Isaya 1

Isaya 1

1Maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na mji wa Yerusalemu, nyakati za utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.[#1:1-31 Aya ya kwanza ya sura hii ni utangulizi mfupi kwa kitabu chote cha Isaya. Baada ya utangulizi huo, aya ya 2 mpaka aya ya 31 tunapewa muhtasari wa mahubiri ambayo nabii aliyatoa nyakati tofautitofauti kama yalivyo sasa katika sura 2—39. Katika sura hii ya kwanza nabii anawashtaki watu wa Yuda (ufalme wa kusini) kuhusu dhambi zao na kutangaza hukumu ya adhabu dhidi yao, adhabu ambayo lengo lake ni kutakasa na kurekebisha maisha yao (rejea aya 24—27). Aidha sura hii ya kwanza, kutokana na muundo wake wa kimaandishi, inaashiria dhamira muhimu za fungu la kwanza la kitabu hiki, yaani sura 1—39.; #1:1 Taz pia tangulizi za vitabu vingine vya baadhi ya manabii, hasa Yer 1:1-3; Hos 1:1; Amo 1:1; Mika 1:1. Kwa kawaida muundo wa tangulizi hizo unataja jina la nabii, wakati wa mahubiri yake na mara nyingine walengwa wa mahubiri hayo. Taz pia Isa 2:1.; #1:1 Isaya pia anayo mahubiri yanayowahusu watu wa mataifa mengine (Isa 9:8-21; 13:1—23:18) lakini ni dhahiri kwamba walengwa wa kwanza ni watu wa Yuda na Yerusalemu.; #1:1 Wafalme hao walitawala mmoja baada ya mwingine kati ya mwaka 731 na 687 K.K. Uzia: 2Fal 15:1-7; 2Nya 26:1-23 (taz pia Isa 6:6). Yothamu: 2Fal 15:32-38; 2Nya 27:1-9. Ahazi: 2Fal 16:1-20; 2Nya 28:1-27. Hezekia: 2Fal 18:1—20:21; 2Nya 29:1—32:33.]

Mungu awakemea watu wake

2Mwenyezi-Mungu asema hivi:[#1:2 Kama kawaida katika tafsiri hii hili ndilo jina la Kiswahili linalotumika miongoni mwa Waswahili kumtaja Mungu yule wa pekee ambaye Waisraeli kwa Kiebrania walimtaja kama “Yahweh”. Jina hilo halitumiki kuitaja miungu mingine; hali kadhalika nalo jina Mwenyezi-Mungu halitumiki kuitaja miungu mingine. Ndiyo maana tafsiri hii imeamua badala ya kutumia neno hafifu sana “Bwana” kama ilivyo katika tafsiri nyingine za Kiswahili, neno ambalo lamtambulisha pia mtu yeyote mwanamume, itumie jina la kawaida: “Mwenyezi-Mungu”.]

“Sikilizeni enyi mbingu,

tega sikio ee dunia.

Mimi nimewalea wanangu wakakua,

lakini sasa wameniasi!

3Ng'ombe humfahamu mwenyewe,

punda hujua kibanda cha bwana wake;

lakini Waisraeli hawajui,

watu wangu, hawaelewi!”

4Ole wako wewe taifa lenye dhambi,

watu waliolemewa na uovu,

wazawa wa wenye kutenda maovu,

watu waishio kwa udanganyifu!

Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu,

mmemdharau Mtakatifu wa Israeli,

mmefarakana naye na kurudi nyuma.

5Kwa nini huachi uasi wako?

Mbona wataka kuadhibiwa bado?

Kichwa chote ni majeraha matupu,

na moyo wote unaugua!

6Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu,

umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu,

navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta.

7Nchi yenu imeharibiwa kabisa;

miji yenu imeteketezwa kwa moto.

Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho,

imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma.

8Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani,[#1:8 Jina lingine la mji wa Yerusalemu.]

kama kitalu katika shamba la matango,

kama mji uliozingirwa.

9Mwenyezi-Mungu wa majeshi asingalituachia wachache,[#1:9 Kiebrania “Yahweh Sabaoth”, jina la sifa la kale la kumtaja Mwenyezi-Mungu likigusia uwezo na nguvu zake. Katika jina hili, maneno “wa majeshi” huenda yanahusu majeshi ya Israeli ambayo Mungu aliyaongoza vitani (taz 1Sam 4:4); au, yahusu nyota za angani ambazo zilitajwa kama jeshi, na ambazo Mungu aliziumba. Maneno hayo Mwenyezi-Mungu wa Majeshi yanatumiwa mara kwa mara katika fungu hili la kwanza la kitabu cha nabii Isaya, yaani sura 1—39.]

tungalikwisha kuwa kama watu wa Sodoma,

tungalikuwa hali ileile ya Gomora.

10Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu

enyi watawala waovu kama wa Sodoma!

Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu

enyi watu waovu kama wa Gomora!

11Mwenyezi-Mungu asema hivi;

“Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu?

Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa

na mafuta ya wanyama wenu wanono.

Sipendezwi na damu ya fahali,

wala ya wanakondoo, wala ya beberu.

12Mnapokuja mbele yangu kuniabudu

nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu?

13Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana;

ubani ni chukizo kwangu.

Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya,

Sabato na mikutano mikubwa ya ibada;

sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi.

14Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo

moyo wangu wazichukia.

Zimekuwa mzigo mzito kwangu,

nami nimechoka kuzivumilia.

15“Mnapoinua mikono yenu kuomba

nitauficha uso wangu nisiwaone.

Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia,

maana mikono yenu imejaa damu.

16Jiosheni, jitakaseni;

ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu.

Acheni kutenda maovu,

17jifunzeni kutenda mema.

Tendeni haki,

ondoeni udhalimu,

walindeni yatima,

teteeni haki za wajane.”

18Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Njoni, basi, tuhojiane.

Ingawa mna madoa mekundu ya dhambi,

mtatakaswa na kuwa weupe kama theluji;

madoa yenu yajapokuwa mekundu kama damu,

mtakuwa weupe kama sufu.

19Mkiwa tayari kunitii,

mtakula mazao mema ya nchi.

20Lakini mkikaidi na kuniasi,

mtaangamizwa kwa upanga.

Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.”

Mji uliojaa dhambi

21Jinsi gani mji uliokuwa mwaminifu

sasa umegeuka kuwa kahaba!

Wakati mmoja haki ilitawala humo,

lakini sasa umejaa wauaji.

22Fedha yenu imekuwa takataka;

divai yenu imechanganyika na maji.

23Viongozi wako ni waasi;

wanashirikiana na wezi.

Kila mmoja anapenda hongo,

na kukimbilia zawadi.

Hawawatetei yatima,

haki za wajane si kitu kwao.

24Kwa hiyo asema Bwana Mwenyezi-Mungu,

Mwenye Nguvu wa Israeli:

“Nitawamwagia maadui zangu hasira yangu,

nitawalipiza kisasi wapinzani wangu.

25Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu;

nitayeyusha uchafu wenu kabisa,

na kuondoa takataka yenu yote.

26Nitawapeni waamuzi wenu kama kwanza

na washauri wenu kama pale awali.

Ndipo Yerusalemu utakapoitwa ‘Mji wa Uadilifu’

utaitwa ‘Mji Mwaminifu’”

27Mji Siyoni utakombolewa kwa haki,

uadilifu utawaokoa watakaotubu humo.

28Lakini waasi na wenye dhambi

wote wataangamizwa pamoja;

wanaomwacha Mwenyezi-Mungu watateketezwa.

29Mtaionea aibu hiyo mialoni mliyoipenda sana;

mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizofurahia.

30Mtakuwa kama mwaloni unaonyauka majani;

kama shamba lisilo na maji.

31Wenye nguvu watakuwa kama majani makavu,

matendo yao yatakuwa kama cheche za moto.

Watateketea pamoja na matendo yao,

wala hapatakuwa na mtu wa kuwaokoa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania