The chat will start when you send the first message.
1Kutoka jangwa la Sini, jumuiya yote ya Waisraeli ilisafiri hatua kwa hatua kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu, watu wakapiga kambi huko Refidimu. Lakini huko hakukuwa na maji ya kunywa.
2Kwa hiyo watu wakamnung'unikia Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Mose akawauliza, “Mbona mnaninung'unikia? Mbona mnamjaribu Mwenyezi-Mungu?”
3Lakini wote walikuwa na kiu, wakamnung'unikia Mose wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri utuue kwa kiu sisi sote na watoto wetu na mifugo yetu?”
4Basi, Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nitawafanyia nini watu hawa? Wako karibu kunipiga mawe!”
5Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Pita mbele ya watu hawa ukiwachukua wazee wao kadhaa; chukua pia mkononi mwako ile fimbo uliyoipiga nayo mto Nili.
6Tazama mimi nitasimama mbele yako mwambani pale Horebu, nawe utaupiga huo mwamba na maji yatabubujika kutoka humo ili watu wote wapate kunywa.” Basi, Mose akafanya hivyo mbele ya wazee wa Waisraeli.[#17:5-6 Taz Kut 7:20. Na, kuhusu “Horebu” taz Kut 3:1 maelezo. Wakati Mose alipoupiga mto Nili alisababisha maji yake yasiweze kunyweka (Kut 7:14-24); hapa, kwa fimbo ile ile, Mose anaupiga mwamba na kububujisha maji watu wanywe.]
7Mahali hapo Mose akapaita “Masa” na “Meriba”, kwa sababu Waisraeli walimnung'unikia na kumjaribu Mwenyezi-Mungu wakisema, “Je, kweli Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi?”[#17:7 Kiebrania maana ya Masa ni “jaribu”. Meriba ni “kunung'unika”. Majina haya mawili hutajwa pamoja mara kwa mara. Katika mapokeo ya Biblia, Masa na Meriba yamekuwa maneno ishara inayotaja ukosefu wa imani kwa Waisraeli (Kumb 6:16; 9:22; 33:8; Zab 95:8-9; Ebr 3:7-11).]
8Waamaleki walikuja na kupigana na Waisraeli huko Refidimu.[#17:8 Yahusu kabila moja la kusini mwa Palestina ambalo liliishi kwenye eneo la Negebu, karibu na Edomu (Hes 13:29; 1Sam 15:7) na lilimiliki eneo lote mpaka Kadeshi (Mwa 14:7).; #17:8 Mahali ambapo hapajulikani dhahiri lakini baadhi ya wafafanuzi wa Biblia wanafikiri ni kwenye eneo la Mlima Sinai.]
9Mose akamwambia Yoshua, “Chagua wanaume uende ukapigane na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilele cha kilima, nikiishika mkononi mwangu ile fimbo ya Mungu.”[#17:9 Anatajwa hapa mara ya kwanza kama kiongozi wa kikosi cha Waisraeli kwa ushirikiano mkubwa na Mose. Jina “Yoshua” Kiebrania lina maana ya “Mwenyezi-Mungu huokoa”. Aliteuliwa kuwaongoza Waisraeli baada ya kifo cha Mose (Kumb 1:38; 31:14; 34:9).]
10Basi, Yoshua akafanya kama Mose alivyosema, akaenda kupigana na Waamaleki. Mose, Aroni na Huri wakapanda kilele cha kilima.[#17:10 Ni mara ya kwanza jina hili linatajwa. Baadaye, Huri alimsaidia Aroni kuwaamua Waisraeli (taz Kut 24:14). Alikuwa babu wa Bezaleli, fundi stadi aliyeteuliwa kutayarisha hema la mkutano (taz 31:2).]
11Ikawa wakati wote Mose alipoinua mkono wake juu, Waisraeli walishinda, na alipouteremsha, Waamaleki walishinda.
12Lakini baada ya muda, mikono ya Mose ilichoka. Kwa hiyo Aroni na Huri walichukua jiwe wakaliweka karibu na Mose naye akaketi. Kisha wakaishika na kuiinua mikono yake, mmoja akauinua mkono wa kulia na mwingine mkono wa kushoto. Hivyo mikono ya Mose ikabaki imara ikiwa imeinuliwa juu hadi jua lilipotua.
13Yoshua akawakatakata Waamaleki.
14Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Liandike jambo hili katika kitabu, liwe ukumbusho. Tena kariri masikioni mwa Yoshua kwamba nitawafuta kabisa Waamaleki duniani.”
15Mose akajenga madhabahu na kuiita, “Mwenyezi-Mungu ni Bendera Yangu”,
16akisema, “Inueni juu bendera ya Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu atapigana na Waamaleki kizazi hata kizazi!”[#17:16 Makala ya Kiebrania si dhahiri. Lakini kwa jumla inaeleweka na wengi kuwa hapa (na pia katika aya 15) yahusu ishara ya ushindi wa Mungu aliowajalia Waisraeli.]