Mwanzo 22

Mwanzo 22

Abrahamu anamtoa Isaka sadaka

1Baada ya muda fulani, Mungu alimjaribu Abrahamu. Mungu alimwita, “Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam nasikiliza.”

2Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, Isaka, mwanao wa pekee umpendaye, uende mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuonesha.”[#22:2 Ndivyo katika Kiebrania lakini tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) badala ya maneno hayo tuna “Mwanao mpendwa”. A.J. linafuata makala ya Septuajinta na kutumia maneno hayo kuhusu Yesu Kristo (Mat 3:17). Taz Efe 1:6.; #22:2 Eneo hilo halijulikani kwa uhakika. Katika 2Nya 3:1 jina la “mlima wa Moria” linataja mahali ambapo Solomoni alijenga hekalu la Yerusalemu.]

3Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu.

4Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali.

5Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.”

6Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja.

7Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?”

8Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao.[#22:8 Katika Kiebrania, maneno “Mungu atajalia” ni jina la Mlima. Na “Moria” linatamkika kama Kiebrania cha “Mungu atajalia”. Kitenzi hicho hicho ‘jalia’ kinatumika pia katika aya ya 14.]

9Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu.

10Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe.

11Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!”[#22:11 Taz Mwa 16:7 maelezo.]

12Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.”

13Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.[#22:13 Kitendo cha kubadili kafara ya binadamu kwa kafara ya mnyama chaweza pia kueleweka kwamba kafara za binadamu hazikubaliki au ni mwiko. Watu wa makabila mengine jirani na Israeli mara kwa mara walitambika kafara za binadamu hasa wakati wa hali ngumu (rejea 2Fal 3:26-27). Tena tunaambiwa mara kadhaa kwamba hata Waisraeli walitambika kafara za binadamu ingawa walikuwa wamekatazwa na sheria ya Mose kufanya hivyo (Lawi 20:1-5). Taz Isa 57:5 maelezo.]

14Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.”

15Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni,

16akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeapa kwa nafsi yangu kwamba kwa kuwa umefanya hivi, wala hukuninyima mwanao wa pekee,

17hakika nitakubariki, na wazawa wako nitawazidisha kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ufuoni mwa bahari. Wazawa wako wataimiliki miji ya adui zao.[#22:15-17 Kutokana na utii wa Abrahamu kwa Mungu, Mungu naye anarudia ile ahadi aliyompa (Mwa 12:2 maelezo; rejea Ebr 6:13-14; 11:12).]

18Kutokana na wazawa wako mataifa yote duniani yatabarikiwa kwa sababu wewe umeitii amri yangu.”[#22:18 Kuhusu ahadi hii taz Mwa 12:2-3 maelezo.]

19Basi, Abrahamu akawarudia wale watumishi wake, nao kwa pamoja wakaondoka, wakarudi Beer-sheba; Abrahamu akakaa huko Beer-sheba.

Watoto wa Nahori

20Baada ya matukio hayo Abrahamu alipata habari kwamba Milka pia amemzalia Nahori, nduguye, watoto wa kiume:

21Usi mzaliwa wa kwanza, Buzi ndugu yake, Kemueli baba yake Aramu,

22Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.

23Bethueli alimzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori, ndugu yake Abrahamu, watoto hao wanane.

24Zaidi ya hayo, Reuma, suria wa Nahori, pia alimzalia watoto: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania