Baruku 5

Baruku 5

1Ee Yerusalemu, vua vazi lako la huzuni na mateso,

ukavae milele uzuri wa utukufu wa Mungu.

2Jivike joho la uadilifu utokao kwa Mungu;

vaa kichwani taji la utukufu wa Mungu wa milele.

3Maana Mungu atadhihirisha fahari yako kila mahali duniani.

4Mungu atakupa jina hili milele:

“Amani kwa uadilifu; fahari kwa uchaji wa Mungu.”

5Inuka, ee Yerusalemu, usimame milimani,

tazama upande wa mashariki,

uwaone watoto wako wamekusanywa kutoka mashariki na magharibi,

kwa amri ya Mungu Mtakatifu.

Wanashangilia kwani Mungu amewakumbuka.

6Waliondoka kwako kwa miguu,

wakichukuliwa na maadui zako.

Lakini Mungu atawarejesha tena kwako

wakiwa wamebebwa kwa fahari kama juu ya kiti cha enzi cha mfalme.

7Mungu ametoa amri:

milima na vilima visawazishwe, na mabonde yafukiwe, nchi yote iwe tambarare,

Waisraeli watembee salama kwa utukufu wa Mungu.

8Kwa amri ya Mungu,

vichaka na miti itoayo harufu nzuri itawapa kivuli Waisraeli.

9Mungu atawaongoza Waisraeli kwa furaha;

kwa mwanga wa utukufu wake, kwa uadilifu utokao kwake mwenyewe.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania