Yudithi 14

Yudithi 14

Mpango wa Yudithi

1Ndipo Yudithi akawaambia, “Ndugu zangu, nisikilizeni sasa, kichukueni kichwa hiki na kukitundika kwenye ukuta wa mji.

2Chagueni kiongozi, na asubuhi na mapema jua linapochomoza, wachukueni wanaume mashujaa wakiwa na silaha zao, watoke nje ya mji, kana kwamba wanakwenda bondeni kukishambulia kituo cha Waashuru; lakini msishuke.

3Walinzi wa Waashuru watachukua silaha zao na kukimbilia kambini ili kuwaamsha maofisa wao. Maofisa watakimbia kwenye hema la Holoferne kumwamsha, lakini hawatamkuta. Hapo jeshi lote litaduwaa na kurudi nyuma huku nyinyi mnasonga mbele kuwashambulia.

4Ndipo nyinyi pamoja na Waisraeli wote mtaweza kuwafuatia na kuwaua wanapokimbia.

5Lakini kabla hamjafanya yote haya, nileteeni Akioro, Mwamoni, ili amuone na kumtambua yule mtu aliyewadharau watu wa Israeli, na aliyempeleka Akioro kwetu, akifikiri kuwa Akioro angeuawa.”

Akioro anakuwa Mwisraeli

6Hivyo, wakamwita Akioro kutoka nyumbani kwa Uzia. Lakini alipokuja na kukiona kichwa cha Holoferne mikononi mwa mtu mmoja katika mkutano wa watu alianguka chini na kuzimia.

7Walipomsaidia kusimama wima, Akioro aliinama mbele ya Yudithi mpaka chini, akasema, “Umebarikiwa wewe katika kila jamaa ya Yuda; na katika kila taifa wale watakaosikia jina lako watashikwa na hofu.

8Sasa tafadhali, nieleze yote uliyoyatenda katika siku hizi zilizopita.”

Watu wote wa mji walipokusanyika, Yudithi akaeleza yote, jinsi alivyofanya tangu siku alipoondoka mjini mpaka wakati huo.

9Baada ya kumaliza kuwaeleza, watu walipiga vigelegele vya furaha na mji mzima ukawaitikia.

10Akioro aliposikia yote aliyotenda Mungu wa Israeli, alimwamini Mungu kwa dhati. Akioro akatahiriwa na kufanywa mmoja wa jumuiya ya Kiisraeli, na ndivyo walivyo wazawa wake mpaka leo.

Hofu kambini kwa Holoferne

11Kesho yake asubuhi, Waisraeli wakakitundika kichwa cha Holoferne kwenye ukuta wa mji. Wanaume wote wakatwaa silaha zao na kutoka wakiwa kwenye vikosi vyao. Wakaanza kuiteremka miteremko ya mji.

12Mara Waashuru walipowaona, wakapeleka taarifa kwa wakuu wao, nao wakuu wakawapelekea majenerali wao, makamanda wao wa maelfu na maofisa wengine.

13Hao wakuu wakaenda kwenye hema la Holoferne na kumwambia aliyesimamia shughuli za binafsi za Holoferne, “Mwamshe jemadari! Wale watumwa Waisraeli wamethubutu kushuka huku kutoka mlimani ili kupigana nasi ili waangamie!”

14Bagoa akaingia ndani ya hema na kutikisa pazia ya chumba cha kulala hemani (kwani alidhani Holoferne alikuwa kitandani na Yudithi).

15Lakini alipoona hakuna jibu, alilivuta kwa upande hilo pazia na kuingia ndani. Kutahamaki, akaukuta mwili wa Holoferne bila kichwa kwenye kiti kidogo cha miguu.

16Bagoa akapiga yowe, akatoa kilio cha huzuni, akaomboleza, akapiga kelele na kurarua mavazi yake.

17Akaenda ndani ya hema alimokuwa analala Yudithi, alipoona hayumo alikimbia nje na kuwaita maofisa kwa sauti kubwa,

18“Wale watumwa wametulaghai! Mwanamke mmoja tu Mwisraeli ameuletea aibu ufalme mzima wa Nebukadneza. Tazameni! Holoferne yuko chini, amebaki kiwiliwili tu bila kichwa!”

19Maofisa waliposikia habari hizo, waliyararua mavazi yao kwa huzuni; vilio na makelele yao vilisikika katika kambi nzima.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania