Malaki 4

Malaki 4

Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja

1Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, siku yaja, nayo inawaka kama tanuri. Wenye kiburi na waovu wote watatupwa humo na kuteketea kama mabua makavu; watateketea kabisa pasibaki hata alama.

2Lakini kwa ajili yenu nyinyi mnaonicha, uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake. Mtatoka mkirukaruka kama ndama watokapo zizini mwao.[#4:2 Maneno haya yanahusu ushindi, wokovu na kusimikwa tena uadilifu wa Mungu ambao utathibitisha ushindi wa wema na kulinda haki za wale wanaomwamini (rejea Zab 22:30-31; 40:10; Isa 45:8; 46:13; 51:7-8). Kichwa “Jua la Haki” au “Jua la Uadilifu” kilitumiwa kwa Kristo tangu zamani katika maisha ya kanisa la Kikristo (rejea Luka 1:78; 2:32).]

3Siku hiyo mtawakanyagakanyaga waovu, nao watakuwa kama majivu chini ya nyayo zenu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

4“Kumbukeni sheria, kanuni na maagizo yangu niliyomwamuru Mose mtumishi wangu kule mlimani Horebu, ili awaamuru watu wote wa Israeli.[#4:4 Rejea Kut 19:16-20:20; 24:1-17; Kumb 5:1-3.]

5“Tazama, kabla ya kufika siku ile kuu na ya kutisha, nitamtuma nabii Elia.

6Nabii Elia atawapatanisha wazazi na watoto wao; la sivyo, nitakuja na kuiangamiza nchi yenu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania