Danieli 7

Danieli 7

Wanyama wanne wakubwa

1Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa mfalme Belshaza wa Babuloni, Danieli aliota ndoto na kuona maono akiwa amelala kitandani mwake. Aliiandika ndoto yake hii:[#7:1 Yaani mwaka 554 au 553 K.K. Matukio yanayoelezwa katika sura ya 7 yalifanyika kabla ya yale ya sura ya 5.; #7:1—12:13 Danieli mwenyewe ndiye anasimulia mambo yanayotukia katika sehemu hii ya pili ya kitabu cha Danieli. Katika 7:2 Danieli anaanza kueleza maono yake na maelezo yanayotolewa na malaika. Maono hayo ni picha ya kufana ya kuanguka kwa madola yaliyofuatana, kuanzia na ufalme wa Babuloni na kubashiri ushindi kwa watu wa Mungu.]

2“Mimi Danieli niliona katika maono usiku, pepo nne toka pande zote za mbinguni zikiichafua bahari kuu.

3Wanyama wakubwa wanne, wakainuka kutoka humo baharini, kila mmoja tofauti na mwenzake.[#7:3-7 Hao wanyama wanawakilisha dola au himaya za kale. Taz pia Ufu 13:1; 17:8. Mnyama wa kwanza anawakilisha ufalme wa Wababuloni (Kumb 2:38-40). Mnyama wa pili anawakilisha ufalme wa Wamedi (taz 2:35-38). Mnyama wa tatu anawakilisha ufalme wa Wapersi. Mnyama wa nne anawakilisha dola lililoanzishwa na Aleksanda Mkuu wa Makedonia ambaye aliwashinda Wapersi mwaka 331.]

4Mnyama wa kwanza alikuwa kama simba, na alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikiwa namwangalia, mabawa yake yaling'olewa, naye akainuliwa na kusimama kwa miguu miwili kama binadamu. Kisha, akapewa akili ya binadamu.

5“Mnyama wa pili alikuwa kama dubu ambaye upande wake mmoja ulikuwa umeinuka. Kinywani mwake alikuwa na mbavu tatu alizozishikilia kwa meno yake. Sauti ikamwambia, ‘Haya, kula nyama nyingi kadiri uwezavyo.’

6“Baada ya hayo, nilimwona mnyama mwingine. Huyu alikuwa kama chui mwenye mabawa manne ya ndege mgongoni mwake. Alikuwa na vichwa vinne na alipewa mamlaka.

7“Kisha, katika maono yangu hayo ya usiku nikamwona mnyama wa nne wa ajabu na wa kutisha, mwenye nguvu sana. Huyu alikuwa na meno makubwa ya chuma ambayo aliyatumia kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Alikuwa tofauti na wale wanyama wengine watatu, kwani alikuwa na pembe kumi.

8Nilipokuwa naziangalia hizo pembe, niliona upembe mwingine mdogo ukiota miongoni mwa zile kumi. Ili kuupa nafasi upembe huu zile pembe nyingine tatu ziling'olewa pamoja na mizizi yake. Ulikuwa na macho ya binadamu na kinywa kilichotamka maneno ya kujigamba.[#7:8 Hapa yamkini anawakilishwa Antioko IV Epifane, mfalme wa Siria (175-164 K.K.) ambaye alishambulia Yerusalemu, akashinda na kuwaua watu wengi. Alijaribu kutokomeza imani ya Wayahudi, akakataza tohara zao na kulitia unajisi hekalu lao. Hiyo ilisababisha uasi ujulikanao kama vita vya Wamakabayo.]

Kuangamizwa kwa wale wanyama

9“Nikiwa bado naangalia, viti vya enzi viliwekwa hapo, kisha ‘Mzee wa kale na kale’ akaja, akaketi. Alikuwa amevaa vazi jeupe kama theluji; nywele zake zilikuwa kama sufu safi. Kiti chake cha enzi kilikuwa cha miali ya moto na magurudumu ya kiti chake yalikuwa ya moto uwakao.[#7:9 Kimoja kwa ajili ya “Mzee wa kale na kale” (taz Ufu 20:4) ambaye yamkini ni Mungu mwenyewe wa milele. Taz pia Isa 6:1-3 na Eze 1:15-28. Na kingine kwa ajili ya mmoja aliye kama “mwana wa mtu” (7:13).]

10Kutoka kiti hicho kijito cha moto kilibubujika, kikatiririka. Maelfu walimtumikia, na mamilioni walisimama mbele yake. Mahakama ikawa tayari kwa kikao, na vitabu vikafunguliwa.[#7:10 Hivi ni vitabu vya hukumu ambavyo vina kumbukumbu za matendo ya kila mtu, mema na mabaya. Mungu hapa anaelezwa kama hakimu. Taz pia Kut 32:32; Zab 56:8; Mal 3:16; Ufu 20:12.]

11“Kutokana na maneno ya kujigamba yaliyokuwa yanasemwa na ile pembe, nikatazama. Nikiwa natazama, huyo mnyama wa nne aliuawa, mwili wake ukaharibiwa na kutolewa uchomwe moto.

12Wale wanyama wengine walinyang'anywa mamlaka yao, lakini wao wenyewe wakaachwa waendelee kuishi kwa muda fulani.[#7:12 Tafsiri yamkini ya makala ngumu. Kiaramu, neno kwa neno: kwa wakati na majira.]

13“Wakati wa maono haya usiku, niliona mmoja kama mwana wa mtu akija katika mawingu, akamwendea yule ‘Mzee wa kale na kale,’ wakanileta mbele yake.[#7:13 Huyu anabainishwa na wale wanyama ambao wanawakilisha tawala za dunia naye anatawazwa mfalme wa utawala wa milele (taz Dan 2:44). Katika A.J. msemo huu unafanana na jina la sifa “Mwana wa Mtu” ambalo Yesu Kristo analitumia kujitaja yeye mwenyewe ili kutilia mkazo hali yake ya kibinadamu na kwamba yeye ndiye aliyekuja kuangamiza utawala wa dhambi na kuanzisha utawala adili na wa milele wa Mungu (taz Mat 24:30; 26:64; Marko 13:26; 14:62; Luka 21:27; Ufu 1:13; 14:14).]

14Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme, ili watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote wamtumikie. Utawala wake ni wa milele na ufalme wake kamwe hautaangamizwa.

Maelezo ya maono ya kwanza

15“Maono niliyoyaona mimi Danieli yalinishtua, nami nikafadhaika.

16Nilimkaribia mmojawapo wa wale waliosimama huko na kumwuliza maana halisi ya mambo hayo yote. Naye akanisimulia na kunieleza maana yake:[#7:16 Huyo huenda ni malaika aliyetumwa kufafanua hayo maono au mmoja wa wale wengi “waliosimama” hapo kutumikia na ambao wametajwa katika 7:10.]

17‘Wanyama hao wanne wakubwa ni wafalme wanne watakaotokea duniani.

18Lakini watakatifu wa Mungu Mkuu watapewa ufalme, nao wataumiliki ufalme huo milele na milele.’

19“Kisha nikataka nielezwe juu ya yule mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti kabisa na wale wengine, wa ajabu na wa kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma na makucha yake ya shaba. Aliyatumia meno hayo kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake.

20Aidha nilitaka nielezwe juu ya zile pembe kumi alizokuwa nazo kichwani mwake, na ule upembe mmoja ambao kabla haujaota, ziling'oka pembe tatu; upembe uliokuwa na macho na kinywa ambacho kilitamka maneno ya kujigamba, na ambao ulionekana kuwa mkubwa kuliko pembe nyingine.

21“Nikiwa bado naangalia, pembe hiyo ilipigana vita na watakatifu, nayo ikawashinda.

22Lakini yule ‘Mzee wa kale na kale’ akainuka, akawapa haki watakatifu wa Mungu na wakati ulipotimia, hao watakatifu wakapewa ufalme.

23“Nikaelezwa hivi: ‘Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaokuwako duniani. Ufalme huo utakuwa tofauti na falme nyingine, nao utaiangamiza dunia nzima. Utaibwaga chini na kuipasua vipandevipande.

24Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huo. Halafu watafuatwa na mfalme mwingine ambaye atakuwa tofauti na wale waliomtangulia, na atawaangusha wafalme watatu.

25Huyo atamkufuru Mungu Mkuu na kuwatesa watakatifu wake. Atajaribu kubadilisha nyakati na sheria zao, na watakatifu watatiwa mikononi mwake kwa muda wa miaka mitatu na nusu.[#7:25 Neno kwa neno: “kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” namna ya kusema juu ya wakati wenye kikomo wa mateso na maumivu (12:7,11; Ufu 11:2-3; 12:14; 13:5).]

26Lakini mahakama itafanya kikao; watamnyang'anya utawala wake, nao utafutwa na kuangamizwa kabisa.

27Ufalme, utawala na ukuu wa falme zote duniani watapewa watu wa watakatifu wa Mungu Mkuu. Ufalme wao utakuwa wa kudumu milele, na tawala zote zitawatumikia na kuwatii.’

28“Huu ndio mwisho wa jambo hilo. Mawazo yangu yalinishtua sana mimi Danieli, hata rangi yangu ikabadilika. Lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania