The chat will start when you send the first message.
1Wakati Onia alipokuwa kuhani mkuu, mji mtakatifu ulikuwa na amani na ustawi, na sheria zilishikwa kiaminifu kabisa, kwa sababu Onia alikuwa mcha Mungu na alichukia maovu.[#3:1-40 Sehemu ya kwanza ya hili simulizi (3:1-40) inaonesha jinsi Mungu alivyolilinda hekalu wakati wa kuhani Onia.; #3:1 Huyo ni Onia III, mwana wa Simoni II (taz 4:4-6; Sira 50:1-21).]
2Wafalme waliliheshimu hekalu, wakalitunukia zawadi za thamani.
3Na mfalme Seleuko, mtawala wa Asia yote, alikuwa analipia gharama za matoleo ya tambiko hekaluni kutoka katika hazina yake mwenyewe.[#3:3 Huyo ni Seleuko IV, aliyeitwa Filopatori, mwana wa Antioko III.]
4Lakini Simoni, mtu mmoja wa kabila la Benyamini, aliyekuwa ofisa mkuu wa shughuli za hekalu, alikuwa na mzozo na Onia kuhusu utaratibu wa soko la mji.
5Wakati huo Apolonio wa Tarso alikuwa mkuu wa Siria Kuu. Basi, Simoni akamwendea Apolonio,[#3:5 Kigiriki: “Apolonio mwana wa Tarso”.]
6akamwambia kwamba hazina ya hekalu ilikuwa na fedha nyingi hivi hata haikuwezekana kuihesabu; na kwamba kwa vile fedha hiyo haikuhitajika kwa ajili ya tambiko, ingeweza pia kuwekwa mikononi mwa mfalme.
7Apolonio alipokutana na mfalme, alimweleza habari ya fedha hiyo, naye mfalme akaamuru Heliodoro, waziri wake mkuu, akaichukue na kumletea fedha hiyo.
8Heliodoro aliondoka mara kwenda alikotumwa, lakini alifanya kana kwamba alikuwa anafanya ziara ya kukagua miji ya Siria Kuu.
9Alipowasili Yerusalemu na kukaribishwa vizuri sana na kuhani mkuu, alieleza madhumuni halisi ya safari yake, na akauliza kama yale aliyokuwa ameambiwa yalikuwa kweli.
10Kuhani mkuu alimweleza kwamba palikuwa na fedha fulani iliyowekwa katika hazina ya hekalu, lakini kiasi fulani ilikuwa kwa ajili ya wajane na yatima,[#3:10 Kusaidia wajane na yatima ilikuwa jukumu la jadi katika Israeli. Rejea Kumb 27:19; Isa 1:23.]
11na kiasi kingine kilikuwa mali ya Hirkano mwana wa Tobia, mtu maarufu sana. Pia alibainisha kwamba kiasi cha fedha hiyo kilikuwa kilo 13,000 tu, na dhahabu ilikuwa kilo 6,500.
12Aliongeza kusema kwamba ilikuwa haiwezekani kabisa kuwadhulumu watu walioweka tumaini lao kwa utakatifu na usalama wa hekalu lililosifika duniani kote.
13Lakini Heliodoro alisisitiza kwamba fedha hiyo lazima ichukuliwe kwa ajili ya hazina ya mfalme, kama mfalme alivyokuwa ameamuru.
14Hivi akapanga siku ya kwenda hekaluni kusimamia hesabu ya fedha hiyo. Kitendo hicho kilisababisha ghasia kubwa mji mzima.
15Makuhani, wakiwa wamevalia mavazi yao ya kikuhani, walianguka kifudifudi mbele ya madhabahu, wakamwomba Mungu ailinde fedha hiyo, kwa vile alikuwa ametoa sheria kulinda fedha waliyoweka watu hekaluni.
16Kila aliyemtazama kuhani mkuu alichomwa moyoni. Uso wake ulibadilika rangi, uchungu wa roho yake ukadhihirika nje.
17Kiwiliwili chake kilikuwa kinatetemeka kwa hofu, huzuni yake ya moyoni haikufichika.
18Watu walitoka mbio majumbani mwao, wakaenda kujiunga na makuhani katika sala kusudi hekalu lisitiwe unajisi.
19Wanawake nao, hali wamejifunga gunia kifuani, walifurika mitaani. Wanawali, ambao wazazi wao hawakuwa wamewaruhusu kutoka ndani, walikimbilia kwenye milango au kuta za mji, na wengine wakabaki wanachungulia madirishani.
20Hao wote, kila walipokuwa, waliinua mikono yao kwa Mungu, wakisali.
21Ama hakika ilisikitisha kumwona kuhani mkuu katika kuvunjika moyo na maumivu makali kama hayo, na kuwaona watu wote mjini wamechanganyikiwa na kulala kifudifudi vumbini.
22Wakati walipokuwa wanamwomba Bwana Mwenye Nguvu ailinde salama fedha hiyo iliyokuwa imewekwa chini ya ulinzi wake,
23Heliodoro aliamua kuendelea na mpango wake.
24Lakini mara tu yeye na walinzi wake walipofika penye hazina, Bwana wa roho zote na mamlaka yote akaleta tukio la ajabu hivi kwamba kila mmoja aliyekuwa amethubutu kuingia na Heliodoro alipigwa na fadhaa na kuishiwa nguvu mwilini kwa hofu.[#3:24 Jina hili la sifa linatumiwa mara chache sana katika Biblia. Taz Hes 16:22 ambapo Kiebrania kina Mungu wa roho (wingi).]
25Katika tukio hilo waliona farasi na mpandaji wake. Farasi alikuwa na matandiko ya fahari, na mpandafarasi alikuwa anatisha. Ghafla, huyo farasi alimkabili Heliodoro na kumshambulia kwa miguu yake ya mbele.
26Pia vijana wawili, wenye nguvu ajabu na uzuri mno wamevalia nguo za fahari, walitokea mbele ya Heliodoro na kusimama mmoja kulia na mmoja kushoto kwake; wakampiga Heliodoro mapigo mengi.
27Heliodoro akaanguka chini mara na kupoteza fahamu. Watu wake wakamwokota na kumweka katika machela,
28wakamtoa nje. Dakika chache tu kabla yake mtu huyu aliyekuwa ameingia kwenye hazina na kundi kubwa la watu, wakiwamo walinzi wake wote, lakini sasa alikuwa anaondolewa kwa machela, yu hoi. Basi, watu wote walikiri uwezo mkuu wa Mungu.
29Kutokana na kipigo hicho kutoka kwa Mungu, Heliodoro alibaki amelala taabuni, hawezi kusema wala hana tumaini la kupona.
30Lakini Wayahudi wakamsifu Bwana aliyetenda kwa namna ya ajabu kwa ajili ya maskani yake. Nalo hekalu ambalo hapo awali lilikuwa na watu wamejaa woga na wasiwasi sasa likawa shangwe na furaha tupu.
31Baadhi ya marafiki wa Heliodoro, walimwomba Onia, kuhani mkuu, amsihi Mungu Mkuu ili amwepushe na kifo huyo aliyekuwa katika hatari ya kufa.
32Basi, kuhani mkuu akatoa tambiko kwa matumaini kwamba Mungu angemponya Heliodoro, maana hakutaka mfalme ahisi kwamba Wayahudi ndio waliokuwa wamemtenda hivyo mtu aliyetumwa naye.
33Onia alipokuwa anatoa tambiko hiyo, wale vijana wawili, wakiwa wamevaa nguo zilezile kama kwanza, wakamtokea tena Heliodoro na kusema: “Umshukuru sana kuhani mkuu; maana kwa ajili yake, Bwana ameyaokoa maisha yako.
34Kumbuka kwamba Bwana wa mbingu ndiye aliyekuadhibu. Sasa nenda zako, na ukamweleze kila mtu habari juu ya nguvu ya ajabu ya Mungu.” Walipokwisha sema hayo, vijana wakatoweka.
35Hapo Heliodoro akamtolea Bwana tambiko na kuweka ahadi nyingi, kwa sababu Bwana alikuwa ameokoa maisha yake. Halafu alimwaga Onia, akarudi kwa mfalme pamoja na jeshi lake.
36Huko akamsimulia kila mtu mambo ambayo Bwana, Mwenye Nguvu alikuwa amefanya.
37Mfalme alipomwuliza Heliodoro kama nani angefaa zaidi kutumwa Yerusalemu safari nyingine, Heliodoro alijibu:
38“Kama unaye adui, au kama unamjua mtu anayefanya njama dhidi ya serikali yako, mpeleke huyo. Atarudi amepigwa vibaya sana - kama atajaliwa kurudi - maana kule Yerusalemu uwezo wa ajabu wa Mungu unatenda kazi.
39Mungu aliye na makao yake mbinguni hulilinda hilo hekalu yeye mwenyewe na kumwangamiza yeyote anayetaka kulidhuru.”
40Hayo ndiyo matokeo ya kisa cha Heliodoro na hazina iliyolindwa ya hekalu.