The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo ambapo hapakuwepo na mfalme katika Israeli, kulikuwa na Mlawi fulani aliyeishi kama mgeni mbali katika eneo la milima ya Efraimu. Mtu huyo alichukua suria kutoka Bethlehemu nchini Yuda.[#19:1 Walawi hawakuwa na sehemu au eneo lao wakati makabila ya Israeli yalipogawiwa maeneo yao. Wao walitawanywa kila mahali miongoni mwa makabila mengine watumikie kama makuhani.; #19:1 Huyo mwanamke kutoka Bethlehemu alikuwa mke wa huyo Mlawi lakini mke wa ngazi ya chini kisheria kama ilivyoruhusu desturi na mila za wakati huo.; #19:1—21:25 Sura hizi za mwisho za kitabu hiki zinaeleza habari za kutisha jinsi makabila mengine ya Waisraeli yalivyopigana na kabila la Benyamini hata karibu kuliangamiza kabisa lakini likaponea chupuchupu. Habari hizo zinaelezwa kwa hatua tatu: 1. Kisa cha vita: uhalifu kule Gibea 2. Mwito wa makabila mengine dhidi ya Benyamini na 3. Kuwapokea tena Wabenyamini baada ya kushindwa.]
2Lakini suria huyo akamkasirikia; huyo Mlawi, akamwacha na kurudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu, akakaa kwa muda wa miezi minne.
3Siku moja, mumewe alikwenda kumtafuta; alikusudia kuongea naye vizuri na kumrudisha nyumbani kwake. Basi huyo mwanamume alikwenda pamoja na mtumishi wake na punda wawili. Basi yule mwanamke akampeleka ndani kwa baba yake, naye baba mkwe wake alipomwona akampokea kwa furaha.
4Baba mkwe wake akamkaribisha, naye akakaa huko kwa muda wa siku tatu; huyo Mlawi na mtumishi wake wakala, wakanywa na kulala huko.
5Siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, wakajitayarisha kuondoka; lakini baba wa yule mwanamke akamwambia, “Kwanza kula chakula kidogo upate nguvu, kisha uondoke.”
6Basi hao watu wawili wakakaa, wakala na kunywa pamoja. Kisha baba mkwe wake akamwambia, “Tafadhali ulale hapa usiku huu na kufurahi.”
7Yule mtu aliposimama akitaka kuondoka, baba mkwe wake akamhimiza abaki, naye akabaki.
8Siku ya tano huyo mtu aliamka asubuhi, akitaka kuondoka. Lakini baba yake yule mwanamke akamwambia, “Kwanza upate nguvu kwa kula, ungoje alasiri, halafu uondoke.” Basi wote wawili wakala pamoja.
9Huyo Mlawi na suria wake pamoja na mtumishi wake walipoinuka kwenda zao, baba mkwe wake akamwambia huyo Mlawi, “Sasa mchana umekwisha na jioni imekaribia. Ulale hapa, na kufurahi. Kesho asubuhi utaamka mapema kuanza safari yako ya kurudi nyumbani.”
10Lakini huyo mtu alikataa kulala huko usiku huo. Basi, akainuka, akaondoka akafika karibu na mji wa Yebusi (yaani Yerusalemu). Alikuwa na wale punda wake wawili waliotandikwa tayari, pamoja na suria wake.[#19:10 Mahali hapo paliitwa hivyo kwa kuwa humo waliishi Wayebusi (taz Yos 15:8; 18:16,28; Amu 1:21). Mji huo ulitekwa na Waisraeli kwa mara ya kwanza wakati wa mfalme Daudi (2Sam 5:6-9).]
11Walipokuwa wamekaribia mjini Yebusi, siku ilikuwa karibu imekwisha; naye mtumishi akamwambia bwana wake, “Sasa heri tuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo usiku huu.”
12Bwana wake akamjibu, “Hatutageuka na kuingia katika mji wa wageni ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea.[#19:12 Kiebrania jina hili lina maana ya “kilima”. Mji huo pia iliitwa “Gibea ya Benyamini” (1Sam 13:2) na “Gibea ya Sauli” (1Sam 11:4). Ulikuwa yapata kilomita 6 kaskazini mwa Yerusalemu.]
13Twende tukaribie sehemu hizo na kulala huko Gibea au Rama.”
14Basi, wakaendelea na safari yao mpaka jua likatua wakiwa karibu na mji wa Gibea ambao ni mji wa kabila la Benyamini.
15Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake.[#19:15 Kwa kawaida hapo kale na hata katika nchi zetu hapo kwanza kuwakaribisha wageni wanaosafiri nyumbani lilikuwa jambo lililotazamiwa.]
16Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini.[#19:16 Hapa mwandishi anaanza kugusia utovu wa Wabenyamini kwani anayemkaribisha huyo msafiri mchovu ni mgeni katika nchi hiyo ya Benyamini (taz pia Mwa 19).]
17Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?”
18Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani; hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake.
19Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.”
20Huyo mzee akamwambia, “Amani iwe nanyi! Nitawapa mahitaji yote. Ila msilale huku uwanjani.”
21Hivyo akawapeleka nyumbani kwake na kuwapa punda wao malisho. Hao wasafiri wakanawa miguu yao, wakala na kunywa.[#19:21 Jambo hilo lilikuwa moja ya matendo muhimu ya kuonesha ukarimu kwa wageni.]
22Walipokuwa wanajifurahisha, kumbe wanaume mabaradhuli wa mji huo wakaja wakaizingira hiyo nyumba na kugonga mlangoni. Wakamwambia mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyekuja kwako, tulale naye.”[#19:22-24 Kwa habari inayofanana na hii kiasi fulani taz Mwa 19:4-8. Kwanza kabisa mwandishi mwenyewe amekwisha wapanga jina hao waovu wa Gibea kuwa ni mabaradhuli (Kiebrania “watoto wa Beliali”) na hivyo kuashiria kisa cha kuchukiza. Pili, jibu la huyo mzee wa nyumba linatokana na mila ya kumlinda mgeni kwa vyovyote vile. Utovu wa maadili wa hao mabaradhuli unamfanya yule mgeni kumtoa suria wake kwao na matokeo yaliyofuata ya kuchukiza. Sheria ya Mose ilipiga marufuku kujamiiana kinyume cha sheria pamoja na kubaka (Kumb 22:22-27) lakini hapa kisa hiki kinaonesha kwamba nyakati hizo kulikuwa na utovu mwingi wa maadili ya sheria.]
23Lakini huyo mzee mwenye nyumba akatoka nje, akawaambia “Sivyo ndugu zangu; nawasihi msitende uovu huo. Huyu ni mgeni wangu, hivyo msimtendee ubaya huo.
24Ninaye bado binti yangu ambaye ni bikira na yupo pia yule suria wa mgeni wangu. Niruhusuni niwatoe nje, muwachukue na kuwatendea kama mnavyotamani; lakini mtu huyu msimtendee jambo hilo la kipumbavu.”
25Lakini wanaume hao hawakumsikiliza. Kwa hiyo Mlawi yule akamchukua suria wake na kumtoa kwao huko nje. Nao wakamchukua na kumnajisi usiku kucha mpaka asubuhi. Karibu na mapambazuko, wakamwacha aende zake.
26Asubuhi, yule mwanamke akaja mpaka mlangoni mwa nyumba alimokuwa bwana wake, akaanguka chini hapo mlangoni na kukaa hapo mpaka kulipopambazuka kabisa.
27Bwana wa mwanamke huyo alipoamka asubuhi, alifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aendelee na safari. Ghafla akamkuta suria wake amelala chini mlangoni, mikono yake ikishika kizingiti cha mlango.
28Akamwambia, “Simama twende.” Lakini yeye hakujibu kitu. Akamchukua, akamweka juu ya punda wake na kumpeleka mpaka nyumbani kwake.
29Alipofika nyumbani kwake akachukua kisu na kumkatakata yule suria vipande kumi na viwili. Kisha akavipeleka vipande hivyo katika maeneo yote ya nchi ya Israeli.[#19:29 Kitendo hiki cha kutisha kinafanyika kuwataka Waisraeli wachukue hatua ya haki. Mauaji ya huyo mama hapa yanachukuliwa sio kama kitendo kinachomhusu mtu mmoja bali kinachoiathiri jumuiya yote ya Waisraeli (rejea pia 1Sam 11:7).]
30Wale wote walioona jambo hilo wakasema, “Jambo kama hili halijawahi kutukia wala kuonekana tangu siku ile Waisraeli walipotoka nchini Misri mpaka leo. Tulifikirie, tushauriane na kuamua.”