Mathayo 13

Mathayo 13

Mfano wa mpanzi

(Marko 4:1-9; Luka 8:4-8)

1Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa.[#13:1-52 Simulizi kuu la tatu la Yesu ambalo lina mafundisho kwa mifano saba kuhusu utawala wa Mungu.; #13:1 (4:18) pwani ya mashariki karibu na Kafarnaumu.]

2Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashuani, akaketi. Watu wote walisimama kwenye ukingo wa ziwa,[#13:2 Taz Mat 5:1 maelezo; Luka 5:1-3.]

3naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano.[#13:3 Namna hii ya kufundisha ni jambo la kawaida katika tamaduni mbalimbali na lasaidia kukazia fundisho linalotolewa lidumu katika kumbukumbu za watu. Mifano hiyo kwa kawaida huwa na tabaka mbili za maana: maana inayotajwa katika hadithi yenyewe (mfano: mpanzi, mkulima anapanda mbegu na matokeo yake), na maana ya pili: ufafanuzi wake (mfano: Mat 13:36-43 ni maana ya 13:24-30). Mifano huchochea ufafanuzi kumfanya mtu ashangae na kujiuliza. Karibu mifano yote ya A.J. yahusu ufalme wa Mungu. Mifano hiyo aghalabu yaambatana sana na nafsi yake Yesu.]

“Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.

4Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.

5Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.

6Jua lilipochomoza, ziliteketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.

7Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga.

8Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini.

9Mwenye masikio na asikie!”

Shabaha ya kusema kwa mifano

(Marko 4:10-12; Luka 8:9-10)

10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.[#13:11 Au, “mafumbo ya ufalme”. Yahusu mipango ya Mungu ambayo sasa inafunuliwa.]

12Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.[#13:12 Wale wanaokubali na kuthamini ukweli waliofundishwa juu ya utawala wa Mungu watapokea zaidi, hali wengine wasiofanya hivyo wataachwa bila chochote (Mat 25:29; Marko 4:25; Luka 8:18; 19:26).]

13Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.

14Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya:

‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa.

Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

15Maana akili za watu hawa zimepumbaa,

wameyaziba masikio yao,

wameyafumba macho yao.

La sivyo, wangeona kwa macho yao,

wangesikia kwa masikio yao,

wangeelewa kwa akili zao,

na kunigeukia, asema Bwana,

nami ningewaponya.’

16“Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia.

17Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.[#13:17 Ling na 1Pet 1:10-12 taz pia Luka 10:23-24.]

Maelezo ya mfano wa mpanzi

(Marko 4:13-20; Luka 8:11-15)

18“Basi, nyinyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi.

19Yeyote asikiaye neno juu ya ufalme wa Mungu bila kuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake.

20Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha.

21Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara.

22Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda.[#13:22 Au “nayo (yaani ile mbegu ya neno la Mungu) haizai matunda”; hapa lakini namna ya kwanza ni dhahiri zaidi kutokana na mpangilio wa mfano wenyewe.]

23Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.”

Mfano wa magugu

24Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

25Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.

26Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.

27Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’

28Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayang'oe?’

29Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang'oa na ngano pia.

30Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’”

Mfano wa mbegu ya haradali

(Marko 4:30-32; Luka 13:18-19)

31Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.[#13:31 Shida hapa ni kwamba mbegu yenyewe si ndogo kuliko mbegu nyingine zote, na mti wake pia hauwi mkubwa kuliko miti yote. Lakini mfano wenyewe wafaa sana kuonesha mwanzo mdogo sana wa ufalme wa Mungu na uenezi wake mkubwa uliofuata baadaye.]

32Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”[#13:32 Eze 17:23; Dan 4:12,21.]

Mfano wa chachu

(Luka 13:20-21)

33Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga madebe mawili na nusu, hata unga wote ukaumuka.”

Kutumia mifano

(Marko 4:33-34)

34Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano,

35ili jambo lililonenwa na nabii litimie:[#13:35 maneno yanayosemwa ni kutoka Zaburi ya 78:2 ambayo ina anwani: “Utenzi wa Asafu”. Katika 2Nya 29:30 Asafu anatajwa kuwa ni mwonaji (pamoja na Daudi).]

“Nitasema nao kwa mifano;

nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.”

Yesu anafafanua mfano wa magugu

36Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.”[#13:36 Yaani nyumba iliyotajwa katika 13:1.]

37Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu.

38Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.

39Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika.

40Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;

41Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu,[#13:41 Au, “vitu vyote vyenye kusababisha dhambi”.]

42na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno.

43Kisha, wale wema watang'ara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie!

Mfano wa hazina iliyofichika

44“Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.[#13:44 Picha tunayopewa katika mfano huu na ule wa 13:45-46 inaashiria bei na thamani kuu ya utawala wa Mungu kwa wale wanaotaka kuupata.]

Mfano wa lulu

45“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri.

46Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.

Mfano wa wavu wa samaki

47“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina.[#13:47-50 Huu mfano, kama vile ule mfano wa magugu (13:23), wasisitiza hali ya kuishi pamoja watu wema na wabaya mpaka mwisho wa nyakati, yaani mpaka siku ya mwisho ya hukumu.]

48Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.

49Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema,

50na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.”

Hazina mpya na ya kale

51Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.”

52Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.”[#13:52 Yahusu mwalimu wa sheria ambaye amejifunza juu ya sheria ya Mose lakini pia anajifunza juu ya utawala wa Mungu na kujua kufundisha huo mpya bila kutupilia mbali kilicho cha thamani katika ile sheria ya kale.]

Yesu anakataliwa huko Nazareti

(Marko 6:1-6; Luka 4:16-30)

53Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo,[#13:53 Taz Mat 7:28 maelezo.]

54akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu?[#13:54 Yaani Nazareti; taz 2:23 (taz pia Luka 4:16,23).]

55Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?[#13:55-56 Taz Mat 12:46 maelezo.]

56Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?”

57Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!”[#13:57 Msemo wa namna ya kitendawili (Marko 6:4; Luka 4:24; Yoh 4:44).]

58Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania