Yobu 14

Yobu 14

1“Mtu ni mtoto tu wa mwanamke;[#14:1 Matumizi ya maneno haya hapa yana shabaha ya kuelezea hali dhaifu ya binadamu.]

huishi siku chache tena zilizojaa taabu.

2Huchanua kama ua, kisha hunyauka.

Hukimbia kama kivuli na kutoweka.

3Ee Mungu, kwa nini unajali hata kumwangalia

na kuanza kuhojiana naye?

4Nani awezaye kutoa kitu kisafi kutoka kitu kichafu?

Hakuna anayeweza.

5Siku za kuishi binadamu zimepimwa;

ee, Mungu umeipanga idadi ya miezi yake;

hawezi kupita kikomo ulichomwekea.

6Angalia pembeni basi, umwache;

ili apate kufurahia siku zake kama kibarua.

7Maana mti ukikatwa lipo tumaini la kuota,

waweza kuchipua tena.

8Japo mizizi yake itazeeka udongoni,

na shina lake kufia ardhini,

9lakini kwa harufu tu ya maji utachipua;

utatoa matawi kama chipukizi.

10Lakini mtu hufa na huo ndio mwisho wake.

Akisha toa roho anabakiwa na nini tena?

11“Kama vile maji yakaukavyo ziwani,

na mto unavyokoma kutiririka,

12ndivyo anavyokufa mtu, wala haamki tena;[#14:12 Katika Agano la Kale jambo la kufufuka kwa wafu na maisha baada ya kifo halikuwa dhahiri, ila tu baadaye. Taz Zab 6:5; 88:10-12; 115:16-17; Isa 38:18. Uhakika wa jambo hili utadhihirika kikamilifu katika A.J. (Mat 13:43; 1Kor 15; Ufu 21—22). Lakini kabla ya A.J. wazo la maisha mapya pamoja na Mungu lilikuwako (taz Zab 16:10; 15; Dan 12:12-13).]

hataamka tena wala kugutuka,

hata hapo mbingu zitakapotoweka.

13“Laiti ungenificha kuzimu;

ungenificha hadi ghadhabu yako ipoe;

nao muda ulionipimia ukiisha ungenikumbuka.

14Je, mtu akifa anaweza kuishi tena?

Siku zangu zote za kazi ningekungoja

hadi wakati wa kufunguliwa ufike.

15Hapo ungeniita, nami ningeitika,

wakati ungetaka kuniona mimi kiumbe chako.

16Ndipo ungeweza kuzihesabu hatua zangu,

ungeacha kuzichunguza dhambi zangu.

17Makosa yangu yangefungiwa katika mfuko,

nawe ungeufunika uovu wangu.

18“Lakini milima huanguka

majabali hung'oka mahali pake.

19Mtiririko wa maji hula miamba,

mvua kubwa hufanya mmomonyoko wa ardhi.

Ndivyo nawe unavyoharibu tumaini la binadamu.

20Wewe wamwangusha binadamu, naye akatoweka milele;

waubadilisha uso wake na kumtupilia mbali.

21Watoto wake wakiheshimika, yeye hana habari.

Wakiporomoshwa, yeye haoni kabisa.

22Huhisi tu maumivu ya mwili wake,

na kuomboleza tu hali yake mbaya.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania