Kutoka 2

Kutoka 2

Mtoto Mose anaokotwa mtoni Nili

1Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi.[#2:1 Kwa kuzaliwa kwake Mose, historia ya ukombozi wa Waisraeli inaanza, na tangu hapa Mose ndiye mhusika mkuu sio tu katika kitabu cha Kutoka bali hata mpaka kitabu cha Kumbukumbu la Sheria ambacho kina habari za kifo chake (Kumb 34).]

2Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu.[#2:2 Tukio hili linakaririwa na Stefano katika Mate 7:20, na pia mwandishi wa Barua kwa Waebrania (Ebr 11:23).]

3Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani.[#2:3 Aina ya majani yaotayo kandokando ya mto Nili na katika ziwa; mabua yake yalitumika hapo kale kutengenezea karatasi (papiri).]

4Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye.[#2:4 Katika Kut 15:20, dada yake Mose anaitwa nabii Miriamu (taz pia Hes 12:1-16; 26:59; Kumb 24:9; 1Nya 6:3. Taz pia Mika 6:4 ambapo Miriamu anatajwa moja kwa moja kama kiongozi).]

5Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue.

6Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.”

7Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?”

8Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto.

9Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea.

10Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose.[#2:10 Jina “Mose” yamkini ni jina linalotokana na Kimisri hasa kwa vile linaonekana limebandikwa katika majina ya Kimisri kama vile “Tutmosis” na “Amosis”, hapa kwa maana ya “Mtoto wa …”. Maelezo yanayotajwa katika kisa hiki yanalihusisha na maana ya neno kitenzi la Kiebrania linalotamkika karibu hivyo hivyo, na lenye maana ya “vuta nje”, “ng'oa”.]

Mose anakimbilia Midiani

11Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose.[#2:11 Simulizi au hotuba ya Stefano katika Mate 7 inayagawa maisha ya Mose katika sehemu tatu: miaka 40 kule Misri (7:23), miaka 40 kule Midia (7:30), na miaka 40 tangu kutoka Misri. Jumla ni miaka 120 na ni idadi sawa na ile inayotajwa katika Kumb 34:7.]

12Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani.[#2:12 Simulizi hili linataja tu kitendo hiki cha mabavu na kulipiza kisasi kwa upande wa Mose bila kukihalalisha au kukilaani. Lakini mambo yatakayofuata yanadhihirisha kwamba Waisraeli hawawezi kukombolewa kwa mtindo huo wa Mose. Ni kana kwamba itahitaji aitwe na Mungu aweze kutekeleza jukumu la kuokoa katika uonevu.]

13Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?”

14Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!”

15Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani.[#2:15 Wamidiani ni jina la makabila ambayo yalihamahama kwenye eneo la kusini-magharibi ya nchi ya Palestina. Kulingana na Mwa 25:2, Wamidiani walikuwa wazawa wa Abrahamu. Katika Mate 7:23-28 Stefano anasimulia kinaganaga juu ya tukio la Mose la kukimbilia Midiani.]

Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji.

16Basi, binti saba wa kuhani mmoja wa huko Midiani walifika kuchota maji na kuwanywesha kondoo na mbuzi wa baba yao.

17Wachungaji wengine wakaja na kuwafukuza hao binti. Lakini Mose akawasaidia binti hao na kuwanywesha wanyama wao.

18Walipomrudia baba yao Reueli, yeye akawauliza, “Mbona leo mmerudi upesi hivyo?”[#2:16-18 Yamkini huyu ni yule yule anayetajwa kama babamkwe wa Mose (taz aya 21) na anayeitwa Yethro (Kut 3:1; 18:1) na pia Hobabu (Amu 4:11).]

19Nao wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa mikononi mwa wale wachungaji, naye mwenyewe akachota maji na kuwanywesha wanyama wetu.”

20Baba yao akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwiteni aje ale chakula.”

21Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu. Basi, huyo mtu akampa Mose binti yake aitwaye Zipora awe mke wake.[#2:21 Maana ya Zipora ni “ndege”. Huyu alimzalia Mose watoto wawili: Gershomu na Eliezeri (taz Kut 18:1-6).]

22Zipora akamzalia mtoto wa kiume. Mose akasema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni”, kwa hiyo akampa huyo mtoto jina Gershomu.[#2:22 Neno kwa neno maana yake ni “mkimbizi huko”, au “mgeni huko”.]

Kilio cha Waisraeli utumwani

23Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakapiga kite na kulia kutokana na hali yao ya utumwa, na kilio chao kikamfikia Mungu juu.

24Mungu akasikia kilio chao, naye akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu, na Isaka na Yakobo.[#2:24 Ni lile agano Mwenyezi-Mungu alilofanya na Abrahamu (Mwa 12:3; 15:14), Isaka (Mwa 26:2) na Yakobo (Mwa 28:14). Taz pia Mwa 8:1 maelezo.]

25Mungu aliwaangalia Waisraeli, akaona kuwa hali yao ni mbaya.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania