Yona 3

Yona 3

Yona anafuata agizo la Mungu

1Neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yona mara ya pili:

2“Nenda Ninewi, ule mji mkuu, ukawatangazie watu ujumbe niliokupa.”

3Basi, Yona akaondoka, akaenda Ninewi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza.

Mji wa Ninewi ulikuwa mkubwa sana. Upana wake ulikuwa mwendo wa siku tatu.

4Alipowasili, Yona aliingia mjini, na baada ya kutembea mwendo wa siku nzima, akaanza kutangaza: “Bado siku arubaini tu na mji huu wa Ninewi utaangamizwa!”[#3:4 Muda huo unapatikana pia katika nyakati za majaribio (taz Mwa 7:12 maelezo; Amu 3:11 na Kut 24:18).]

5Basi, watu wa Ninewi wakauamini ujumbe wa Mungu, wakatangaza mfungo, na kwamba kila mmoja wao, mkubwa kwa mdogo, avae vazi la gunia kama ishara ya kutubu.

6Habari hizi zikamfikia mfalme wa Ninewi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake rasmi, akajivika vazi la gunia na kuketi katika majivu.[#3:6 Huyo labda alikuwa mfalme wa Ashuru ambaye ikulu yake ilikuwa huko Ninewi. Kitendo chake kinaonesha kwamba naye pia hayuko nje ya sheria ya Mungu na anapaswa kumtii. Anaamuru watu wake wamwombe Mungu wa Yona ingawaje wao waliabudu miungu mingi.]

7Kisha mfalme akawatangazia wakazi wa Ninewi: “Mimi mfalme, pamoja na wakuu wangu, natoa amri hii: Pasiwe na binadamu yeyote, ng'ombe au mnyama yeyote wa kufugwa, atakayeonja kitu chochote. Ni mwiko kwa mtu yeyote au mnyama kula au kunywa.

8Watu wote na wanyama wavae mavazi ya gunia. Kila mtu na amwombe Mungu na kumsihi kwa moyo. Naam, kila mmoja na aache uovu na ukatili wake.

9Huenda Mungu akabadili nia yake, akaacha kutukasirikia, tusije tukaangamia!”

10Mungu alipoona walivyofanya, na jinsi walivyouacha uovu wao, akabadili nia yake, akaacha kuwatenda kama alivyokuwa amekusudia.[#3:10 Zingatia uhusiano wa aya hii na mafundisho yaliyo katika Yer 18:7-8; 26:3: kama Mungu akiona ishara ya kutubu wakati adhabu inawakabili watu yeye kwa huruma na kwa wingi huwajalia watu msamaha (rejea pia Kut 32:14; 2Sam 24:16; Amo 7:3,6).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania