The chat will start when you send the first message.
1Mnamo mwaka wa pili wa utawala wake, mfalme Nebukadneza aliota ndoto, akawa na wasiwasi sana rohoni hata usingizi ukamtoweka.[#2:1 Yaani mwaka 604 au 603 K.K.; #2:1-23 Simulizi hili la ndoto na jinsi Danieli alivyoifumbua linakumbusha kisa cha Yosefu na mfalme wa Misri (Mwa 41).]
2Basi, mfalme akaamuru waganga, walozi na wachawi wa Wakaldayo waletwe ili wamfasirie ndoto yake. Wote wakaja na kusimama mbele yake.[#2:2 Katika 2:10 inaonekana kwamba vikundi hivyo tofauti vilikuwa na majukumu au kazi zao tofauti ila wote walidhaniwa kuwa na uwezo au ujuzi fulani wa kubashiri.]
3Mfalme Nebukadneza akawaambia, “Niliota ndoto, nayo inanipa wasiwasi, nami nataka nijulishwe tafsiri yake.”
4Wale Wakaldayo wakamwambia mfalme kwa Kiaramu, “Uishi, ee mfalme! Tusimulie ndoto yako nasi watumishi wako tutakufasiria.”[#2:4 Tangu aya hii mpaka mwishoni mwa sura ya 7 lugha inayotumika ni Kiaramu na sio Kiebrania (taz Utangulizi), lugha ya kawaida ya mawasiliano na biashara katika nchi nyingi za Mashariki ya Kati ya Kale wakati huo. “Uishi ee mfalme!”: Namna ya kawaida ya kuwasalimu wafalme wa Persia kwa muda mrefu.]
5Mfalme akawaambia, “Nimetoa kauli yangu kamili: ikiwa hamtanijulisha ndoto yenyewe na maana yake, mtang'olewa viungo vyenu kimojakimoja, na nyumba zenu zitabomolewa.
6Lakini mkiniambia hiyo ndoto na maana yake, nitawapa zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi, nijulisheni ndoto hiyo na maana yake!”
7Wao wakamjibu mara ya pili, “Mfalme, tusimulie ndoto hiyo, nasi watumishi wako tutakufasiria.”
8Hapo mfalme akawakatiza kwa kusema, “Najua kweli kwamba mnajaribu kupoteza wakati kwa kuwa mnaona kwamba nilikwisha toa kauli yangu kamili,
9kwamba msiponijulisha ndoto hiyo, adhabu yenu ni moja. Mmepatana kunidanganyadanganya na kunilaghailaghai huku muda unapita. Niambieni ndoto hiyo, nami nitajua kuwa mnaweza kunijulisha maana yake.”
10Wale Wakaldayo wakamjibu: “Mfalme, hakuna mtu yeyote duniani awezaye kutimiza matakwa yako. Hakuna mfalme yeyote, hata awe mkuu na mwenye nguvu kiasi gani aliyepata kuwauliza waganga au walozi au Wakaldayo jambo kama hilo.
11Jambo unalouliza, ee mfalme, ni gumu. Hakuna mtu anayeweza kukufunulia isipokuwa miungu peke yake ambayo haikai miongoni mwa wanaadamu.”
12Kusikia hivyo, mfalme Nebukadneza alikasirika na kughadhibika sana, akaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waangamizwe.
13Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe.
14Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni,
15akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote.
16Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake.
17Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.
18Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni.[#2:18 Hili ni jina la sifa la Mungu ambalo lilitumika mara nyingi katika maandishi ya wakati wa himaya ya Persia 539-333. Linatumiwa karibu mara ishirini na mbili katika A.K. (mara kumi na saba katika vitabu vya Ezra, Nehemia na Danieli kwa pamoja). Neno “fumbo” ambalo linatumiwa mara tatu tu A.K. (Dan 2:18 na Marko 4:11 katika Danieli linatumika kwa maana yake ya awali, yaani kitu ambacho hakiwezi kuelezwa au kutatuliwa kwa kutumia akili ya kibinadamu ila tu kwa ufunuo wa kimungu (taz Dan 2:18-19,28-30; 4:9 na Marko 4:11).]
19Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni,
20akasema,
“Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu.
Hekima na nguvu ni vyake.
21Hubadilisha nyakati na majira,
huwaondoa na kuwatawaza wafalme.
Wenye busara huwapa hekima,
wenye maarifa huwaongezea ufahamu.
22Hufunua siri na mafumbo,
ajua kilichoko gizani,
mwanga wakaa kwake.
23Kwako, ee Mungu wa wazee wangu,
natoa shukrani na kukusifu,
maana umenipa hekima na nguvu,
umetujulisha kile tulichokuomba,
umetujulisha kile kisa cha mfalme.”
24Basi, Danieli akamwendea Arioko aliyekuwa ameteuliwa kuwaangamiza wenye hekima wa Babuloni, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babuloni, ila nipeleke mimi mbele ya mfalme, nami nitamweleza maana ya ndoto yake.”
25Basi, Arioko akampeleka Danieli mbele ya mfalme kwa haraka na kumwambia, “Nimempata mtu fulani miongoni mwa mateka wa Yuda anayeweza kukufasiria ndoto yako, ee mfalme.”
26Mfalme akamwuliza Danieli, ambaye pia aliitwa Belteshaza, “Je, unaweza kunijulisha ndoto niliyoota na maana yake?”
27Danieli akamjibu mfalme, “Hakuna wenye hekima, wachawi, waganga wala wanajimu wanaoweza kukujulisha fumbo hilo lako.
28Lakini, yuko Mungu mbinguni ambaye hufumbua mafumbo, naye amekujulisha, ee mfalme Nebukadneza, mambo yatakayotukia siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyokujia kichwani mwako ulipokuwa umelala ni haya:[#2:28-30 Taz 2:18 maelezo kuhusu “fumbo”.]
29Kwako ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani mwako, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotukia baadaye; naye Mungu afumbuaye mafumbo, alikuonesha yale yatakayotukia.
30Lakini mimi sikufumbuliwa fumbo hili kwa sababu nina hekima kuliko wanaadamu wengine, bali ili wewe mfalme, upate kujulishwa maana ya ndoto yako na kujua mawazo yako.
31“Katika ndoto yako, ee mfalme, uliona sanamu kubwa, yenye nguvu na iliyong'aa sana, imesimama mbele yako. Sanamu hiyo ilikuwa ya kutisha mno.
32Kichwa cha sanamu hiyo kilikuwa cha dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha na tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba.
33Miguu yake ilikuwa ya chuma na nyayo zake zilikuwa za mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi.
34Ukiwa bado unaangalia, jiwe liling'oka lenyewe, bila kuguswa, na kuipondaponda miguu ya shaba na udongo wa mfinyanzi ya ile sanamu, na kuivunja vipandevipande.
35Mara kile chuma, udongo wa mfinyanzi, shaba, fedha na dhahabu, vyote vikavunjika vipandevipande na kuwa kama makapi ya mahali pa kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperushia mbali kisibakie hata kipande kimoja. Lakini lile jiwe lililoivunja ile sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.[#2:31-35 Vitu vilivyotumiwa kutengenezea sanamu hiyo vina thamani yake ambayo inapungua na kuonesha kwa namna hiyo kupungua kwa tawala nne zinazohusika.]
36“Hiyo ndiyo ndoto yako, ee mfalme. Na sasa tutakupa maana yake.
37Wewe, ee mfalme, mfalme wa wafalme! Mungu amekupa ufalme, uwezo, nguvu na utukufu![#2:37 Katika Biblia, Mungu anasemekana kuwapa wafalme wa dunia uwezo wa kutawala, hata wale ambao hawamtambui kama Mungu wao (taz Isa 45:1-4; Yer 27:5-7; Rom 13:1).]
38Amekupa mamlaka juu ya wanaadamu wote, wanyama wa porini na ndege wote wa angani, kokote kule waliko. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu!
39Baada yako utafuata ufalme mwingine, lakini ufalme huo utakuwa dhaifu. Huu utafuatwa na ufalme wa tatu unaofananishwa na shaba; huo utaitawala dunia yote.
40Baada ya falme hizo, utafuata ufalme mwingine imara kama chuma. Na kama vile chuma kivunjavyo na kupondaponda vitu vyote, ndivyo ufalme huo utakavyovunjavunja na kusagilia mbali falme zilizotangulia.[#2:39-45 Falme tatu zinatajwa. Wafafanuzi wengine wanafikiri yahusu kwanza utawala wa Wababuloni (chini ya Nebukadneza II); kisha utawala wa Wamedi, kisha utawala wa Wapersi na mwishowe utawala wa Wagiriki. Iwe iwavyo, katika 5:31 anatajwa mfalme Dario, Mmedi ambaye alitawala baada ya utawala wa Wababuloni na kabla ya utawala wa Koreshi, Mpersi ambaye aliwaruhusu Waisraeli kurudi makwao kutoka Babuloni.]
41Uliona pia kuwa nyayo na vidole vya sanamu hiyo vilikuwa nusu udongo wa mfinyanzi na nusu chuma. Hii ina maana kwamba ufalme huo utagawanyika; lakini utakuwa na kiasi fulani cha nguvu za chuma kwa sababu kulikuwa na chuma kilichochanganyikana na udongo wa mfinyanzi.
42Kama ulivyoona, vidole vyake vya miguu vilikuwa nusu chuma na nusu udongo wa mfinyanzi, na hii inamaanisha kwamba ufalme huo utakuwa na nguvu kiasi fulani na udhaifu kiasi fulani.
43Hii inamaanisha kwamba watawala wa ufalme huo watachanganyikana kwa kuoana na watu wasio wa taifa lao, lakini hawatafaulu kuchanganyikana kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.[#2:43 Mnamo mwaka 250 K.K. arusi ilipangwa kati ya himaya ya Misri na ile ya Siria kwa kile kilichokuwa jaribio la bure la kuunganisha tawala hizo mbili.]
44Wakati wa wafalme hao, Mungu wa mbinguni ataanzisha ufalme ambao kamwe hautaangamizwa. Watu wengine hawataushinda na kuutawala ufalme huo, bali ufalme huo utaziponda na kuzikomesha falme zilizotangulia, nao utadumu milele.
45Uliliona jiwe lililong'oka lenyewe toka mlimani, bila kuguswa, na jinsi lilivyoivunja vipandevipande ile sanamu iliyotengenezwa kwa chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu. Ee mfalme, Mungu Mkuu amekufunulia mambo yatakayotukia baadaye. Mimi nimekusimulia. Ndoto yako ni ya kweli na maana yake ni halisi.”
46Ndipo mfalme Nebukadneza alipoanguka kifudifudi na kumsujudia Danieli na kuamuru wamtolee Danieli tambiko na ubani.
47Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika, Mungu wako ni Mungu wa miungu na Bwana wa wafalme, na ndiye afumbuaye mafumbo kwa sababu umefaulu kunifumbulia fumbo hili.”[#2:46-47 Wasomaji Wayahudi wa simulizi hili hapa bila shaka waliona kitendo hicho cha mfalme kuwa ni ishara au mfano wa ushindi wa watu wa Mungu juu ya Babuloni (taz pia Isa 49:23; 60:14).]
48Kisha mfalme Nebukadneza akamtunukia Danieli heshima kubwa, akampa zawadi nyingi kubwakubwa, na kumfanya mtawala wa mkoa wote wa Babuloni, na mkuu wa wenye hekima wote wa Babuloni.
49Danieli akamwomba mfalme, naye mfalme akawaweka Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa mambo ya utawala ya mkoa wa Babuloni. Lakini Danieli akabakia katika jumba la mfalme.