kutulizwa.

18Lakini kuhusu mfalme wa Yuda aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu, mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, juu ya maneno uliyoyasikia,

19Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia mbele yangu, hapo uliposikia niliyosema dhidi ya mahali hapa na dhidi ya wakazi wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nami pia nimekusikia.

20Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na babu zako nawe utawekwa kaburini kwa amani, macho yako hayataona uovu nitakaouleta juu ya mahali hapa.’” Basi wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi.[#22:20 Mfalme Yosia alikufa kabla ya kutekwa kwa mji wa Yerusalemu na kwa sababu hiyo inaweza kusemwa alikufa kwa amani. Hata hivyo, kifo chake hakikuwa cha amani kwani aliuawa mwaka 609 na Wamisri mjini Megido wakati akijaribu kuweka mpango wa kuufanya utawala wa Yuda ujitegemee wenyewe. Kifo chake vitani kilikomesha mipango ya marekebisho ya kidini katika Yuda.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania