Mathayo 19

Mathayo 19

Kuhusu talaka

(Marko 10:1-12)

1Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda Yudea, ng'ambo ya mto Yordani.[#19:1 Taz maelezo ya namna hii ya kusema katika Mat 7:28.; #19:1 Yaani upande wa mashariki wa mto Yordani.]

2Watu wengi walimfuata huko, naye akawaponya.

3Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, “Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?”[#19:3 Ionekanavyo swali lenyewe na jinsi lilivyowekwa linaonesha kulikuwa na mgawanyiko kuhusu namna ya kufafanua sheria ya Kumb 24:1.]

4Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke,

5na akasema: ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?’

6Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe.”

7Lakini wao wakamwuliza, “Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?”

8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

9Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini.”[#19:9 Taz Mat 5:32 maelezo; rejea pia Luka 16:18. Taz pia Mal 2:13-16; Marko 10:11-12; 1Kor 7:10-13.]

10Wanafunzi wake wakamwambia, “Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa.”

11Yesu akawaambia, “Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu.

12Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee.”[#19:12 Yahusu mazingira ya pekee ambayo yanawahusu watu fulani tu. Taz pia 1Kor 7:6-9.]

Yesu anawabariki watoto wadogo

(Marko 10:13-16; Luka 18:15-17)

13Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea.

14Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.”[#19:14 Kuhusu “watoto wadogo” taz maelezo ya Mat 18:3.]

15Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.

Kijana tajiri

(Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)

16Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?”

17Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.”

18Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo,

19Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”

20Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia; nifanye nini zaidi?”

21Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako, uwape maskini fedha hiyo, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.”[#19:21 Neno hili katika Mathayo latumika tu katika 5:48 ambapo latumiwa kuhusiana na jinsi ya kuwapenda jirani. Hapa, kuwa mkamilifu ni sawa na kutimiza kabisa matakwa ya Mungu ambayo yamo katika kumfuata Kristo. Taz Mat 5:48.]

22Huyo kijana aliposikia hayo, akaenda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.

23Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.[#19:23-29 Mwishoni mwa majibizano na huyo kijana tajiri, Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba ni vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni (aya 23-24). Wanafunzi walishangaa (aya 25) kwani walifikiri utajiri ni ishara ya kukubaliwa na Mungu. Katika aya ya 26 Yesu anakabili mshangao wa hao wanafunzi.]

24Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”[#19:24 Msemo namna ya kitendawili kuelezea jambo lisilowezekana (aya 26).]

25Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?”

26Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”

27Kisha Petro akasema, “Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?”

28Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti chake cha enzi kitukufu katika ulimwengu mpya, nyinyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.

29Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uhai wa milele.

30Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania