The chat will start when you send the first message.
1Haya ni maneno yaliyoandikwa na Baruku mwana wa Neria, mjukuu wa Maaseya, wa ukoo wa Sedekia, Hasadia na Hilkia. Baruku aliandika haya huko Babuloni[#1:1 Baruku, Neria na Maaseya wanatajwa katika Yer 32:12. Huyu Baruku alikuwa rafiki na katibu wa nabii Yeremia (taz Yer 36:4; 45:1).; #1:1 Kadiri ya Yer 43:6-7, Baruku na Yeremia walipelekwa Misri mara baada ya kuuawa kwa Gedalia ambaye alikuwa mtawala wa mwisho huko Yerusalemu (2Fal 25:22-26).]
2mnamo siku ya saba ya mwezi katika mwaka wa tano baada ya Wakaldayo kuuteka mji wa Yerusalemu na kuuteketeza.[#1:2 Labda ni mwezi wa tano katika kalenda ya Kiebrania (taz 2Fal 25:8; Yer 52:12).; #1:2 Haisemwi ni mwezi gani lakini wengi wanafikiri ni mwezi wa tano katika kalenda ya Kiyahudi (taz aya 8 na rejea 2Fal 25:8 ambapo inasemwa Nebukadneza aliuteketeza mji wa Yerusalemu mnamo mwezi wa tano). Kuhusu “mwaka wa tano”, yaelekea kwamba mwandishi anahesabu tangu mji wa Yerusalemu ulipoteketezwa, yaani mwaka 586; kwa hiyo wakati wenyewe unaotajwa hapa ni mwaka 582 K.K., aghalabu siku ya ukumbusho ya tukio hilo.; #1:2 Mji wa Yerusalemu ulitekwa mnamo mwaka 587 K.K. Kwa hiyo mwaka unaohusika hapa utakuwa yapata mwaka 582 K.K.]
3Baruku aliyasoma maneno haya aliyoandika mbele ya mfalme Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na mbele ya watu wote waliokuja kusikiliza,[#1:3 Jina lingine la Yoakimu, mfalme wa Yuda (taz Yer 22:24-30). Kuhusu aya yote rejea pia 2Fal 24:8-17.]
4na mbele ya wakuu na wana wa wafalme, na wazee; aliyasoma mbele ya watu wote, wakubwa kwa wadogo, ambao waliishi huko Babuloni pande za mto Sudi.[#1:4 Rejea Yer 36:28; 38:6.; #1:4 Mto huo haujulikani; hata hivyo, huenda ni mojawapo ya mifereji iliyopitia mjini Babuloni. Katika Eze 1:1 wale watu waliopelekwa uhamishoni kule Babuloni walikaa kwenye eneo la mto Kebari.]
5Baada ya kuyasikia, waliomboleza, wakafunga chakula na kuomba dua kwa Bwana.[#1:5 Jina hili ambalo ni sawa na jina Mwenyezi Mungu kwa vile ni tafsiri ya Kigiriki ya jina hilo, linatumika mara nyingi sana katia sehemu ya kwanza ya kitabu hiki (1:15—3:8). Katika sehemu nyingine za kitabu hiki majina ya “Mungu” (kwa wingi zaidi), “Mungu wa milele” (4:35) “Mungu mtakatifu” (4:37; 5:5). Jambo hili la mtindo tofauti wa matumizi ya majina ya Mungu limesababisha kufikiri kwamba waandishi tofauti wanahusika.]
6Kisha wakachanga fedha, kila mtu akatoa kadiri ya uwezo wake,
7wakizipeleka Yerusalemu kwa kuhani Yoakimu mwanawe Hilkia, na mjukuu wa Shalumu, na kwa makuhani wengine pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu.[#1:7 Huyu kuhani hatajwi mahali pengine.]
