The chat will start when you send the first message.
1Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Yehoyakimu wa Yuda, mfalme Nebukadneza wa Babuloni alikwenda Yerusalemu, akauzingira mji.[#1:1 Huyu alikuwa mfalme wa Yuda mnamo 609-598 K.K. “mwaka wa tatu wa utawala” wake utakuwa ni mwaka 606 K.K.; #1:1-21 Hili ni simulizi ambalo linaonesha jinsi kushika sheria kwa uaminifu kunavyoweza kutuzwa.]
2Bwana akamwacha Yehoyakimu atiwe mikononi mwa mfalme Nebukadneza pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu. Basi mfalme Nebukadneza akachukua mateka na vyombo akavipeleka nchini Shinari, akaviweka katika hazina ya miungu yake.[#1:2 Ripoti ya kukamatwa kwa Yehoyakimu inasimuliwa katika 2Fal 24:1 na 2Nya 36:5-7. Kulingana na 2Fal 24:8-16, mfalme Nebukadneza II aliuteka mji wa Yerusalemu mwaka 587 au 586 wakati wa utawala wa Yehoyakini, mwanawe Yehoyakimu. Watu wengi wa Yuda walipelekwa uhamishoni wakati huo kwa sababu waliacha kumtii Mungu (Dan 9:3-14; Yer 25:1-11).; #1:2 Nebukadneza alivichukua vyombo hivyo, akaviweka katika nyumba ya mungu wa Wababuloni aitwaye Marduki na ambaye huitwa pia “Beli”. Taz pia 2Fal 20:17-18; 24:10-16; 2Nya 36:6-7; Isa 39:7-8.; #1:2 Hili lilikuwa jina la kale la Babuloni (Mwa 10:10; 11:2; Isa 11:11).]
3Mfalme Nebukadneza akamwamuru Ashpenazi, towashi wake mkuu, amchagulie baadhi ya vijana wa Israeli wa jamaa ya kifalme na ya watu mashuhuri.
4Mfalme alitaka vijana wasio na kasoro, wazuri kwa umbo, wenye uzoefu wa kila hekima, wenye akili na maarifa na wanaofaa kutoa huduma katika ikulu. Alitaka pia vijana hao wafundishwe kusoma na kuandika lugha ya Wakaldayo.[#1:4-5 Lugha iliyotumika huko Babuloni kwa kawaida ilikuwa Kiaramu.]
5Mfalme aliagiza vijana hao wapewe chakula bora ambacho yeye mwenyewe alikula na divai ambayo alikunywa. Vijana hao walitakiwa wapewe mafunzo kwa miaka mitatu, kisha wapelekwe kwa mfalme.
6Miongoni mwa vijana waliochaguliwa walikuwa Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, wote wa kabila la Yuda.[#1:6 Maana ya jina hili ni “Mungu wangu ni hakimu”. Jina Hanania lina maana ya “Mungu ameonesha neema”; na Mishaeli lina maana ya “Alivyo Mungu ni nini?”. Nalo jina Azaria lina maana ya “Mwenyezi-Mungu husaidia”.]
7Huyo towashi mkuu akawapa majina mengine; Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki na Azaria akamwita Abednego.[#1:7 Majina hayo yanawekwa sambamba na majina ya Kibabuloni waliyopewa ambayo yanahusishwa na miungu ya Wababuloni. Jina jipya la Danieli: Belteshaza lilikuwa na maana ya kitu kama: “Beli amlinde” (4:8). Na jina Abednego huenda linajumuisha jina la mungu Nebo.]
8Lakini Danieli aliamua kutojitia unajisi kwa kula chakula bora cha mfalme na kunywa divai yake. Kwa hiyo, alimwomba towashi mkuu amruhusu asile vitu hivyo na kujitia unajisi.[#1:8 Katika sheria ya Mose Waisraeli walikatazwa kula vyakula fulani fulani (Lawi 11; Kumb 14:3-21). Inawezekana kwamba mila za kidini za Wababuloni za kuwatambikia miungu yao sehemu fulani ya vyakula vyao ndizo zilizowafanya akina Danieli kuviona vyakula hivyo kuwa najisi.]
9Basi, Mungu akamjalia Danieli kupendelewa na kuhurumiwa na Ashpenazi, towashi mkuu.[#1:9 Upendeleo wa Ashpenazi kwa Danieli unafanana na upendeleo aliopewa Yosefu kule Misri (Mwa 39:4,21).]
10Lakini, towashi mkuu akamwambia Danieli, “Nina hofu kwamba bwana wangu mfalme ambaye ametoa maagizo kuhusu chakula na vinywaji unavyopaswa kutumia, ataona kuwa afya yako si nzuri kama ya wenzako wa rika lako. Hivyo maisha yangu yatakuwa hatarini.”
11Hapo Danieli akamwendea mtumishi aliyewekwa na towashi mkuu kumlinda yeye na wenzake kina Hanania, Mishaeli na Azaria, akamwambia,
12“Tafadhali utujaribu, sisi watumishi wako kwa muda wa siku kumi kwa kutupa mboga za majani na maji.
13Kisha, tulinganishe sisi na hao vijana wengine wanaokula chakula cha mfalme, halafu utoe uamuzi wako kulingana na jinsi utakavyoona.”
14Mlinzi akakubaliana nao, akawajaribu kwa muda wa siku kumi.
15Baada ya siku hizo kumi, aliwaangalia akaona kuwa wale vijana waliokula mboga za majani walionekana wenye afya na nguvu kuliko wale wengine wote waliolishwa chakula cha kifalme.
16Basi, yule mlinzi akawaacha waendelee kula mboga za majani badala ya chakula cha fahari na divai.
17Mungu aliwajalia vijana hao wanne maarifa na ujuzi katika elimu na hekima. Zaidi ya hayo, alimjalia Danieli kipawa cha kufasiri maono na ndoto.
18Muda ulipotimia ambapo hao vijana wangepelekwa kwa mfalme kama alivyokuwa ameagiza, yule towashi mkuu akawapeleka vijana wote mbele ya Nebukadneza.
19Mfalme alipozungumza nao wote, hakuna walioonekana kuwa bora kama Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Basi, wakakubaliwa kumhudumia mfalme.
20Jambo lolote la hekima au maarifa ambalo mfalme aliwauliza alijionea mwenyewe kwamba vijana hao wanne walikuwa bora mara kumi kuliko waaguzi na wachawi wote katika utawala wake.
21Danieli alidumu katika huduma ya ikulu mpaka mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.[#1:21 Mtawala huyu mkuu aliishinda nchi ya Babuloni mnamo mwaka 539 K.K. (Ezra 1:1 maelezo). Wakati huu Danieli ambaye alipelekwa uhamishoni Babuloni mnamo mwaka 606 K.K. (1:2) akiwa na umri upatao labda miaka 20, angekuwa na umri wa miaka 90.]