The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoni kwangu, wewe Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli, mniabudu kwa mbali.[#24:1 Hawa walikuwa watoto wa Aroni (Kut 6:23). Hao wawili waliuawa kwa sababu ya kukataa kumtii Mwenyezi-Mungu (Lawi 10:1-2; Hes 3:4; 20:25-28). Na, kuhusu hao “wazee” inaonekana kwamba hawa walikuwa wawakilishi wa watu wote ambao wanatajwa kwa mara ya kwanza katika Kut 3:16 kama “wazee wa Waisraeli”.]
2Wewe Mose peke yako ndiwe utakayenikaribia, lakini wengine wasije karibu, na Waisraeli wasipande mlimani pamoja nawe.”
3Basi, Mose akaenda na kuwaambia watu wote maneno na maagizo yote Mwenyezi-Mungu aliyomwambia. Watu wote wakajibu kwa sauti moja, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.”
4Mose akayaandika maagizo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimpa. Kisha akaamka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili kulingana na idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli.[#24:4 Hapa, katika mazingira ya kuratibisha agano, “madhabahu” inawakilisha Mwenyezi-Mungu. Na hizo nguzo ni ishara wakilishi za ushahidi na pia ukumbusho wa agano lililoadhimishwa mahali hapo. Taz Mwa 31:44-53; Yos 4:7; 24:27.]
5Kisha akawatuma vijana wa Waisraeli wamtolee Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na kumchinjia sadaka za amani za ng'ombe.
6Mose akachota nusu ya damu ya wanyama hao na kuiweka katika mabirika, na nusu nyingine akairashia ile madhabahu.[#24:6 Taz Mat 26:28; Marko 14:24; Luka 22:20; 1Kor 11:25; Ebr 9:19-20; 10:29. Hapa, damu ambayo katika utamaduni wa A.K. ilichukuliwa kuwa ni makao ya uhai, inatumika kuratibisha lile agano na kuweka uhusiano wa kudumu kati ya Waisraeli na Mwenyezi-Mungu.]
7Kisha akachukua kitabu cha agano la Mwenyezi-Mungu, akakisoma mbele ya watu, nao wakasema, “Hayo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya, nasi tutakuwa watiifu.”
8Mose akaichukua ile damu na kuwanyunyizia watu, akisema, “Hii ndiyo damu ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
9Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani,
10wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu.
11Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa.[#24:11 Katika agano na Abimeleki (Mwa 26:26-31) na lile la Yakobo na Labani (Mwa 31:54) kulikuwa pia na chakula na kinywaji cha kushiriki pamoja.]
12Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoo kwangu juu mlimani, ungoje huko. Mimi nitakupa vibao viwili vya mawe vyenye sheria na amri nilizoandika kwa ajili ya kuwafunza Waisraeli.”
13Basi, Mose akaondoka pamoja na Yoshua, mtumishi wake, akaenda kwenye mlima wa Mungu.
14Mose aliwaambia wale wazee, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi; yeyote aliye na tatizo na awaendee wao.”
15Basi, Mose akaenda mlimani, na wingu likaufunika mlima.
16Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatua juu ya mlima Sinai na wingu likaufunika mlima kwa muda wa siku sita. Siku ya saba Mungu akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu.
17Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulionekana mbele ya macho ya watu wa Israeli kama moto unaowaka juu ya mlima.
18Mose akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani. Alikaa huko kwa muda wa siku arubaini, mchana na usiku.[#24:18 Katika aya hii simulizi hili linawekwa kando kwa muda mpaka Kut 32 ambapo panatajwa tena kukaa kwake Mose kule juu mlimani. Na kuhusu muda wa siku “arubaini” taz Mwa 7:12 maelezo.]