Ezra 1

Ezra 1

Wayahudi wanaamriwa kurudi

1Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia litimie, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake na kuiweka katika maandishi:[#1:1 Mwaka 539 K.K. ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi. Yeye aliushinda utawala wa Babuloni mwezi Oktoba mwaka huo wa 539 K.K. na alitawala Persia tangu mwaka 550 mpaka 530 K.K.; #1:1 Yeremia alikuwa ametoa unabii kwamba Waisraeli wangekaa uhamishoni Babuloni kwa miaka sabini (Yer 25:11-12; 29:10. Taz Dan 9:2). Tangu mwaka 605 K.K. wakati wahamishiwa wa kwanza walipochukuliwa mpaka mwaka 538 K.K. wakati ilani ya Koreshi ya kuwafanya Waisraeli wahamishiwa warudi makwao ilikuwa imepita miaka sitini na saba. Utabiri mwingine waweza pia kutumika kutia mwanga miaka hiyo (Yer 16:14-15; 27:22).]

2“Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni na ameniagiza nimjengee nyumba Yerusalemu, huko Yuda.[#1:2 Jina la sifa ambalo linamtambua Mwenyezi-Mungu kama mwenye uwezo mkuu (5:12; 6:9-10; 7:12,21,23; Neh 1:4-5; 2:4,20; Dan 2:18-19,44; Yona 1:9; Ufu 11:13).; #1:2 Kwamba Koreshi anakiri mamlaka ya Mungu, kwake bila shaka ilikuwa ni jambo la kawaida kwa vile maandishi ya Koreshi yaliyogunduliwa yana maneno hayo hayo au yanayofanana na hayo kuhusu miungu mingine (1:3).; #1:2-4 Ilani hiyo yamkini iliandikwa kwa kusaidiwa na maofisa wa Kiyahudi.]

3Basi sasa, kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake, Mungu wake awe naye na aende Yerusalemu huko Yuda, na kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, Mungu anayeabudiwa huko Yerusalemu.[#1:3 Maneno hayo ni mada muhimu kabisa katika vitabu vya Ezra na Nehemia. Koreshi aliwatendea Waisraeli kama alivyowatendea watu wa mataifa mengine waliokuwa chini ya mamlaka yake. Lengo lilikuwa kuwapata miungu wa watu hao wamfae yeye kwa namna moja au nyingine (taz nia hiyohiyo kuhusu Dario katika 6:10 na Artashasta katika 7:23).]

4Kila mmoja aliyebaki hai uhamishoni akitaka kurudi, jirani zake na wamsaidie kwa kumpa fedha, dhahabu, mali na wanyama, pamoja na matoleo ya hiari kwa ajili ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu.”[#1:4 Katika Kut 12:35-36 Wamisri waliwaachia Waisraeli waondoke na mali nyingi.]

5Basi, wakaondoka viongozi wa koo za makabila ya Yuda na Benyamini, makuhani na Walawi, na kila mtu ambaye Mungu alimpa moyo wa kwenda kujenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, iliyoko Yerusalemu.[#1:5 Hayo mawili ndiyo makabila ambayo eneo lao lilikuwa utawala wa Kusini.]

6Majirani waliwasaidia watu hao kwa kuwapa vyombo vya fedha, dhahabu, mali, wanyama na vitu vingine vya thamani, mbali na vile vilivyotolewa kwa hiari.

7Mfalme Koreshi aliwarudishia vyombo ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuviweka katika nyumba ya miungu yake.

8Alimkabidhi Mithredathi, mtunza hazina, vyombo hivyo, naye akamhesabia Sheshbaza, mtawala wa Yuda.[#1:8 “Sheshbaza” alikuwa amewekwa na mfalme Koreshi kuwa mtawala wa Yuda. Hatujui mengi juu yake lakini anaweza kuwa mtu yule yule ambaye anatajwa kama “Shenazari” katika 1 Nya 3:18 ambaye alikuwa mtoto wa kiume wa nne wa Yehoyakini (aitwaye pia Yekonia). Na huyo “Sheshbaza” anadhaniwa na wataalamu kadhaa wa mambo ya Biblia kuwa ni sawa na Zerubabeli (5:1-3), lakini huenda alikuwa tu afisa mmoja wa Kipersi.]

9Ifuatayo ndiyo hesabu yake:

bakuli 30 za dhahabu;

bakuli 1,000 za fedha;

vyetezo 29;

10bakuli ndogo za dhahabu 30;

bakuli ndogo za fedha 410;

vyombo vinginevyo 1,000.

11Vyombo vyote vya dhahabu na fedha, pamoja na vitu vinginevyo vilikuwa jumla yake 5,400. Vyote hivi, Sheshbaza alivichukua hadi Yerusalemu wakati yeye pamoja na watu wengine alipotolewa uhamishoni Babuloni kwenda Yerusalemu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania