Ezekieli 25

Ezekieli 25

Unabii dhidi ya Amoni

1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:[#25:1—32:32 Kama vile katika vitabu vingine vya manabii (hasa Isa 13—21; Yer 46—51; Amo 1—2; Sef 2:4-15), hapa katika kitabu cha Ezekieli tuna mfululizo wa ujumbe wa mashutumu dhidi ya mataifa mengine. Kwa mara nyingi na kwa namna mbalimbali nabii aliwatangazia watu wa Mungu tishio la kuangamizwa kwa sababu ya dhambi zao na kwamba watu wa mataifa mengine ndio watakaotumiwa kama chombo cha ketekeleza adhabu hiyo kutoka kwa Mungu. Walakini, mara baada ya watu wa mataifa mengine kutekeleza adhabu hiyo na kuzidisha maangamizi dhidi ya Yerusalemu na Yuda, nabii anatoa shutuma dhidi ya makosa ya jinai yaliyofanywa na hao watu wa matifa mengine na kuwatangazia adhabu wanayostahili. Baada ya hayo nabii anatangaza kurekebishwa kwa Israeli baada ya kurudi uhamishoni (Eze 33—48).]

2“Wewe mtu! Wageukie Waamoni, ukatoe unabii dhidi yao.

3Waambie Waamoni: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu: Nyinyi mlifurahia kuona maskani yangu ikitiwa unajisi, nchi ya Israeli ikiangamizwa na watu wa Yuda wakipelekwa uhamishoni.

4Basi, nitawatia nyinyi mikononi mwa watu wa mashariki; watapiga hema zao kati yenu na kufanya makazi yao katika nchi yenu. Nao watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu.

5Mji wa Raba nitaufanya kuwa malisho ya ngamia na nchi ya Amoni zizi la kondoo. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

6“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu mlipiga makofi, mkarukaruka kwa furaha na kushangilia sana juu ya nchi ya Israeli,

7basi, mimi nimeunyosha mkono dhidi yenu; nitawaacha mtekwe nyara na watu wa mataifa mengine. Nitawaangamizeni, nanyi hamtakuwa taifa tena wala kuwa na nchi. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Unabii dhidi ya Moabu

8Bwana Mwenyezi-Mungu alisema: “Kwa kuwa Moabu imesema kuwa Yuda ni sawa tu na mataifa mengine,

9mimi nitaifanya miji inayolinda mipaka ya Moabu ishambuliwe, hata miji ile bora kabisa, yaani Beth-yeshimothi, Baal-meoni na Kiriathaimu.

10Nitaitia nchi hiyo pamoja na nchi ya Amoni mikononi mwa watu wa mashariki iwe mali yao. Nchi ya Moabu haitakuwa taifa tena.

11Mimi nitaiadhibu nchi ya Moabu, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Unabii dhidi ya Edomu

12Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Waedomu wamefanya kisasi na Yuda, wakawalipiza watu wa Yuda kisasi kibaya sana

13basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitanyosha mkono dhidi ya nchi ya Edomu na kuwaua watu wote na wanyama. Nitaifanya kuwa ukiwa kutoka mji wa Temani hadi mji wa Dedani, watu watauawa kwa upanga.

14Nitawafanya watu wangu Israeli walipize kisasi juu ya Waedomu nao watawatenda Waedomu kadiri ya hasira na ghadhabu yangu. Ndipo Waedomu watakapotambua uzito wa kisasi changu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”

Unabii juu ya Filistia

15Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Wafilisti walifanya kisasi, wakawalipiza kisasi adui zao kwa ubaya sana na kuendelea kuwa maadui zao daima,

16basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitanyosha mkono dhidi ya Wafilisti; nitawaangamiza hao Wakerethi na wakazi wa pwani.

17Nitawalipiza kisasi kikali kwa adhabu ya ghadhabu. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania