Luka 3

Mahubiri ya Yohane Mbatizaji

(Mat 3:1-12; Marko 1:1-8; Yoh 1:19-28)

1Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mtawala wa Galilaya, na ndugu yake Filipo alikuwa mtawala wa eneo la Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mtawala wa Abilene,[#3:1 Yapata mwaka wa 28 au 29 B.K. Hapa kama vile katika 1:5 na 2:13, Luka anatoa habari hizo kwa kuziweka katika historia kwa kutaja matukio mengine ya kihistoria ya wakati huo.; #3:1 Alikuwa mtawala mkuu wa Waroma mnamo mwaka 14-37 B.K.; #3:1 Alikuwa gavana wa Kiroma na alitawala Yudea, Samaria na Idumea mnamo 14-37 B.K.; #3:1 Huyu ni yule aitwaye Antipa, mtoto wake Herode Mkuu (taz maelezo ya Mat 2:1). Alikuwa mtawala au gavana (neno kwa neno: au Kiswahili cha zamani kidogo: wa Galilaya na Perea tangu mwaka wa 4 K.K. mpaka mwaka wa 39 B.K.; #3:1 Mtoto mwingine wa Herode Mkuu na Kleopatra wa Misri ambaye alitawala Iturea na Trakoniti kaskazini mwa Galilaya 4 K.K. mpaka 39 B.K.]

2na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane mwana wa Zakaria, kule jangwani.[#3:2 Alikuwa kuhani mkuu mwaka 6-15 B.K.; na chini ya Kayafa mnamo mwaka wa 18-36 B.K. Aliendelea kutajwa kama kuhani mkuu na bila shaka alikuwa na madaraka kiasi kikubwa (ling Yoh 18:13; Mate 4:6).]

3Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani. Akawa anahubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.[#3:3 Tafsiri nyingine: maneno ambayo yanawataka watu waachane na dhambi zao na kumrudia Mungu.]

4Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Sauti ya mtu anaita jangwani:

‘Mtayarishieni Bwana njia yake;

nyosheni barabara zake.

5Kila bonde litafukiwa,

kila mlima na kilima vitasawazishwa;

palipopindika patanyoshwa,

njia mbaya zitatengenezwa.

6Na, watu wote watauona wokovu aletao Mungu.’”[#3:6 Isaya 40:3-5, imenukuliwa hapa kadiri ya tafsiri ya kale ya Kigiriki iitwayo Septuajinta (LXX).]

7Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja?

8Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kujisemea: ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.[#3:8 Linganisha na Yoh 8:33,39 na Rom 2:28-29. Hao watu walikuwa wanasema hivyo kujitakia kuwa wao ni wa pekee na wenye kupendelewa na Mungu kwa kule kuwa tu wazao wa Abrahamu!]

9Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

10Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?”

11Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.”

12Nao watozaushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?”[#3:12 Walikuwa wameajiriwa na utawala wa Roma. Ndiyo maana Wayahudi wengine waliwachukia na kuwaona kuwa wahaini au kwa maneno mengine: wenye dhambi.]

13Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.”

14Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.”

15Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane, kuwa labda yeye ndiye Kristo.

16Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.[#3:16 Hiyo ilikuwa kazi ya chini waliyofanya watumwa.; #3:16 Kama kielelezo au alama au mfano wa hukumu na utakaso; taz aya ya 17 na Isa 31:9; 66:15-16; Zek 13:8-9; Mal 3:2. Ling na pia moto wa Pentekoste (Mate 2:3).]

17Yeye anacho mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka aipure nafaka yake, akusanye ngano katika ghala, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.”[#3:17 Kawaida mavuno ya ngano na nafaka nyingine yaliwekwa mahali pa uwanda halafu baada ya kupigwapigwa watu walirusha masazo yake juu kwa kutumia chombo maalumu ili makapi na takataka nyingine zichukuliwe na upepo na nafaka yenyewe ibaki.]

18Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema.

19Lakini Yohane alimgombeza mtawala Herode, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya.

20Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani.

Yesu anabatizwa

(Mat 3:13-17; Marko 1:9-11)

21Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka,[#3:21 Luka anaanza hapa dhamira yake juu ya sala; na karibu kila mara katika mazingira maalumu katika huduma ya Yesu sala huwapo: 5:16; 6:12; 9:18,28-29; 11:1; 22:41-46; 23:34,46.]

22na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.”[#3:22 Msemo ambao waweza kueleweka pia kama Sehemu nyingine zinazogusia msemo huu: Mat 3:17; 12:18; 17:5; Marko 9:7; Luka 9:35; (ila hapa wazo la kuteuliwa ndilo linalohusika ingawa hati nyingine zina pia); 2Pet 1:17 baadhi ya hati za mkono za kale zina: Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa baba yako (Zab 2:7).]

Ukoo wa Yesu

(Mat 1:1-17)

23Yesu alipoanza kazi yake hadharani alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mtoto wa Yosefu mwana wa Heli.

24Heli alikuwa mwana wa Mathati, aliyekuwa mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yanai, mwana wa Yosefu,

25aliyekuwa mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Hesli, mwana wa Nagai,

26aliyekuwa mwana wa Maathi, mwana wa Matathia, mwana wa Shemeni, mwana wa Yoseki, mwana wa Yuda,

27aliyekuwa mwana wa Yohanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri,

28mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, aliyekuwa mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri,

29aliyekuwa mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri, mwana wa Yorimu, mwana wa Mathati, mwana wa Lawi,

30aliyekuwa mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yosefu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliakimu,

31aliyekuwa mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi,

32aliyekuwa mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni,

33aliyekuwa mwana wa Aminadabu, mwana wa Admini, mwana wa Arni, mwana wa Hesroni, mwana wa Peresi, mwana wa Yuda,

34aliyekuwa mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Abrahamu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori,

35aliyekuwa mwana wa Serugi, mwana wa Reu, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala,

36aliyekuwa mwana wa Kainamu, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Noa, mwana wa Lameki,

37aliyekuwa mwana wa Methusela, mwana wa Henoki, mwana wa Yaredi, mwana wa Mahalaleli, mwana wa Kainamu,

38aliyekuwa mwana wa Enoshi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, aliyekuwa wa Mungu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania