The chat will start when you send the first message.
1“‘Twendeni, tukamrudie Mwenyezi-Mungu![#6:1 Taz 2:7; 3:5, ingawa maneno haya huonesha haja ya toba, watu hawa hawakuwa na toba ya kweli. Taz 7:2,9. Wanatubu lakini hawajitambui. Ling 6:2 n.k. Waliamini kuwa Mungu wa Baali aliyekuwa anakufa na kufufuka. Mfano wa toba ya kweli. Taz Luka 15:18; 5:8, ling Zab 51:4 pia 2Kor 7:10.]
Yeye mwenyewe ameturarua,
lakini yeye mwenyewe atatuponya.
Yeye mwenyewe ametujeruhi,
lakini yeye mwenyewe atatibu majeraha yetu.
2Baada ya siku mbili, atatupa uhai tena,
naam, siku ya tatu atatufufua
ili tuweze kuishi pamoja naye.
3Basi tumtambue,
tujitahidi kumjua Mwenyezi-Mungu.
Kuja kwake ni hakika kama alfajiri,
yeye atatujia kama manyunyu,
kama mvua za masika ziinyweshayo ardhi.’”
4Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitakutendea nini ee Efraimu?
Nikufanyie nini ee Yuda?
Upendo wenu kwangu ni kama ukungu wa asubuhi,
kama umande unaotoweka upesi.
5Ndiyo maana nimewavamia kwa njia ya manabii,
nimewaangamiza kwa maneno yangu,
hukumu yangu huchomoza kama pambazuko.
6Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si tambiko,[#6:6 Kuhusu msimamo wa manabii juu ya tambiko na sadaka rejea 1Sam 15:22; Zab 40:6-8; 51:17-19; Isa 1:10-17; Yer 6:19-20; Amo 5:21-24; Mika 6:6-8. Taz pia Mat 9:13 maelezo.]
Kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa.
7“Lakini mlilivunja agano langu
kama mlivyofanya mjini Adamu;
huko walinikosea uaminifu.
8Gileadi ni mji wa waovu,[#6:8 Jina hili kwa jumla linataja eneo la milima kaskazini ambamo kulikuwa na mji uitwao Ramoth-gileadi ambao ulifana kwa ukatili. Yabesh-gileadi ulikuwa mji mwingine, mashariki ya mto Yordani.]
umetapakaa damu.
9Kama wanyang'anyi wamwoteavyo mtu njiani,
ndivyo na makuhani walivyojikusanya na kuvizia.
Wanaua watu njiani kuelekea Shekemu,
naam, wanatenda uovu kupindukia.
10Nimeona jambo la kuchukiza sana
miongoni mwa Waisraeli:
watu wa Efraimu wanakimbilia miungu mingine
naam, Waisraeli wamejitia unajisi.
11Nawe Yuda hali kadhalika,
nimekupangia wakati utakapovuna adhabu.