The chat will start when you send the first message.
1Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu.
2Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, uso wake ukang'aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga.[#17:2 Neno la Kigiriki linalotafsiriwa mahali pengine linatumika juu ya mabadiliko ya kiroho (Rom 12:2; 2Kor 3:18). Hapa mabadiliko hayo ni mabadiliko yaonekanayo kwa macho. Lugha inayotumiwa hapa ni ya kimfano; ilikuwa vigumu kwa waandishi kueleza hali Yesu ilivyokuwa kweli wakati huo, ling 2Pet 1:16,18. Kugeuka kwa sura yake Yesu kwadokezea utukufu wake wa baadaye, baada ya kufufuka (taz pia Marko 9:2-8; Luka 9:28-38; 2Pet 1:16).]
3Mose na Elia wakawatokea, wakawa wanazungumza naye.[#17:3 Hawa wanaonekana hapa si tu kwa kuwa wao ni manabii au kama mashahidi wa Agano ila pia kwa vile wao walichukuliwa kama watangulizi wa Masiha. Picha nyingine tunayopata ni kwamba Mose anatokea kama mhusika katika utoaji wa sheria (taz Kut 20:1—Kumb 5; Mate 7:35-37) naye Elia kama nabii aliyepaa na aliyetazamiwa kurudi (Mal 4:5-6).]
4Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.”
5Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka hilo wingu: “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni.”[#17:5 Mara nyingi katika A.K. wingu liliambatishwa na kuweko au kutokea kwa Mungu: rejea Kut 16:10; 33:9-10; 40:34-38; 1Fal 8:10-11.; #17:5 Mwa 22:2; Zab 2:7; Isa 42:1; Mat 3:17; 12:18; Marko 1:11; Luka 3:22. Kuhusu maneno: “Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye”, taz Mat 3:17 maelezo. Na neno “msikilizeni” linatukumbusha Kumb 18:15.]
6Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana.
7Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, “Simameni, msiogope!”
8Walipoangalia juu hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake.
9Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: “Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu.”[#17:9 Taz Marko 1:34 maelezo.]
10Kisha wanafunzi wakamwuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?”
11Yesu akawajibu, “Kweli, Elia atakuja kutayarisha mambo yote.
12Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao.”[#17:12-13 Mat 11:14 maelezo. Yesu anaona kwamba unabii wa Mal 4:5 ulikamilika katika nafsi yake Yohane Mbatizaji.]
13Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane Mbatizaji.
14Walipoufikia tena ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti,
15akasema, “Bwana, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini.[#17:15 Waandishi wote wa sunoptiki wanaambatisha ugonjwa huo na pepo mbaya (taz pia Marko 9:17-29; Luka 9:39).]
16Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.”
17Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia nyinyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto.”
18Basi, Yesu akamkemea huyo pepo, naye akamtoka, na yule mtoto akapona wakati huohuo.
19Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?”
20Yesu akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, iwe ndogo hata kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: ‘Toka hapa uende pale,’ nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu.”[#17:20 Taz 6:30.; #17:20 Mat 21:21; Marko 11:23; Luka 17:6; 1Kor 13:2. Kuhusu matumizi ya mbegu ya haradali katika maandishi haya taz Mat 13:31 maelezo.; #17:20 Namna au Mtindo huu wa kusema karibu ni kama kitendawili ambacho chatumika kwa maana ya kufanya kitu ambacho ni kigumu mno au kisichowezekana (rejea Zek 4:7).; #17:20 Baadhi ya hati nyingine za kale za Injili ya Matayo zina aya 21: “Pepo wa namna hii hawezi kuondelewa ila kwa sala na kufunga.” Taz Marko 9:29.]
22Walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu.
23Watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika mno.
24Walipofika Kafarnaumu watu wenye kukusanya fedha ya zaka ya hekalu walimwendea Petro, wakamwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa fedha ya zaka?”[#17:24 Neno la Kigiriki hapa ni “didrakhma”. Ilitakiwa ilipwe mara moja kwa mwaka kwa ajili ya huduma ya hekalu. Waisraeli wote, hata wale walioishi nje ya Palestina walitakiwa kulipa zaka hiyo (taz Kut 30:11-19). Thamani ya zaka hiyo ilikuwa karibu mshahara wa siku mbili wa kibarua nyakati hizo za kale.]
25Petro akajibu, “Naam, hulipa.” Basi, Petro alipoingia ndani ya nyumba, kabla hata hajasema neno, Yesu akamwuliza, “Simoni, wewe unaonaje? Wafalme wa dunia hukusanya ushuru au kodi kutoka kwa kina nani? Kutoka kwa wananchi ama kutoka kwa wageni?”
26Petro akajibu, “Kutoka kwa wageni.” Yesu akamwambia, “Haya basi, wananchi hawahusiki.
27Lakini kusudi tusiwakwaze, nenda ziwani ukatupe ndoana; chukua samaki wa kwanza atakayenaswa, fungua kinywa chake, na ndani utakuta fedha taslimu ya zaka. Ichukue ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”