The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uhai tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu,[#1:1-2 Barua hii inaanza kama kawaida ya barua za nyakati hizo (taz Rom 1:1-7 na maelezo kwa utangulizi wa Barua za A.J.)]
2nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo.[#1:2 Rejea 1Tim 1:2 maelezo.]
Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka katika sala zangu usiku na mchana.[#1:3-5 Kwa kutoa shukrani kwa Mungu (taz Rom 1:8,9,10,11,13 maelezo) kwa sababu ya imani ya Timotheo, Paulo anatoa hapo msingi wa mashauri ambayo ataendelea kumpatia huyo mwenzake katika kuhubiri Injili.]
4Nakumbuka machozi yako na ninatamani sana kukuona, ili nijazwe furaha.[#1:4 Yamkini yahusu kisa kinachotajwa katika Mate 20:36-38 (ikiwa Timotheo alikuwa mmojawapo wa wale waliolia kwa sababu ya maneno ya Paulo ya kuwaaga). Wengine wanafikiri, “kwa machozi” hapa, inahusu machozi ya jumla ambayo yaliandamana na shughuli na kazi za kuhubiri Injili kwa upande wa Paulo na mshiriki mwenzake Timotheo (taz Mate 20:19,31).]
5Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.[#1:5 Hao akina mama walikuwa Wayahudi na walimlea na kumfunza Timotheo juu ya tumaini la kuja kwake Masiha kulingana na Maandiko Matakatifu (2Tim 3:15). Tunajua, kutokana na Mate 16:1, kwamba mama yake Timotheo alikuwa Mkristo.]
6Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.[#1:6 Juu ya kitendo hicho cha ishara tazama yaliyosemwa katika 1Tim 4:14. Katika Barua hii ya pili kwa Timotheo, uhusiano wa karibu kati ya Paulo na Timotheo ni dhahiri zaidi kwa vile anamwita Timotheo “mwanawe”.]
7Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
8Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu.
9Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu kabla ya wakati,[#1:9 Tito 3:5; rejea Rom 3:27-28; 4:2,5; Gal 2:16; Efe 2:8-9. Aya 9-10 ni muhtasari mdogo wa Injili; rejea 2Tim 2:8; Mate 2:36; taz 1Kor 15:4 maelezo.]
10lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo.
11Mimi nimechaguliwa niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema,
12nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile.[#1:12 Neno “alichonikabidhi” linaendana na kitu ambacho ni “hazina” au “kitu cha thamani kuu” ambacho lazima kitunzwe kwa uangalifu mpaka mwenyewe atakapokitaka. Na, maneno: “siku ile” yanahusu siku ya hukumu ya mwisho (taz 1:18).]
13Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu.[#1:13 Au, “mafundisho safi”; au, “mafundisho yaliyo sawa”. Namna hiyo ya kusema ni kawaida katika barua hizi zinazojulikana kama za “kichungaji”; taz 1 Tim1:10 maelezo.]
14Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.[#1:14 Au, “fundisho lile jema ulilokabidhiwa”. Na kuhusu neno “kukabidhiwa”, taz aya ya 12 maelezo.]
15Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene.[#1:15 Mkoa wa Kiroma katika eneo ambalo sasa ni sehemu ya Magharibi ya nchi ya Uturuki; mji wake mkuu ulikuwa Efeso. Kuhusu hao watu ambao walimwacha Paulo hatuna habari zaidi ila rejea 2Tim 4:10. Wala hatuna habari zaidi juu ya Figelo na Hermogene.]
16Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni,[#1:16 Mkristo kutoka Efeso ambaye anatajwa tu hapa na katika 2Tim 4:19.]
17ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata.[#1:17 Paulo aliandika barua hii akiwa gerezani kule Roma (2Tim 2:9).]
18Bwana amjalie kupata huruma ya Mungu katika siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.[#1:18 Yaani, siku ile ya hukumu ya mwisho.]