The chat will start when you send the first message.
1Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.[#16:1 Yaani kutoka kwa Mungu na hivyo kuonesha kwamba Yesu anacho kibali cha Mungu (taz Mat 12:38; Marko 8:11; Luka 11:16; Yoh 6:30).]
2Lakini Yesu akawajibu, “Ikifika jioni nyinyi husema: ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!’[#16:2-3 Maneno ya Yesu katika aya hizi yameachwa na baadhi ya hati na tafsiri kadhaa za kale. Yesu anawalaumu viongozi wa dini kwa kutoweza ama kutotaka kwao kutambua ishara au miujiza ya Yesu (Mat 11:4-5) ambayo inaashiria kuwasili kwa ufalme wa mbinguni.]
3Na alfajiri mwasema: ‘Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!’ Basi, nyinyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia hali ya anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.
4Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake.[#16:4 Mat 12:39; Luka 11:29; rejea Yona 3:3-5.]
5Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate.
6Yesu akawaambia, “Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”[#16:6 Chachu inaelezwa katika 16:12 (na pia Luka 12:1). Kwa jumla neno “chachu” linatumiwa hapa kama mfano wa nguvu mbaya inayoathiri vitu au hali, kisirisiri, yaani bila kufichuliwa kwa urahisi (1Kor 5:6-7; Gal 5:7-9).]
7Lakini wao wakawa wanajadiliana: “Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate.”
8Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?
9Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu 5,000? Je, mlijaza vikapu vingapi vya mabaki?
10Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu 4,000, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.
11Mbona hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”
12Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
13Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?”[#16:13 Mji wa Kiroma, kaskazini ya bahari ya Galilaya, eneo la watu wasio Wayahudi.; #16:13 Jina la sifa ambalo Yesu analitumia kujitaja yeye mwenyewe. Taz pia Orodha ya Maneno.]
14Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.”[#16:14 Nabii aliyeishi nyakati za mfalme Ahabu (1Fal 17; 2Fal 2). Wayahudi walimtazamia arudi tena kutangaza kuwasili Siku ya Bwana (Mal 4:5-6).]
15Yesu akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?”
16Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”[#16:16 Katika 3:17 sauti kutoka mbinguni inamtaja Yesu kama “Mwanangu mpendwa” na katika 14:33 wanafunzi wanakariri: “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu”. Walakini msemo huo unatajwa hapa kikamilifu na haupatikani namna hiyo popote katika A.J. Katika A.K. msemo “Mwana wa Mungu” unatumiwa kwa watu ambao Mungu aliwateua kufanya kitu kwa niaba yake. Hapa msemo huo waonesha Yesu alitoka kwa Mungu na anao uhusiano wa pekee na Mungu.]
17Yesu akasema, “Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufunulia jambo hili, ila Baba yangu aliye mbinguni.[#16:17 Neno hili latumika kutafsiria maneno mawili ya Kigiriki: “sarks” (nyama), na “haima” (damu), maneno ambayo yatumika kumtaja binadamu na utu wake wote.]
18Nami nakuambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala nguvu za kifo hazitaweza kulishinda.[#16:18 Kigiriki ni “Petros”, jina ambalo limetokana na “Petra” yaani mwamba (taz Mat 7:24-25 ambapo neno mwamba linatumika). Mara nyingi Simoni anatajwa kwa jina la Kiaramu “Kefa” (rejea Yoh 1:42; 1Kor 1:12; Gal 2:9) ambalo lina maana ya “jiwe” na pia “mwamba”.; #16:18 Neno la Kigiriki ni “eklesia”. Katika Injili zote nne, linatumiwa hapa tu na katika Mat 18:17; lakini linatumiwa mara nyingi katika vitabu vingine vya Agano Jipya. Neno lenyewe lina maana ya jumuiya mpya ya watu wa Mungu ambayo imesimikwa na Yesu Kristo.; #16:18 Tafsiri ya neno kwa neno: “milango ya kuzimu”, kuzimu kukiwa mahali pa wafu na “milango” likitumika kama kifano cha uwezo au nguvu zake (taz Yobu 38:17). Neno “ufunguo” linatumika kama ishara ya uwezo na mamlaka au madaraka ya msimamizi wa jamaa ya jumba la kifalme ya kufungua na kufunga, labda kwa kugusia wazo lililopo katika Isa 22:15-25. Maneno “kufunga” na “kufungua” yalitumika pia kwa maana ya kuruhusu na kuzuia.]
19Nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni.”
20Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.[#16:20 Taz Marko 1:34 maelezo.]
21Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake kwamba ni lazima aende Yerusalemu, na huko kupata mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba, atauawa na siku ya tatu atafufuliwa.[#16:21 Mat 17:22-23; 20:17-19. Taz pia Marko 8:31—9:1 maelezo.]
22Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: “Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!”
23Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu!”[#16:23 Hapa Yesu anaona kwamba majaribu ya Shetani kuhusu kazi yake Yesu yataendelea (rejea Mat 4:10).]
24Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.[#16:24 Taz maelezo katika Mat 10:38; rejea pia Luka 14:27; 17:33; Yoh 12:24-25.]
25Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza;[#16:25-26 Neno la Kigiriki “psukhe” laweza kuwa na maana ya “roho”, “uhai” au “nafsi”; taz 10:28. Hutumika mara nyingi badala ya viwakilishi; “mimi”, “wewe”, n.k. kwa maana ya mtu binafsi. Msemo wenyewe karibu ni kitendawili cha hali ya Kikristo; kupoteza nafsi yako (aya 6) ni sawa na kujikatalia wewe mwenyewe kama inavyosemwa wazi katika Luka 9:25.]
26lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?
27Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.[#16:27 Mat 25:31.]
28Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika ufalme wake.”[#16:28 Tamko hili la Yesu limepata kufafanuliwa kwa namna mbalimbali: Yahusu (a) kuja kwake mara ya pili, kuja ambako wakristo wa kwanza walitazamia kufanyike wakiwa bado hai; (b) kutukuzwa kwake Yesu, yaani kifo na ufufuo wake (Luka 24:6; yoh 12:23; 13:31-32; Mate 3:13) au, (c) kugeuka sura kwa Yesu, jambo ambalo linasimuliwa katika sehemu ifuatayo.]