Danieli 12

Danieli 12

Wakati wa mwisho

1“‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa.[#12:1 Katika sura iliyotangulia kulikuwa na vita vya watawala wa kidunia, lakini sasa itakuwa vita ambayo itafanywa na mjumbe wa Mungu ambaye alikwisha kuwa pamoja na Danieli katika sehemu hiyo iliyotangulia akimweleza mambo. Si dhahiri kwamba anakuja wakati wa Antioko IV Epifane au ni wakati mwingine baadaye. Na kuhusu hicho “kitabu cha uhai” rejea 7:10 na 10:20-21 maelezo.]

2Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele.[#12:2 Hapa ni mahali pekee ambapo panasema wazi wazi juu ya kufufuka kwa wema na wabaya.; #12:2 Fungu hili la maneno muhimu kabisa katika theolojia linatajwa hapa kwa mara ya kwanza katika Biblia.]

3Wale wenye hekima watang'aa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watang'aa kama nyota milele.

4Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”

5“Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.[#12:5 Yamkini malaika wengine wawili. Hao wawili ni mashahidi wa ujumbe anautangaza yule malaika (12:7). Kadiri ya sheria ya Mose mashahidi wawili walitakiwa kuthibitisha jambo au tukio fulani (Kumb 19:15).]

6Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe?

7Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’

8Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’

9Akanijibu, ‘Danieli, sasa nenda zako, kwani maneno haya ni siri na yamefungwa kwa kutiwa mhuri mpaka wakati wa mwisho.

10Watu wengi wataondolewa uchafu, watatakaswa na kusafishwa. Lakini watu waovu wataendelea kutenda uovu. Hakuna hata mmoja wa hao waovu atakayeelewa; wenye hekima ndio watakaoelewa.

11“‘Tangu wakati wa kukomeshwa kwa sadaka za kuteketezwa kila siku, yaani kutoka wakati ule chukizo haribifu litakaposimamishwa itakuwa muda wa siku 1,290.

12Heri yao watakaostahimili mpaka siku zile 1,335 zitakapotimia.

13“‘Lakini wewe, ee Danieli, jiendee, ukapumzike kaburini, na wakati huo utakapotimia, utafufuka na kupata tuzo lako.’”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania