The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mwanamume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi-Mungu ninavyowapenda Waisraeli, ingawa wao wanaigeukia miungu mingine na kuwa na uchu wa maandazi ya zabibu kavu.”[#3:1 Hayo maandazi yaliliwa katika taratibu za tambiko kwa miungu (taz Yer 7:18).]
2Basi, nikamnunua huyo mwanamke kwa vipande kumi na vitano vya fedha na magunia mengi ya shayiri.[#3:2 Maneno hayo yanaweza kumaanisha kwamba mwanamke huyo alikuwa mtumwa wa mtu fulani au mtumwa wa uzinzi katika hekalu la miungu.]
3Kisha nikamwambia, “Lazima uwe wangu kwa siku nyingi bila kufanya uzinzi au kuwa mke wa mtu mwingine; nami pia nitakuwa mwaminifu.”[#3:3 Masharti anayowekewa yana shabaha ya kuondoa ile hali ya uzinzi na hivyo kumrudisha katika hali ya uaminifu tena. Kwa namna hiyo Waisraeli wanaweza kumrudia Mungu tena.]
4Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokuwa: watakaa kwa muda mrefu bila mfalme au mkuu; bila tambiko, wala mnara wala kizibao cha kifuani wala kinyago.[#3:4 Aya hii inatoa maana ya vitendo hivyo vya ishara vilivyotajwa katika aya iliyotangulia kwa watu wa Israeli. Watakaa bila mfalme, bila tambiko na bila mnara … Katika aya hii hatua za adhabu ni wazi na lengo lake ni kurekebishwa kwa watu wa Israeli (aya ya 5).]
5Baadaye, Waisraeli watarudi na kumtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na kumtafuta mfalme wao, mzawa wa Daudi. Ndipo watakapomcha Mwenyezi-Mungu, na kutazamia wema wake siku za mwisho.