Luka 16

Luka 16

Karani mjanja

1Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake.[#16:1 Sura ya 16 ina mifano miwili ambayo yote ina fundisho moja kuhusu matumizi mema ya mali. Aya 14-18 ina misemo mbalimbali ya Yesu.; #16:1 Huko Palestina ilikuwa kawaida kwa tajiri kumkabidhi wakili wake mamlaka ya kushughulikia mali zake na biashara zake.]

2Yule tajiri akamwita, akamwambia: ‘Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.’

3Yule karani akafikiri: ‘Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu.

4Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.’

5Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmojammoja, akamwambia yule wa kwanza: ‘Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?’

6Yeye akamjibu: ‘Mapipa 100 ya mafuta ya zeituni.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.’

7Kisha akamwuliza mdeni mwingine: ‘Wewe unadaiwa kiasi gani?’ Yeye akamjibu: ‘Magunia 100 ya ngano.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, andika themanini.’

8“Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga.”[#16:8 Yahusu watu ambao wameupokea mwanga wa ujumbe wa Mungu. Katika Efe 5:8 ni Wakristo; hali kadhalika katika 1Thes 5:5.]

9Naye Yesu akaendelea kusema, “Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, wawapokeeni katika makao ya milele.[#16:9 “Wingi” unatumika hapa labda kwa ajili ya kumtaja Mungu ambaye ndiye mwenye kuwapokea, bila kumtaja moja kwa moja (Mat 5:4).]

10Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa.

11Kama basi, nyinyi si waaminifu kuhusu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli?

12Na kama nyinyi si waaminifu kuhusu mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe?

13“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.”[#16:13 Taz Mat 6:24. Kigiriki “Mamona”; jina linalotoka katika lugha ya Kiaramu na lenye maana hiyo ya mali.]

Misemo kadha ya Yesu

(Mat 11:12-13; 5:31-32; Marko 10:11-12)

14Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu.

15Hapo akawaambia, “Nyinyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.[#16:1-15 Mfano huo umesababisha matatizo katika kuufafanua kutokana na namna ya kutenda ya huyo wakili. Kitu ambacho mfano huu unahusikana nacho ni juu ya werevu na ya vitendo vya huyo wakili, si juu ya au wa vitendo vyake.]

16“Sheria na maandishi ya manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohane Mbatizaji. Tangu hapo, ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu.[#16:16 Msemo ambao unatumiwa kutaja Maandiko Matakatifu ambayo sisi tunayataja kama Agano la Kale - (taz Utangulizi wa Agano Jipya).; #16:16 Yaani Yohane Mbatizaji.; #16:16 Tafsiri nyingine yaweza kuwa]

17Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya sheria kufutwa.[#16:17 Mat 5:18; Luka 21:33 neno kwa neno mkato mdogo. Au katika Mathayo “pembe” yaani sehemu ya herufi mbili za Kiebrania iliyojitokeza na kawaida hubainisha herufi hizo na nyingine mbili. Msemo huo wasema juu ya sehemu ndogo kabisa au zisizo muhimu sana za sheria (Mat 5:18).]

18“Yeyote anayempa mkewe talaka na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.[#16:18 Kwa mafundisho mengine kuhusu talaka taz Mat 5:32; 19:9; Marko 10:11-12; 1Kor 7:10-11.]

Tajiri na Lazaro

19“Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku.[#16:19 Neno kwa neno: , yaani mavazi ya kupendeza ambayo yalivaliwa na watawala, wafalme na wakuu.; #16:19 Simulizi pekee ambalo Yesu anatoa na kumtaja kwa jina mmoja wa wahusika yaani Lazaro.]

20Na, mlangoni pa huyo tajiri kulikuwa na maskini mmoja jina lake Lazaro, ambaye alikuwa amejaa vidonda.

21Lazaro alitamani kupewa makombo yaliyoanguka kutoka mezani pa huyo tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kuramba vidonda vyake![#16:21 Wanyama waliofikiriwa na Wayahudi kuwa wanyama duni na najisi (Zab 22:16,20; Meth 26:11; Mat 7:6). Kilele cha maafa na hali duni iliyompata Lazaro ni kwamba yeye mwenyewe hakuwa hata na uwezo wa kuweza kuwafukuza hao mbwa wasimkaribie! Hakuwa na uwezo wa kujikinga nao.]

22“Basi, huyo maskini akafa, nao malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa.[#16:22 Neno kwa neno: , msemo unaonesha nafasi anayopata, yaani, nafasi ya heshima. (Taz Yoh 13:23) na kuona pia jinsi maneno haya yalivyo kinyume cha aya 19-21.]

23Huyo tajiri, akiwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye.[#16:23 Mahali waendapo wanaokufa na ambapo kadiri ya fikira za Wayahudi wa nyakati hizo wafu hukaa humo wakingojea hukumu.]

24Basi, akaita kwa sauti: ‘Babu Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.’

25Lakini Abrahamu akamjibu: ‘Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa.

26Licha ya hayo, kati yetu na nyinyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, na wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.’

27Huyo aliyekuwa tajiri akasema: ‘Basi babu, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu,

28maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.’

29Lakini Abrahamu akamwambia: ‘Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.’[#16:29 Taz Yoh 5:45-47. Maandiko Matakatifu ya A.K. (taz maelezo katika 16:16).]

30Lakini yeye akasema: ‘Sivyo babu Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka kwa wafu na kuwaendea, watatubu.’

31Naye Abrahamu akasema: ‘Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka kwa wafu.’”[#16:31 Agano la Kale kama vile pia Agano Jipya, yote mawili yanafundisha kuwajibika kwa matajiri kuwasaidia maskini (k.m. Yobu 31:16-23; Yak 5:1-6). Kosa la huyo tajiri lilikuwa kutokujali mateso na dhiki ya Lazaro.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania