Yona 1

Yona 1

Yona anajaribu kumkwepa Mungu

1Siku moja, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yona, mwana wa Amitai:[#1:1 Taz 2Fal 14:25. Jina “Yona” lina maana ya “njiwa, ndege mjinga”. Nabii anatumia wazo la “njiwa mjinga” kama ishara au mfano wa Israeli (Hos 7:11).]

2“Ondoka uende Ninewi, ule mji mkuu, ukaukemee, maana nimeona uovu wake ni mkubwa mno.”[#1:2 Mji wenyewe ulikuwa mji mkuu wa Ashuru, ufalme ambao mnamo mwaka 721 K.K. uliangamiza ufalme wa kaskazini wa Israeli na kuwapeleka watu wengi wa Israeli uhamishoni (rejea 2Fal 14:1-23). Manabii Nahumu (1:14—3:19) na Sefania (2:13-15) walitangaza kuangamizwa kwa mji huo jambo ambalo lilitukia mwaka 612 K.K. Wakati wa maandishi ya Yona, mji huo ulikuwa mfano na ishara ya ukatili na utumiaji wa nguvu dhidi ya watu wa Mungu. Rejea Nah 1:1; 2:13—3:19.]

3Basi, Yona akaanza safari, lakini akashika njia ya kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Akaenda hadi mjini Yopa ambapo alikuta meli moja iko tayari kwenda Tarshishi. Alilipa nauli, akapanda meli, akasafiri na mabaharia hao kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu.[#1:3 Huo ulikuwa bandari ya bahari ya Mediteranea karibu na Yerusalemu (rejea 2Nya 2:16; Mate 9:36).; #1:3 Ni vigumu kubainisha kwa uhakika mji huo ulikuwa wapi. Wataalamu wengi wa mambo ya Biblia wanafikiri ulikuwa kusini-mashariki mwa Spania.]

Yona anaaibishwa na watu wa mataifa mengine

4Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika.

5Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito.[#1:5 Rejea Mwa 2:21.]

6Nahodha akamwendea, akamwambia, “Wawezaje wewe kulala? Amka umwombe Mungu wako; labda Mungu wako atatuhurumia, tusiangamie.”[#1:3-6 Mabaharia wanamkabili Yona kwa mshangao kama si kwa kuonesha tatizo. Wao walikuwa wenye kuabudu miungu mingi, Yona mwenye kuabudu Mwenyezi-Mungu. Yeye zaidi kuliko wao angalijua la kufanya - kumwomba Mungu wake wakati wa hatari.]

7Mabaharia wakasemezana: “Tupige kura tujue balaa hili limetupata kwa kosa la nani.” Basi, wakapiga kura; kura ikamwangukia Yona.[#1:7 Namna hii ya kupiga kura ilikuwa kawaida hapo kale kujua matakwa ya Mungu (rejea Hes 26:55-56; 1Sam 10:20-21; 14:36-42; Mate 1:26).]

8Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?”

9Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.”[#1:9 Katika A.K. jina hili linatumiwa karibu kila mara na watu wasio Waisraeli na hasa Wamisri (Mwa 40:15; 41:12; Kut 1:16) na Wafilisti (1Sam 4:6,9; 13:3); nao Waisraeli wanajiita hivyo wakati wanapojitambulisha kwa wageni.; #1:9 2Nya 36:23; Ezra 1:2; 5:11; 7:12; Neh 1:4-5; 2:4; Dan 2:18-19. Kwa tamko hili la imani Yona anabainisha dhahiri ukosefu wa uwiano kati ya kitendo chake na imani yake: kwa upande mmoja anakiri ukuu wa Mungu juu ya ulimwengu wote kama “Muumba wa ulimwengu”, lakini kwa upande mwingine anafikiri anaweza kujificha mbali naye (Yona 1:3).]

10Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!”

11Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?”

12Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.”

13Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia.

14Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.”

15Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia.

16Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri.[#1:16 Walifanya hivyo kwa kuogopa kwamba wangeadhibiwa kwa kumtupa Yona majini.]

17Kisha, Mwenyezi-Mungu akaamuru samaki mkubwa ammeze Yona, naye akawa tumboni mwa samaki huyo kwa muda wa siku tatu, usiku na mchana.[#1:17 Haisemwi alikuwa samaki gani; ila inasemwa tu kwamba kupitia kwa huyo samaki Yona anaokolewa kutoka majini ili atimize kazi aliyoagizwa kuifanya.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania