The chat will start when you send the first message.
1Ifuatayo ni orodha ya wazawa wa Adamu. Wakati Mungu alipomuumba binadamu, alimuumba kwa mfano wake.
2Aliwaumba mwanamume na mwanamke, kisha akawabariki na kuwapa jina “Binadamu.”[#5:2 Taz Mwa 1:28 maelezo.]
3Adamu alipokuwa na umri wa miaka 130, alipata mtoto aliyefanana naye, na mwenye sura kama yake; akamwita Sethi.[#5:3 Tafsiri ya neno kwa neno ni “kwa sura yake, kwa mfano wake”. Tafsiri nyingine yamkini ni: “aliyefanana naye kabisa”.]
4Baada ya kumzaa Sethi, Adamu aliishi miaka 800, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
5Adamu alifariki akiwa na umri wa miaka 930.[#5:5 Tatizo la umri wa miaka mingi waliyoishi hao watu kumi tangu Adamu mpaka Noa litaendelea kuwa kitendawili.]
6Sethi alipokuwa na umri wa miaka 105, alimzaa Enoshi.
7Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka 807, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
8Sethi alifariki akiwa na umri wa miaka 912.
9Enoshi alipokuwa na umri wa miaka 90, alimzaa Kenani.
10Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka 815 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
11Enoshi alifariki akiwa na umri wa miaka 905.
12Kenani alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Mahalaleli.
13Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka 840 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
14Kenani alifariki akiwa na umri wa miaka 910.
15Mahalaleli alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Yaredi.
16Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka 830 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
17Mahalaleli alifariki akiwa na umri wa miaka 895.
18Yaredi alipokuwa na umri wa miaka 162, alimzaa Henoki.
19Baada ya kumzaa Henoki, Yaredi aliishi miaka 800 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
20Yaredi alifariki akiwa na umri wa miaka 962.
21Henoki alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Methusela.[#5:21 Huyu Henoki si sawa na Henoki wa Mwa 4:17.]
22Henoki alikuwa mcha Mungu. Baada ya kumzaa Methusela, Henoki aliishi miaka 300 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.[#5:22,24 Katika Kiebrania tuna “Henoki alitembea na Mungu”, yaani katika maisha yake aliiishi kadiri ya matakwa ya Mungu. Katika Mwa 6:9 namna hiyohiyo ya kusema inatumiwa kumtaja Noa kama mtu mwadilifu na mwaminifu kwa Mungu.]
23Henoki aliishi miaka 365.[#5:21-23 Umri wa Henoki wa miaka mia tatu sitini na tano huenda ni idadi ya mfano kwa vile mwaka una siku mia tatu sitini na tano.]
24Alikuwa mcha Mungu, akatoweka, kwa maana Mungu alimchukua.[#5:24 Katika habari za babu Henoki (aya 21-24) maneno haya yanachukua nafasi ya msemo wa kawaida wa kusema alikufa. Hapa bila shaka kuna maana kwamba Henoki alichukuliwa kutoka duniani kwa kitendo cha pekee cha Mungu hivyo kwamba uhusiano wake wa urafiki na Mungu unaendelea baada ya maisha yake ya hapa duniani. Rejea Ebr 11:5. Taz pia kisa cha Elia katika 2Fal 2:11.]
25Wakati Methusela alipokuwa na umri wa miaka 187, alimzaa Lameki.
26Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka 782, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
27Methusela alifariki akiwa na umri wa miaka 969.
28Wakati Lameki alipokuwa na umri wa miaka 182, alimzaa mtoto wa kiume.
29Alimwita mtoto huyo Noa, akisema, “Mtoto huyu ndiye atakayetufariji kutokana na kazi yetu ngumu tunayofanya kwa mikono yetu katika ardhi aliyoilaani Mwenyezi-Mungu.”[#5:29 Jina Noa lina maana ya “pumziko” na linafanana na kitenzi cha Kiebrania cha neno ambalo lina maana ya “atatufariji”. Tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) inatafsiri “atatupa pumziko”.]
30Baada ya kumzaa Noa, Lameki aliishi miaka 595 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
31Lameki alifariki akiwa na umri wa miaka 777.[#5:31 Idadi hiyo yaweza kuwa inatumiwa hapa kama mfano kama hesabu hiyo inavyotumika katika Mwa 4:24.]
32Noa alipokuwa na umri wa miaka 500, alimzaa Shemu na Hamu na Yafethi.