The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2“Waambie watu wa Israeli hivi: Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
3Kamwe msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Misri ambako mlikaa; wala msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Kanaani ambako nawapeleka. Kamwe msifuate mitindo yao.[#18:3 Waisraeli walikatazwa kufuata mila na desturi mbaya za watu walioishi Kanaani (Mwa 19:1-7; 34:2; 39:1-9; Kut 23:23-24; Eze 16:23-36; Hos 4:9-10).]
4Nyinyi mtafuata maagizo yangu na kuyashika masharti yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
5Kwa hiyo, ili mtu apate kuyaokoa maisha, mnapaswa kuyashika masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
6“Mtu yeyote wa Israeli haruhusiwi kumkaribia mtu wa jamaa yake wa karibu ili kulala naye. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.[#18:6 Mojawapo ya sheria na maagizo ambayo Waisraeli walipewa ni tahadhari za kujamiiana na watu wa jamaa moja, na hivyo kuwatenga na desturi za mataifa mengine kuhusu jambo hilo. Miiko mingine waliyowekewa kuhusu kujamiiana inafanana na miiko ya mataifa na makabila mengine ya eneo hili la Afrika.]
7Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mama yako aliyekuzaa. Usimwaibishe; yeye ni mama yako.
8Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mmoja wa wake zake. Hao ni mama zako.
9Kamwe usilale na dada yako, awe ni dada yako halisi au dada yako wa kambo.
10Kamwe usilale na mjukuu wako, mtoto wa mwanao au binti yako; maana sehemu zao za siri ni kama zako mwenyewe.
11Kamwe usilale na msichana aliyezaliwa na mama yako wa kambo aliyeolewa na baba yako; msichana huyo ni dada yako.
12Kamwe usilale na shangazi yako; kwani huyo ni dada wa baba yako.
13Kamwe usilale na dada wa mama yako; kwani huyo ni mama yako mkubwa au mdogo.
14Kamwe usilale na mke wa baba yako mkubwa au mdogo; huyo ni mama yako.
15Kamwe usilale na mke wa mwanao; huyo ni mkewe mwanao. Kamwe usilale naye.
16Kamwe usilale na mke wa ndugu yako; huyo ni shemeji yako.
17Ukilala na mwanamke, basi, kamwe usilale naye na binti yake, wala wajukuu zake. Hao ni ndugu. Kuwachanganya ni kufanya uovu.
18Kamwe usimwoe dada wa mkeo wakati mke wako yungali hai; hiyo itasababisha ushindani.
19“Kamwe usilale na mwanamke awapo mwezini.
20Kamwe usilale na mke wa jirani yako na hivyo kujitia mwenyewe najisi naye.
21“Kamwe usimtoe mtoto wako yeyote kuwa sadaka kwa mungu Moleki maana kufanya hivyo utalikufuru jina langu mimi Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.[#18:21 Jina hili linafanana na jina la Kiebrania lenye maana ya “mfalme” (melek). Lakini hapa linasikika kama neno lenye maana ya “aibu”. Watu waliwatambika watoto wao kwa huyo mungu Moleki kwa kuwachoma moto kwenye bonde la Hinomu karibu na Yerusalemu. Taz Lawi 20:1-5; Kumb 12:31; 2Fal 16:3; 17:17; 23:10; Yer 7:30-31; 19:2-5; Eze 16:20-21; 20:31.]
22“Kamwe usilale na mwanamume mwenzio kana kwamba ni mwanamke. Hilo ni chukizo.
23Kamwe usilale na mnyama ili usijitie najisi; mwanamume au mwanamke yeyote kamwe asifanye hivyo; kufanya hivyo ni upotovu.
24“Msijitie najisi kwa kufanya mambo hayo kwani kwa sababu ya mambo hayo nayafukuza mataifa yaliyo mbele yenu kwa vile wao hufanya hayo na kujitia najisi.
25Nchi yao ilitiwa unajisi nami nikaiadhibu, nayo ikawakataa wakazi wake.
26Lakini nyinyi na wageni wanaokaa kati yenu ni lazima kuyashika masharti na maagizo yangu na wala msifanye machukizo hayo.
27Machukizo hayo waliyafanya watu waliokaa katika nchi ya Kanaani kabla yenu, nao wakaitia nchi unajisi.
28Basi, nyinyi msifanye mambo hayo, la sivyo nchi hiyo itawatapika kama ilivyolitapika taifa lililokuwa kabla yenu.
29Watu wote watakaofanya mambo hayo ya kuchukiza ni lazima watengwe mbali na watu wao.
30Kwa hiyo shikeni kikamilifu yote ninayowaagiza; msifuate mazoea yoyote ya kuchukiza yaliyofanywa na wale walioishi nchini kabla yenu, msije mkajitia unajisi kwayo. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”