The chat will start when you send the first message.
1Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa.
Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria.
2Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa.
3Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani.[#8:3 Mate 22:4-5; 26:9-11; Gal 1:13. Paulo mara nyingi atarejea katika maandishi yake tukio hilo anaposema kwamba alilidhulumu Kanisa.]
4Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe.
5Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo.[#8:5 Huyu alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kuhudumu katika kanisa. Taz maelezo ya Mate 6:5.; #8:5 Eneo kati ya Yudea na Galilaya.; #8:5 Yaani Masiha. Kuhusu tumaini la Wasamaria juu ya Masiha, taz Yoh 4:25.]
6Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya.[#8:6 Kulikuwa na uadui kati ya Wayahudi na Wasamaria ambao Wayahudi waliwafikiria kuwa karibu kama wapagani (taz maelezo ya Yoh 4:9 na neno Samaria na Wasamaria katika Fahirisi).]
7Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa.
8Kukawa na furaha kubwa katika mji ule.
9Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu.[#8:9-10 Anajulikana kuwa “mchawi” kwa matendo yake ya uchawi na (taz pia wengine wanaotajwa namna hiyo katika Mate 13:6).]
10Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’”
11Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu.
12Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume.
13Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika.
14Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma huko Petro na Yohane.
15Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu;
16maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa amemshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu.
17Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu.[#8:17 Mate 19:6. Kuhusu kuwawekea watu mikono taz Mate 6:6 maelezo.]
18Hapo Simoni aling'amua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema,
19“Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu.”
20Lakini Petro akamjibu, “Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!
21Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu.
22Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo.
23Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!”
24Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.”
25Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria.
26Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza.” (Njia hiyo hupita jangwani).[#8:26 Tafsiri nyingine yamkini: Kuongoka kwa huyo towashi wa Ethiopia kunadhihirisha pia lile jambo lililosemwa katika Mate 2:39 kwamba ujumbe huo utawafikia wale “walio mbali”.]
27Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa mkurugenzi maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa.[#8:27 Wakati huo eneo ambalo lilijulikana kama Ethiopia lilikuwa sehemu ya mto Nili na huenda lilienea mpaka pande za kusini hadi Ethiopia na Eritrea ya sasa (ling Zab 68:31; Sef 3:10).; #8:27 Ilikuwa jambo la kawaida kwa mtu aliye towashi kupewa madaraka makubwa hasa katika makao ya kifalme.; #8:27 Neno kwa neno: malkia wa nchi hiyo walipewa jina la sifa; #8:27 Yamkini huyo Mwethiopia hakuwa na dini maalumu lakini aliithamini dini ya Wayahudi. Yafaa lakini kusema kwamba towashi akiwa ni mtu ambaye amehasiwa alikuwa ametengwa na mambo ya kidini kama vile ibada ya Waisraeli (Kumb 23:1; lakini ling na Isa 56:3-5).]
28Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya.[#8:28 Au: kama ilivyokuwa hapo kale.]
29Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo.”
30Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo unayosoma?”
31Huyo mtu akamjibu, “Ninawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye.
32Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:
“Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa;
kimya kama vile mwanakondoo anapokatwa manyoya,
yeye hakutoa sauti hata kidogo.
33Alifedheheshwa na kunyimwa haki.
Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake,
kwa maana maisha yake yameondolewa duniani.”
34Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, “Niambie, huyu nabii anasema juu ya nini? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?”
35Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu.
36Walipokuwa bado wanaendelea na safari, walifika mahali penye maji, na huyo ofisa akasema, “Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?”[#8:36 Baadhi ya hati za mkono zina aya 37:]
38Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo towashi wakashuka majini, naye Filipo akambatiza.
39Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo towashi hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake mwenye furaha.
40Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Injili mpaka alipofika Kaisarea.[#8:40 Au: Ashdodi katika A.K., mahali kaskazini mwa Gaza, katika pwani ya Palestina ya Mediteranea. Filipo alipitia kwa wakazi wa sehemu hiyo hata akafika Kaisarea ambapo kulikuwa makao yake kadiri ya Mate 21:8.]