8Siku ya kumi ya mwezi wa Siwani, Baruku alitwaa vyombo vitakatifu vilivyokuwa vimetolewa katika nyumba ya Mungu, akavirudisha nchini Yuda. Vyombo hivyo vya fedha vilikuwa vimetengenezwa na mfalme Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda,[#1:8 Huu ulikuwa mwezi wa tatu katika kalenda ya Kiyahudi (yapata Mei-Juni kadiri ya kalenda yetu). Katika 2Fal haitajwi kwamba mfalme Sedekia alitengeneza vyombo vya fedha mahali pa vile vilivyochukuliwa na majeshi ya Nebukadneza (rejea 2Fal 25:13-16).; #1:8 Katika Ezra 1:7-11 tuna habari kwamba vyombo vitakatifu vilirudishwa Yerusalemu wakati wa mfalme Koreshi.]
9baada ya Nebukadneza mfalme wa Babuloni kumwondoa mfalme Yekonia huko Yerusalemu na kumpeleka Babuloni yeye pamoja na wakuu, wafungwa, wenye mamlaka na watu wengine wa kawaida.[#1:9 Kigiriki. Katika tafsiri nyingine za kale tuna “mafundi”.]
10Basi, watu waliandika hivi:
Hizi ndizo fedha tunazowapelekeeni. Kwa fedha hizo tafadhali, nunueni wanyama wa sadaka za kuteketezwa na za kuondolea dhambi na ubani, mtayarishe na tambiko za nafaka, mzitoe juu ya madhabahu ya Bwana Mungu wetu;
11mwombeeni Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mwanawe Belshaza waishi maisha marefu kama vile mbingu.[#1:11 Ezra 6:10; taz pia 1Tim 2:2 kuhusu kuwaombea walio na mamlaka ya kidunia, na rejea Yer 29:7.; #1:11 Kigiriki ni “Baltasari”. Huyu hakuwa mwanawe Nebukadneza kama inavyotajwa hapa, ila alikuwa mwanawe Nabonido aliyekuwa mfalme wa mwisho katika himaya mpya ya Wababuloni (556-539 K.K.).; #1:11 Kumb 11:21; Ezra 6:10; taz pia Zab 89:29.]
12Hapo Bwana atatujalia nguvu na kuyaangaza macho yetu. Tutakaa chini ya ulinzi mwema wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mwanawe Belshaza na kuwatumikia kwa muda wa siku nyingi na kupata kibali mbele yao.[#1:12 Rejea Zab 13:3 na 19:8 ambapo tafsiri hii inatoa maana ya msemo: “Huyaangazia macho” kama “kumwelimisha mtu”.]
13Hali kadhalika, mtuombee na sisi kwa Bwana Mungu wetu, maana tumetenda dhambi dhidi yake Bwana Mungu wetu na mpaka hivi sasa ghadhabu na hasira yake bado vinatukabili.
14Tafadhali, someni kitabu hiki tunachowapelekeeni, mkaungame dhambi zenu nyumbani mwa Bwana siku ya sikukuu ya vibanda na katika sikukuu nyingine.
15Hivi ndivyo mtakavyosema:
“Bwana Mungu wetu ni mwadilifu, lakini sisi tulivyo leo tumejaa aibu! Sisi sote, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu,
16wafalme wetu, wakuu wetu, makuhani wetu, manabii wetu na wazee wetu.[#1:16 Yer 32:32. Katika Yer maneno: “wazee wetu” hayatajwi; badala yake tuna: “watu wa Yuda … na wakazi wa Yerusalemu”; rejea Bar 1:15.]
17Sisi tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.
18Tulimwasi, wala hatukutii sauti ya Bwana Mungu wetu aliposema tuishi kufuatana na amri alizotupa sisi.
19Tangu siku ile Bwana alipowatoa wazee wetu nchini Misri mpaka leo, tumeendelea kukosa utii kwa Bwana Mungu wetu, tukawa wazembe kuhusu jambo la kusikia sauti yake.
20Kwa hiyo, mpaka leo hii tumekabiliwa na balaa na laana zile alizotamka Mose mtumishi wa Bwana kwa amri yake, siku ile alipowatoa wazee wetu nchini Misri ili kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali.[#1:20 Kumb 28:15-68; Lawi 26:14-39.]
21Sisi hatukusikiliza maneno ya manabii ambao Bwana Mungu wetu aliwatuma kwetu.
22Badala yake, kila mmoja wetu amepania kufuata mipango ya moyo wake mwovu, kwa kutumikia miungu mingine na kufanya yaliyo maovu mbele ya Bwana Mungu wetu.