The chat will start when you send the first message.
1Basi, kuhani mkuu akamwuliza, “Je, mambo haya ni kweli?”
2Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea babu yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani.
3Mungu alimwambia: ‘Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonesha!’
4Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa.[#7:2-4 Mwa 11:31—12:5. Lakini amri ya kuondoka alipewa akiwa Harani, mji ulio kaskazini mwa Mesopotamia, sasa ni nchi ya Uturuki, mpakani na Siria.; #7:4 Yaani Kanaani au Palestina.]
5Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidi kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto.
6Mungu alimwambia hivi: ‘Wazawa wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka 400.[#7:6 Kulingana na Mwa 15:13; hali Kut 12:40 inasemwa miaka 430.]
7Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.’[#7:7 Yahusu maneno aliyoambiwa Mose karibu na mlima Sinai (Kut 3:12); Stefano anayatumia kuhusu yaani hekalu, ambalo lilikuwa juu ya mlima Siyoni.]
8Halafu Mungu akafanya naye agano ambalo tohara ni ishara yake. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo.[#7:8 Ling na Mwa 17:10-14 na pia angalia Fahirisi.]
9“Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamwuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye,
10akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme.[#7:10 Ling na Mwa 41:15-16,25-36.]
11Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote.[#7:11 Wanawe Yakobo (aya 8).]
12Basi, Yakobo aliposikia habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza.
13Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu.
14Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na watano, waje Misri.[#7:14 Hapa, kulingana na tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) ya Mwa 46:27 na Kut 1:5. Makala ya Kiebrania ya sehemu hii inasema]
15Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa.[#7:15-16 Kadiri ya A.K. Yakobo alizikwa kule Hebroni, pangoni Makpela (Mwa 49:29-32; 50:7-13), eneo ambalo lilinunuliwa na Abrahamu (Mwa 23:1-20); aliyezikwa ni Yosefu (Yos 24:32), katika uwanja ambao Yakobo alikuwa ameununua (Mwa 33:18-19).]
16Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
17“Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi.
18Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri.
19Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.[#7:19 Kut 1:10—11:22. Ni watoto wa kiume tu waliuawa.]
20Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu,
21na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake.
22Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo.[#7:22 Ling na Luka 24:19. Katika Kut 4:10 Mose, anataja kwamba si hodari wa kusema!]
23“Alipokuwa na umri wa miaka arubaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli.
24Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. (
25Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo).
26Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’
27Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?[#7:27 Maneno ambayo hayamo katika kitabu cha Kutoka.]
28Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’
29Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.[#7:29 Kut 2:15; 18:3-4. Watoto hao ni Gershomu na Eliezeri (mama yao alikuwa Zipora).]
30“Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.[#7:30 Horebu (Kut 3:1) ni jina lingine la mlima huohuo.]
31Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:
32‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.
33Bwana akamwambia: ‘Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu.
34Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.’[#7:30-34 Taz Kut 3:1-10. Kuhusu kuvua viatu, itakaumbukwa kwamba ilikuwa marufuku kulingana na miiko ya kidini kuvaa viatu mahali patakatifu (Yos 5:15).]
35“Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?’ Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.[#7:35 Maneno yanayosimulia kukataliwa kwa Mose na kukuzwa kwake kama mkombozi yanafanana na yale yaliyotumika katika kuhubiri juu ya Yesu (Ling na Mate 5:31).]
36Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani, kwa muda wa miaka arubaini.
37Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: ‘Mungu atawateulieni nabii kama mimi miongoni mwa ndugu zenu nyinyi wenyewe.’[#7:37 Kumb 18:15,18, sehemu ambayo ilitumiwa juu ya Kristo katika mahubiri ya mitume yaliyotangulia kidogo (Mate 3:22-23).]
38Waisraeli walipokusanyika kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko kama mjumbe kati ya hao wazee wetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai. Ndiye aliyekabidhiwa yale maneno ya uhai atupe sisi.[#7:38 Mose alifanya kama kijumbe msuluhishi kati ya Waisraeli na malaika. Malaika hapa kama mahali kadha wa kadha katika A.K. likitumika kwa maana ya Mwenyezi-Mungu mwenyewe; kama Mwa 16:7.]
39“Lakini yeye ndiye babu zetu waliyekataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.
40Walimwambia Aroni: ‘Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata huyo Mose aliyetuongoza kutoka Misri!’[#7:40-42 Stefano analiona tukio la sanamu ya ya dhahabu (Kut 32:1-6) kama kitovu na kisa cha Waisraeli kumkataa Mose na Mungu na ambalo lilisababisha Mungu kwa upande wake kuwakataa.]
41Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.
42Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii:[#7:42-43 Msemo ambao wahusu mkusanyo wa pamoja wa vitabu vya manabii kumi na wawili waitwao “Wadogo”. Hapa amekaririwa Amo 5:25-27 kadiri ya Kigiriki ila hapa panasemwa Babuloni badala ya Damasko. Makala ya Kiebrania ya kitabu cha Amosi ina matatizo kadhaa; huko, hiyo miungu inayotajwa ni ya Babuloni na Ashuru.]
‘Enyi watu wa Israeli!
Si mimi mliyenitolea tambiko na sadaka
kwa miaka arubaini kule jangwani!
43Nyinyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki,[#7:43 Mungu wa Waamoni ambao waliishi upande wa mashariki wa mto Yordani.]
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu.
Kwa sababu hiyo nitawapeleka mateka mbali kupita Babuloni!’
44Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema la maamuzi. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichooneshwa.[#7:44 Au: neno kwa neno: Hema la ushuhuda. Tofauti na maskani au hema la mungu Moloki katika aya 43 (ling na Kut 26). Stefano anasema juu ya hema ambalo Mose alitengeneza kulingana na mfano aliooneshwa na Mungu; hilo lilikuwa hema la kufaa.]
45Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi.
46Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo.
47Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
48“Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo:
49‘Bwana asema:
Mbingu ni kiti changu cha enzi
na dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu.
50Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea,
na ni mahali gani nitakapopumzika?
Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?’
51“Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Nyinyi ni kama babu zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu.[#7:51 Neno kwa neno: (Ling na Kut 32:9; 33:3,5; Kumb 10:16; 31:27).; #7:51 Neno kwa neno Msemo unaotokana na Lawi 26:41; Yer 4:4; 6:10; 9:26.]
52Je, yuko nabii yeyote ambaye babu zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, nyinyi mmemsaliti, mkamuua.[#7:52 Yaani Yesu. Taz Mate 3:13-14 maelezo, na ling na Mate 2:23,36; 3:13-15.]
53Nyinyi mliipokea ile sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii.”[#7:53 Gal 3:19; Ebr 2:2. Kadiri ya mapokeo ya Kiyahudi yanayoungwa mkono kiasi fulani na fasiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) ya Kumb 33:2, Mungu aliwapa watu sheria kwa njia ya]
54Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira.
55Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia wa Mungu.
56Akasema, “Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”[#7:56 Jina la sifa ambalo Yesu alilitumia kujitaja yeye mwenyewe katika Injili; ling na Luka 22:69.]
57Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja,
58wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo.[#7:58 Ya wale waliotoa ushahidi dhidi yake (Mate 22:20) na ambao kadiri ya Kumb 17:7 walikuwa wa kwanza kumpiga mawe huyo aliyeshtakiwa. Haieleweki kwa nini waliweka makoti yao chini ya ulinzi wa Paulo. Wengine wanafikiri yeye alikuwa anasimamia mauaji hayo.; #7:58 Jina la Kiebrania la mtume Paulo (Mate 13:9). Huyo huyo Saulo baadaye ataongoka na kuwa mfuasi mashuhuri wa Yesu na atatumia jina la Paulo.]
59Waliendelea kumpiga Stefano kwa mawe huku akiwa anasali: “Bwana Yesu, ipokee roho yangu!”
60Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: “Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii.” Baada ya kusema hivyo, akafa.[#7:60 Ling na Luka 23:34. Maneno ya mwisho ya Stefano, hapa na katika aya 59, yanatukumbusha yale ya Yesu pale msalabani (taz Mate 6:8 maelezo).]