Waamuzi 17

Waamuzi 17

Sanamu za Mika

1Kulikuwa na mtu mmoja huko katika milima ya Efraimu, jina lake Mika.[#17:1 Kuna watu kadhaa katika Biblia wanaoitwa “Mika”, jina ambalo lina maana ya “Nani kama Mwenyezi-Mungu?” Mika huyu si sawa na yule nabii Mika ambaye aliishi wakati wa nabii Isaya. Jina hili pia huandikwa kirefu katika Kiebrania kama “Mikeya”.]

2Siku moja alimwambia mama yake, “Vile vipande 1,100 vya fedha ulivyoibiwa, nawe ukamlaani aliyekuibia nikisikia, mimi ninavyo. Mimi ndiye niliyevichukua.” Mama yake akasema, “Mwanangu, ubarikiwe na Mwenyezi-Mungu.”[#17:2 Tamko la mama yake Mika la baraka lina shabaha ya kuondoa au walau kupunguza uzito wa ile laana aliyoitamka wakati zile fedha zilipoibiwa. Iliaminika kwamba laana ikisha tamkwa iliweza kupunguzwa makali yake kwa baraka.]

3Mika akamrudishia mama yake hivyo vipande 1,100 vya fedha. Mama yake akasema, “Ili laana niliyotoa isikupate, fedha hii naiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, ili kutengenezea sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sasa ninakurudishia vipande hivyo vya fedha.”[#17:3 Sanamu hiyo huenda ilikuwa imechongwa kutoka mti kisha ikapakwa dhahabu.]

4Mika alipomrudishia mama yake hiyo fedha, mama yake akachukua vipande 200 vya fedha, akampa mfua fedha, naye akafua sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sanamu hiyo ikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.

5Mtu huyo, Mika, alikuwa na mahali pake pa ibada. Alitengeneza kizibao cha kuhani na kinyago, kisha akamfanya mmoja wa watoto wake kuwa kuhani wake.[#17:5 Taz Amu 8:27.]

6Siku hizo hapakuwepo na mfalme katika Israeli. Kila mtu alifanya chochote alichoona ni chema.[#17:6 Maneno hayo yanatumiwa mara nne katika sura hizi za mwisho za kitabu hiki cha Waamuzi: 18:1; 19:1 na 21:25 ili kutilia mkazo kwamba kabla ya kuweka ufalme katika Israeli kulikuwa na hali ya fujo isiyo na utaratibu wa kisheria. 1 Samueli 8:1-22 inatoa picha hiyo pia.]

7Wakati huo kulikuwa na kijana mmoja Mlawi mjini Bethlehemu nchini Yuda.[#17:7 Katika nyakati za kale wadhifa wa kuhani ulifanywa na Walawi ambao walizunguka huko na huko kutekeleza wajibu wao. Kijana huyo Mlawi hakuwa na makazi ya kudumu: hapo awali alikuwa mkazi wa Bethlehemu ya Yuda, kisha akaajiriwa na Mwefraimu mmoja (aya 8-12) kisha akaambatana na kabila la Dani na kuelekea kaskazini (Amu 18:20).]

8Kijana huyo akaondoka Bethlehemu nchini Yuda, akaenda kutafuta mahali pengine pa kuishi. Katika safari yake akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya milima ya Efraimu.

9Mika akamwuliza, “Umetoka wapi?” Naye akamjibu, “Mimi ni Mlawi, kutoka mjini Bethlehemu nchini Yuda. Nitakaa popote nitakapopata nafasi ya kukaa kama mgeni.”

10Mika akamwambia, “Kaa pamoja nami, uwe kwangu kama baba na kuhani wangu. Nitakulipa vipande kumi vya fedha kila mwaka na mavazi pamoja na mahitaji yako.”[#17:10 Neno “baba” hapa linatumiwa kama jina la sifa kwa mtu anayestahili kuheshimiwa kwa namna ya pekee kama vile ilivyokuwa kwa nabii Elia na Elisha (2Fal 2:12; 6:21; 13:14), kama mfalme (1Sam 24:11) au kwa watu maarufu kama vile Yosefu (Mwa 45:8).; #17:10 Mika alikwisha kumchagua mwanawe kuwa kuhani wa nyumbani kwake lakini sasa anachukua fursa ya kumpata kuhani halali Mlawi na kutumaini kwamba atabahatika.]

11Huyo Mlawi akaingia akakubali, akakaa huko na kuwa kama mmoja wa wana wa Mika.

12Naye Mika akamfanya kijana huyo Mlawi kuwa kuhani wake huko nyumbani kwake.

13Kisha akasema, “Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu atanifanikisha kwani nina kijana huyu Mlawi kama kuhani wangu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania