The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri,[#12:1—13:22 Sura hizi mbili zina ugumu wake wa kipekee kwa vile zinachanganya simulizi la pigo la mwisho na maagizo kuhusu sikukuu ya kidini ambayo kuna tambiko na damu ya kafara inayotumika kama ishara ya kinga (Kut 12:2-14,21-27,43-49), kisha tunapewa kanuni za kuadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu ambayo inaendeleza na kurefusha Pasaka (12:15-20; 13:3-10). Kisha kanuni za kuwaweka wakfu wazaliwa wa kwanza wa kiume zinatangazwa (13:1-2,11-16). Halafu sehemu ya masimulizi hayo inaeleza juu ya pigo la kumi (12:29-36), kisha kuondoka kwa Waisraeli kwa haraka (12:37-42) kuelekea jangwani (13:17-22).]
2“Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka.[#12:2 Mwezi huo, kadiri ya kalenda ya Kiyahudi, ulijulikana kama Abibu, maana yake katika Kiebrania “masikio mapya ya ngano.” Unatajwa pia katika 13:4; 23:15; 34:18; Kumb 16:1. Mwezi Abibu ni wakati tangu katikati ya Machi mpaka katikati ya Aprili katika kalenda yetu. Baada ya Waisraeli kutoka uhamishoni Babuloni ulijulikana pia kama Nisani (taz Neh 2:1; Esta 3:7).]
3Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja.[#12:3 Tafsiri nyingine: mkutano wote wa Israeli. Neno la Kiebrania ni ‘adath’ ambalo lamaanisha mkutano, jumuiya au umati wa watu waliokusanyika pamoja.; #12:3 Ilikuwa kawaida katika Mashariki ya Kati ya Kale kuchinja au kutoa Mwanakondoo kwa sadaka kwa mungu fulani.]
4Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula.
5Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi.
6Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni.
7Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao.
8Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani.
9Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani.
10Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni.
11Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.[#12:11 Hali ya kuwa tayari kwa safari maalumu.; #12:11 Sikukuu ya Pasaka imehusishwa na kukombolewa kwa Waisraeli kutoka utumwani kule Misri. Yenyewe ni ukumbusho wa tukio hilo kwa watu wa Israeli (taz Lawi 23:5; Hes 9:1-5; 28:16; Kumb 16:1-2). Katika A.J. sikukuu hiyo inachukua maana ya pekee kwa Wakristo kwa vile inafafanuliwa kama ishara ya kitendo cha Yesu Kristo cha kuwakomboa binadamu wote. Yeye amekuwa ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu (Yoh 1:29). Taz Mat 26:2-29; 1Kor 5:7; 1Pet 1:18-19; taz pia Yoh 19:14 maelezo.]
12“Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
13Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri.[#12:13 Neno Pasaka linahusiana na neno la Kiebrania “pesah” lenye maana ya 201ckupita” au “kuruka” kitu au mahali. Taz aya 27.]
14Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.”
15Mwenyezi-Mungu akasema, “Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtaondoa chachu katika nyumba zenu. Mtu yeyote akila kitu kilichotiwa chachu katika muda huo wa siku saba, ni lazima aondolewe miongoni mwa Waisraeli.[#12:15 Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu (aya 17) ambayo iliadhimishwa kwa siku saba mara baada ya Pasaka ilikuja kuchukuliwa kama sehemu ya sikukuu hiyo ya Pasaka (Kumb 16:1-8). Taz pia Lawi 23:6-8; Hes 28:17-25.]
16Siku ya kwanza na siku ya saba mtakuwa na mkutano mtakatifu. Katika siku hizo mbili hamtaruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya lazima ya kutayarisha chakula.
17Mtaadhimisha sikukuu hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ukumbusho wa siku nilipowatoa nyinyi, vikundi vya Israeli, kutoka Misri. Sikukuu hiyo itaadhimishwa na vizazi vyenu vyote vijavyo, kama agizo la milele.
18Basi, mtakula mikate isiyotiwa chachu kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huohuo wa kwanza.[#12:18 Ilikuwa kawaida ya Waisraeli kuhesabu siku kuanzia jioni (ling Mat 27:57; Marko 15:42; Luka 23:54; Yoh 19:42).; #12:18 Yaani, mwezi Abibu, yapata Machi-Aprili katika kalenda yetu.]
19Katika siku hizo saba, msiwe na chachu yoyote katika nyumba zenu. Mtu yeyote, awe mgeni au mwenyeji, akila kitu kilichotiwa chachu, ataondolewa miongoni mwa jumuiya ya Waisraeli.
20Popote pale mnapoishi, ni mwiko kabisa kula chochote kilichotiwa chachu. Mnapaswa kula mikate isiyotiwa chachu.”
21Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka.
22Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi.[#12:22 Taz Orodha ya Maneno (Fahirisi). Majani ya mmea huo yalitumika hata kwa kutakasa watu, nyumba, n.k. yakiwa yamechovywa katika damu au maji.]
23Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua.[#12:23 Au: “malaika wa kifo”. Huyo alipewa jukumu la kutekeleza uamuzi au hukumu ya Mungu. Na, labda ilihusu “malaika” kama katika 2Sam 24:16-17; Taz 1Kor 10:10; Ebr 11:28.]
24Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele.
25Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza.
26Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’
27Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu.[#12:27 Kuonesha heshima (taz pia 4:31; Mwa 24:26; 1 Nya 29:20; taz Yoh 19:30).]
28Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.
29Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi-Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri. Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa gerezani. Hata wazaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa.
30Basi Farao, watumishi wake na wakazi wote wa Misri wakaamka usiku. Kukawa na kilio kikubwa nchini kote Misri kwa maana hapakuwa hata nyumba moja ambamo hakufa mtu.
31Hapo Farao akawaita Mose na Aroni, usiku huohuo, akamwambia, “Amkeni! Ondokeni miongoni mwa watu wangu. Nendeni, nyinyi pamoja na hao Waisraeli, mkamtumikie Mwenyezi-Mungu kama mlivyosema.
32Chukueni makundi yenu ya kondoo na ng'ombe, mwondoke; niombeeni na mimi baraka.”
33Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke haraka, wakisema, “Hakika tutakufa sote!”
34Basi, Waisraeli wakauchukua unga wao uliokandwa kabla haujatiwa chachu, na mabakuli yao ya kukandia wakiwa wamezifunga kwa nguo na kubeba mabegani.
35Waisraeli walikuwa wamekwisha fanya kama Mose alivyowaagiza hapo awali: waliwaomba Wamisri wawapatie vito vya fedha, dhahabu na mavazi.
36Naye Mwenyezi-Mungu alikwisha wafanya Waisraeli wapendwe na Wamisri, nao Wamisri wakawapa kila kitu walichoomba. Ndivyo Waisraeli walivyowapokonya Wamisri mali yao.
37Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi, wakasafiri kwa miguu kuelekea Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao 600,000, licha ya wanawake na watoto.[#12:37 Au “Pi-Ramesesi” mji ambao ulijengwa na Farao Ramesesi II (1290-1224 K.K.), ukawa makao yake. Ulikuwa umejengwa kaskazini-mashariki ya Delta ya mto Nili katika nchi ya Gosheni walimokaa Waisraeli (taz Mwa 47:6,27; 46:28-29). Yakobo na watoto wake waliishi karibu na mji huo. Mji wa Ramesesi, kama vile mji wa Pithomu, ulitumiwa na Farao kama mji wa kuwekea akiba ya vyakula.; #12:37 Katika Kiebrania jina hili lina maana ya vibanda. Mji wenyewe labda ulikuwa upande wa mashariki ya Palestina, sio mbali na Bonde la Yordani.; #12:37 Katika Hes 1:46 idadi inayotajwa ni wanaume 603,550 bila kuhesabu wanawake na Walawi 8,580 (taz Hes 4:48).]
38Kulikuwa pia na kundi la watu wengine walioandamana nao pamoja na mifugo mingi, kondoo na ng'ombe.[#12:38 Idadi yao haitajwi wala haisemwi walikuwa akina nani, lakini kwamba jambo hilo limetajwa hapa ni muhimu kwa ajili ya kujifunza historia kamili ya Waisraeli. Hawakuwa tu wazawa wa Yakobo bali pia “makabila” mengine yalijiunga nao.]
39Kwa kuwa walikuwa wameondoka Misri kwa haraka, hawakuweza kutayarisha chakula cha safarini, ila tu ule unga uliokandwa bila kutiwa chachu. Basi, wakaoka mikate isiyotiwa chachu.
40Waisraeli walikuwa wameishi nchini Misri kwa muda wa miaka 430.
41Katika siku ya mwisho ya mwaka wa 430, siku hiyohiyo maalumu ndipo makabila yote ya Mwenyezi-Mungu yaliondoka nchini Misri.[#12:40-41 Taz Mwa 15:13-16; Mate 7:6; na taz Gal 3:17 maelezo.]
42Usiku huo ambao Mwenyezi-Mungu alikesha ili kuwatoa Waisraeli nchini Misri, unapaswa kuadhimishwa na Waisraeli wote na vizazi vyao vyote, kama usiku wa kukesha kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.
43Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Yafuatayo ni maagizo juu ya adhimisho la Pasaka. Mgeni yeyote hatashiriki chakula cha Pasaka.
44Lakini mtumwa yeyote aliyenunuliwa kwa fedha, baada ya kumtahiri, ataruhusiwa kushiriki.
45Msafiri yeyote, wala kibarua yeyote, hatashiriki chakula hicho.
46Mwanakondoo wa Pasaka ataliwa katika nyumba moja. Hamtatoa nyama yoyote nje ya nyumba alimochinjiwa, wala hamtavunja hata mfupa mmoja wa mnyama wa Pasaka.[#12:46 Taz Hes 9:12 maneno ambayo yananukuliwa na kutumiwa juu ya Yesu katika Yoh 19:36.]
47Jumuiya yote ya watu wa Israeli itaadhimisha sikukuu hiyo.
48Mgeni yeyote anayeishi miongoni mwenu akipenda kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, ni lazima kwanza wanaume wote wa nyumba yake watahiriwe; hapo atahesabiwa kuwa kama mwenyeji na kuruhusiwa kushiriki. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa asishiriki kamwe.
49Sheria zilezile zitamhusu mzalendo Mwisraeli na wageni watakaoishi miongoni mwenu”.
50Waisraeli wote walitii sheria hiyo na kufanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Mose na Aroni.
51Siku hiyohiyo Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri kwa makundi.