The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo, Daudi aliwapiga, akawashinda Wafilisti. Akauteka mji wa Metheg-ama kutoka utawala wa Wafilisti.[#8:1-14 Sehemu hii inaelezea visa vya ushindi kadha wa kadha dhidi ya Wafilisti, Wamoabu na tawala nyingine mbalimbali. Kwamba ushindi huo wa Daudi hauelezwi kinaganaga labda ni kwa sababu mwandishi anataka kuonesha kwamba kwa wingi ushindi huo ulikuwa ushindi wa Mungu.; #8:1 Hawa wanatajwa wa kwanza miongoni wa wale walioshindwa na Daudi kwa vile walikuwa hatari sana kwa utawala wake.]
2Kisha aliwashinda Wamoabu. Aliwapanga katika mistari mateka hao, na kuwalaza chini. Aliamuru wale waliokuwa katika mistari miwili wauawe na wale wa mstari wa tatu waachwe hai. Hivyo, Wamoabu wakawa watumishi wake Daudi na wakawa wanamlipa kodi.[#8:2 Uhusiano kati ya Wamoabu na Waisraeli karibu kila mara ulikuwa wa wasiwasi sana (Hes 22—24; Amu 11:17-18; rejea Isa 15—16; Yer 9:26; Eze 25:8-11; Amo 2:1; Sef 2:8-11). Hata hivyo tunaarifiwa katika 1Sam 22:3-5 kwama Wamoabu walimsaidia Daudi na kulingana na Rut 4:13-22 Daudi mwenyewe alikuwa mzawa wa mama mmoja Mmoabu.]
3Daudi pia alimshinda Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Daudi alipata ushindi huu wakati Hadadezeri alipokuwa njiani kwenda kulirudisha eneo la mto Eufrate kuwa chini ya utawala wake.
4Daudi aliteka wapandafarasi 1,700, na askari wa miguu 20,000. Kisha Daudi alikata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wa magari, ila alibakiza farasi wa kutosheleza magari 100.
5Nao Waaramu wa Damasko walipokwenda kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi aliwashambulia na kuwaua watu 22,000.[#8:5 Damasko ulikuwa mji mkubwa kuliko miji mingine ya Aramu au Siria. Inasemekana kwamba huo ulikuwa mji wa kale zaidi ambao ulikaliwa mfululizo. Kwa kuteka eneo hilo Daudi alikuwa na uwezo juu ya karibu eneo lote la Siria.]
6Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Waaramu wa Damasko. Basi, Waaramu wakawa watumishi wake na wakawa wanamlipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda.
7Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri na kuzipeleka Yerusalemu.
8Pia alichukua shaba nyingi sana kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri.
9Wakati Toi, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,
10alimtuma mwanawe Yoramu kwa mfalme Daudi kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Toi mara nyingi. Yoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
11Zawadi hizo, pamoja na fedha na dhahabu alizokuwa ameziteka kwa mataifa yote aliyoyashinda, aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu,
12yaani kutoka Edomu, Moabu, Amoni, Filistia, Amaleki, pamoja na nyara alizoteka kwa mfalme Hadadezeri, mwana wa Rehobu mfalme wa Soba.[#8:12 Katika makala ya Kiebrania kuna “Aramu”. Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko wanaeleza tofauti hii kutokana na kwamba katika Kiebrania neno “Edomu” na “Aramu” yanafanana kwa namna yanavyoandikwa.]
13Daudi alijiongezea umaarufu wake. Alipokuwa anarudi baada ya kumshinda Hadadezeri, aliwaua Waedomu 18,000, katika Bonde la Chumvi.
14Akaweka kambi za kijeshi katika Edomu yote. Nao Waedomu wote wa huko wakawa watumishi wake. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda.
15Hivyo, Daudi akatawala juu ya Israeli yote, akahakikisha watu wake wote wanatendewa haki ipasavyo.
16Yoabu mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa majeshi. Yehoshafati mwana wa Ahiludi, alikuwa mweka kumbukumbu.
17Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani. Seraya alikuwa katibu.
18Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi, nao wana wa Daudi wakawa makuhani.[#8:18 Wakerethi na Wapelethi walikuwa walinzi binafsi wa Daudi. Hawa hawakuwa Waisraeli ila walikuwa maaskari wa kukodiwa ambao walimsindikiza Daudi wakati alipomkimbia Shauli (rejea 1Sam 27—31).]