The chat will start when you send the first message.
1Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa. Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi, wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli.[#1:1 Mji huu ulikuwa mji katika eneo la milima la Yuda kusini mwa Yerusalemu (2Sam 14:1-4; 2Nya 11:5-6).; #1:1 Kuna kumbukumbu, kutokana na uvumbuzi wa mambo ya kale (Akiolojia) katika mji wa Hazori, kwamba kulitokea tetemeko la ardhi mwaka 760 K.K. na huenda ndilo linalohusika hapa.; #1:1 Mfalme Uzia (2Fal 15:1-7; 2Nya 26:1-24; Isa 6:1) alitawala mwaka 781-740 K.K. katika utawala wa kusini wa Yuda, naye Yeroboamu II (2Fal 14:23-29) alitawala mwaka 783-743 katika utawala wa kaskazini Israeli.]
2Amosi alisema hivi:
Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni,
anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu,
hata malisho ya wachungaji yanakauka,
nyasi mlimani Karmeli zinanyauka.
3Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena;
kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu;
waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya.
4Basi, nitaishushia moto ikulu ya mfalme Hazaeli,[#1:4 Matumizi ya moto mara nyingine huwa na maana yake halisi na mara nyingine maana ya mfano au ishara, kwa Amosi matumizi hayo yanaashiria hasira ya Mungu. Rejea Amo 1:4,7,10,12; 2:2,5; 5:6; 7:4.]
nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi.
5Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko,
na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni,
pamoja na mtawala wa Beth-edeni.
Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
6Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Gaza wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka watu kabila zima,
wakawauza wawe watumwa kwa Waedomu.
7Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Gaza,
nao utaziteketeza kabisa ngome zake.
8Nitawang'oa wakazi wa mji wa Ashdodi,
pamoja na mtawala wa Ashkeloni.
Nitanyosha mkono dhidi ya Ekroni,
nao Wafilisti wote waliosalia wataangamia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
9Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Tiro wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka kabila zima hadi Edomu,
wakaukiuka mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya.
10Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Tiro,
na kuziteketeza kabisa ngome zake.”
11Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Edomu wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Waliwawinda ndugu zao Waisraeli kwa mapanga,
wakaitupilia mbali huruma yao yote ya kindugu.
Hasira yao haikuwa na kikomo,
waliiacha iwake daima.
12Basi, nitaushushia moto mji wa Temani,
na kuziteketeza kabisa ngome za Bosra.”
13Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Amoni wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Katika vita vyao vya kupora nchi zaidi,
waliwatumbua wanawake waja wazito nchini Gileadi.
14Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Raba,[#1:14 Huu ulikuwa mji mkuu wa ufalme wa Waamoni, na ambao unaitwa pia Rabat-Amoni. Taz Yer 49:2.]
na kuziteketeza kabisa ngome zake.
Siku hiyo ya vita patakuwa na makelele mengi,
nayo mapambano yatakuwa makali kama tufani.
15Mfalme wao na maofisa wake,
wote watakwenda kukaa uhamishoni.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”